23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Brazil kuboresha kilimo cha pamba Tanzania

AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

BAADA ya Tanzania kupata uhuru kutoka kwa wakoloni wa Uingereza mwaka 1961, mazao makuu ya biashara yalitajwa kuwa ni pamba, tumbaku, kahawa, pareto, katani, korosho na ufuta.

Katika hali isiyoeleweka, miaka ya 90 baadhi ya mazao hayo yalipoteza mwelekeo na mengi kati ya hayo yakawa hayana mchango wa maana katika pato la Taifa na kwa wakulima.

Sasa hivi mazao yanayoongoza ni korosho, karafuu, mbogamboga, maua na maharage kijani na parachichi, n.k.

Pamba limekuwa zao la biashara nchini kwa muda mrefu, hata hivyo zao hilo linakumbwa na changamoto nyingi katika uzalishaji hali inayowakatisha tamaa wakulima.

Pamba hulimwa na wakulima wadogo katika mikoa 15 na wilaya 46 za Tanzania Bara na Kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Mara, Geita, Kigoma, Kagera, Tabora na Singida hulimwa  kwa asilimia 95.

Pia, pamba inalimwa katika Kanda ya Mashariki yenye mikoa ya Iringa, Morogoro, Kilimanjaro, Pwani, Manyara na Tanga wakati zao hilo likiwa limezuiwa katika Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Mbeya, Songwe, Ruvuma, Katavi na Mtwara kutokana na athari za funza mwekundu (Diparopsis castanea) na hivyo kunyima kipato kwa wakulima wa huko wakati imethibitika kila zao linashambuliwa na wadudu ikiwamo kahawa, korosho na ufuta, lakini hayajafungiwa. Wadadisi  wanahoji kwanini wakulima wa mikoa ya kusini wanaonewa?

Kwa wastani uzalishaji wa pamba nchini upo chini sana kwani hekta moja hutoa kati ya kilo 750 hadi 800, wakati nchi ya Burkina Faso inayotumia teknolojia ya uhandisi jeni (genetic engineering) hutoa hadi kilo 2,900 kwa hekta.

Hivi karibuni Tanzania na Brazil ziliingia makubaliano ya kuinua kilimo cha pamba ili kiwe na tija kwa wakulima nchini.

Makubaliano hayo yamejiri wakati ambapo Brazil ipo katika hatua kubwa za kimageuzi ya kilimo, huku ikiwa na mafanikio makubwa katika sekta hiyo ambapo unatekelezwa katika nchi tatu za Burundi, Kenya na Tanzania.

Mradi wa kuinua kilimo cha pamba unaotekelezwa na Brazil nchini Tanzania utajikita zaidi katika kuhakikisha wakulima nchini wanapata pamba za mbegu bora na uzinduzi wa utafiti utamfikia mkulima ili aweze kuongeza tija.

Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa, aliyasema hayo  baada ya kutembelea na kukagua mashamba ya mfano wa kilimo cha pamba katika kituo cha Utafiti TARI-Ukiriguru mkoani Mwanza.

Bashungwa anasisitiza kuwa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli imedhamiria kwa kauli moja kuimarisha sekta ya kilimo, huku katika zao la pamba imejipanga kuhakikisha inazalisha mbegu vipara za pamba zitakazotosheleza kwa wakulima wote nchini na kuondokana na utumiaji wa pamba manyoya ambayo imezoeleka, lakini tija yake ni ndogo katika uzalishaji kuliko pamba manyonya.

Anasema Wizara ya Kilimo itakuwa na jukumu la kushawishi wawekezaji ili kuwekeza kwenye viwanda vya pamba na nyuzi pamoja na viwanda vya nguo na kufanya hivyo tutakuwa tumetekeleza vyema maelekezo yaliyoainishwa kwenye ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020.

Anasema Serikali pia imejipanga kupanua maabara za utafiti wa zao la pamba ili kuimarisha ufanisi na tija ya zao hilo kwani mafanikio ya kilimo yanategemea zaidi katika utafiti.

Bashungwa anaishukuru Serikali ya Brazil kwa utekelezaji wa mradi huo nchini Tanzania ambao unatokana na mahusiano mazuri kati ya nchi hizo mbili inayoakisi katika kufungamanisha kilimo na uchumi wa viwanda.

Anasema Serikali tayari imeanzisha vituo viwili vya kuzalisha mbegu za pamba aina ya vipara katika Mkoa wa Simiyu pamoja na Mkoa wa Tabora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles