24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ubora wa vyakula, dawa, udhibitiwe kabla haujamfikia mlaji – Dk. Chaula

VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), imetakiwa kuhakikisha inaendelea kuimarisha mifumo yake ya ufuatiliaji na udhibiti wa ubora wa bidhaa za vyakula na dawa kabla hazijamfikia mtumiaji.

Agizo hilo lilitolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Zainab Chaula,  alipofungua mafunzo ya siku tano kwa wataalam wa TFDA, Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) na Mamlaka ya Malawi.

Dk. Chaula aliipongeza mamlaka hiyo kwa  kutambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa miongoni mwa nchi 50 sawa na asilimia 26 kati ya nchi 194 zenye mifumo imara ya udhibiti wa bidhaa hizo.

“Hii inamaanisha mifumo ya udhibiti Tanzania inatambulika duniani kote na kwamba misingi ya udhibiti ya mamlaka yetu imefikia ngazi ya  mataifa.

“WHO imetutambua na imetupa level (daraja) la tatu, hii ni hatua nzuri, TFDA imefanya kazi kubwa.

“Lakini pamoja na hatua hiyo lazima iendelee kujiimarisha ikiwezekana tupande daraja tufikie level 4 ambayo ndiyo kiwango cha juu zaidi.

“Ili tuweze kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi, mamlaka yetu inapaswa kutengeneza mifumo ya ufuatiliaji ubora na usalama wa bidhaa kuanzia viwandani hadi kwa mtumiaji kuhakikisha hakuna dawa bandia zinaingia nchini mwetu” alisema.

Akiwasilisha mada katika semina hiyo, Mtaalam wa Udhibiti wa Madawa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO-Uswisi), Dk. Alireza Khadem Broojerdi,   alisema ili kuongeza nguvu ya udhibiti nchi zinapaswa kushirikiana kwa ukaribu.

“Tunayo malengo 17 ya dunia (SDGs), lengo namba tatu linasisitiza juu ya afya bora kwa wote, tunayo pia malengo ya mwaka 2019- 2030.

“Mpaka sasa nchi 50 ikiwamo Tanzania sawa na asilimia 26 zimefikia daraja la tatu na nne.

“Nchi 45 sawa na asilimia 23 zipo daraja la pili, nchi 96 zimefikia daraja la kwanza na nyingine zilizobaki bado hazijafikia viwango hivyo,” alisema.

 Kaimu Mkurugenzi wa TFDA, Dk. Candida Shirima alisema kupitia semina hiyo iliyoandaliwa na WHO, watajifunza mbinu mbalimbali  zitakazowasaidia kufikia malengo waliyojiwekea katika kuendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti wa bidhaa hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles