ABUJA, NIGERIA
RAIS Muhammadu Buhari (76) ameshinda majimbo mawili ya kwanza kati ya 36, kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) iliyoanza kutangaza matokeo ya uchaguzi yaliyocheleweshwa jana.
Hayo yamekuja huku matokeo ya uchaguzi yakilalamikiwa kwa kuchelewa kutangazwa, huku pia kukitokea machafuko yaliyosababisha vifo vya watu 40.
INEC ilitangaza jana kuwa Buhari alimshinda mpinzani wake mkuu Makamu Rais wa zamani Atiku Abubakar (72) katika Jimbo la Ekiti kwa asilimia 58 ya kura.
Kwa mujibu ya matokeo yaliyokuwa yakiendelea kutangazwa jana jioni, Buhari aliyepoteza jimbo hilo miaka minne iliyopita, pia alishinda Jimbo la Osun kwa asilimia 49 dhidi ya 47 za mpinzani wake huku akielekea kulitwaa Jimbo la Lagos.
Watu milioni 73 walikuwa wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo wenye ushindani mkali baina ya Buhari na Abubakar ambaye pia ni mfanyabiashara mashuhuri.
INEC inaweza kuchukua siku moja au mbili kukamilisha kutangaza matokeo yote na itategemeana na mwitikio wa wapigakura, ambao walikuwa chini ya asilimia 44 miaka minne iliyopita wakati Buhari alipokuwa mgombea wa kwanza wa upinzani kuchaguliwa kuwa rais katika historia ya taifa hilo kubwa la Afrika Magharibi.
Kwa mujibu wa waangalizi ambao wamesikitishwa na kuchelewa kutangazwa kwa matokeo, watu 40 wameuawa katika machafuko yanayohusiana na uchaguzi huo.
Jeshi la Polisi ambalo halikutoa idadi ya vifo, limesema watu 126 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali ikiwamo kukwapua masanduku ya kura.
Aidha Mwenyekiti wa INEC, Mahmood Yakubu alisema mfanyakazi mmoja wa tume hiyo ameuawa kwa risasi katika Jimbo la Rivers, ambako taarifa zisizo rasmi zilisema Atiku anaongoza kushinda maeneo mengi.
Kushinda urais, mgombea anatakiwa kupata wingi wa kura na angalau asilimia 25 ya theluthi mbili ya majimbo 36 na eneo la mji mkuu wa shirikisho.
Iwapo hakuna atakayefikia kiwango hicho kutafanyika duru la pili.