Serikali ya Brazil imeisamehe Tanzania deni la zaidi ya Sh bilioni 445, lilitokana na mkopo uliotolewa kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Morogoro-Dodoma, mwaka 1979.
Deni hilo ambalo ni pamoja riba lilikuwa ni Dola za Marekani milioni 203, deni lililoifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zenye madeni sugu zinazodaiwa na Brazil.
Kwa mujibu wa tarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkataba wa kusamehewa kwa deni hilo, umesainiwa mwishoni mwa wiki hii nchini Brazil na Balozi wa Tanzania nchini humo, Dk. Emmanuel Nchimbi kwa niaba ya Serikali.
Akisaini mkataba huo, Balozi Nchimbi alishukuru Serikali ya Brazil kwa Msamaha huo ambao alisema umeunga mkono jitihada za Rais John Magufuli, kujenga uchumi imara wa Tanzania.
“Pamoja na mambo mengine, napenda niwahakikishie Serikali ya Brazil utayari wa Tanzania katika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uchumi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Serikali ya Brazil ilitamka rasmi kufunguliwa kwa milango ya ushirikiano wa kifedha na kibiashara iliyokuwa imefungwa kutokana na deni hilo ambapo kuanzia sasa kampuni za Brazil zinaruhusiwa kutekeleza miradi nchini lakini pia Serikali ya Tanzania inaruhusiwa kuanzisha majadiliano ya miradi mipya ya maendeleo.