27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 4, 2023

Contact us: [email protected]

Bongo ilivyovunja kibabe rekodi ya Uganda JAMAFEST

Christopher Msekena

MWAKA 2017, katika viwanja vya Kololo  Ceremonial jijini Kampala, Uganda, watu zaidi ya 46,000 walishuhudia tamasha la tatu la Jumuiya ya Afrika Mashariki Utamaduni (JAMAFEST).

Mamia ya wasanii na wana utamaduni kutoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani ya Kusini na Tanzania walipata nafasi ya kuonyeshana makali katika sekta hizo.

Tamasha la JAMAFEST  ambalo hufanyika kila baada ya miaka miwili lilianzishwa mwaka 2013 huko Rwanda na likafanyika kwa mara ya pili jijini Nairobi, Kenya na msimu wa tatu ukafanyika Uganda, nchi ambayo ilikuwa inashikilia rekodi ya watu wengi zaidi kuhudhuria.

Habari njema ni kwamba, Tanzania imefanikiwa kuvunja rekodi  ya Uganda kwa tamasha la JAMAFEST kuhudhuliwa na watu wengi zaidi toka lililopozinduliwa Jumapili iliyopita na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan katika  Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Tamasha hilo ambalo linatarajia kuhitimishwa kesho limefanikiwa kuvuka matarajio yaliyowekwa. Wwanamuziki wa aina zote za muziki, wasanii wa sanaa za maonyesho na ufundi pamoja na mashabiki walikutana pamoja.

Akizungumza na Swaggaz jana Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Maelezo, Rodney Mbuya alisema mwamko umekuwa mkubwa katika tamasha hilo na Tanzania imefanikiwa kuvunja rekodi ya Uganda kwa JAMAFEST kuhudhuriwa na watu zaidi ya 80,000 toka kuzinduliwa kwake.

“Mpaka sasa ni zaidi ya watu 80,000 wameshuhudia hili tamasha kwa wale wanaohudhuria Uwanja wa Taifa na bado tuna siku mbili mbele (leo na kesho), kwahiyo idadi ya watu inaweza kuongezeka zaidi.

“Mara nyingi nyakati za jioni ndiyo watu wengi huwa kwenye tamasha, wakishatoka makazini wanakuja kuburudika kwahiyo tumevunja rekodi, tupo vizuri sana,” anasema Mbuya.

Tamasha hilo lilipofanyika Uganda mwaka 2017, wasanii nyota wa kizazi kipya walijitokeza kwa wingi kutumbuiza na hali kadharika hapa Tanzania ndani ya siku sita mfululizo wasanii wa Bongo Fleva wamekuwa wakitumbuiza.

Rodney Mbuya anasema sababu za wasanii wa Bongo Fleva kupewa nafasi ya kutumbuiza katika tamasha hilo ni mpango wao wa kuchanganya  aina zote za sanaa zionekane.

 “ ’Impact’ ya wasanii wa Bongo Fleva imeonekana sababu wasanii wake wameleta watu wengi na mara nyingi huwa wanatumbuiza jioni lakini katika upande wa kuwashirikisha, unajua muziki wowote ni sanaa na hili ni tamasha la sanaa na utamaduni kwahiyo hatukutaka tuache aina fulani ya wanamuziki ili watu wapate ladha tofauti,” anasema.

Kwa siku tofauti tofauti, mastaa wa Bongo Fleva walikonga nyoyo za maelfu ya watu waliohudhuria JAMAFEST, mwaka huu.

Miongoni mwa maonyesho ya wasanii wa kizazi kipya yaliyokuwa na mvuto wa aina yake ni shoo ya Diamond Platnumz, iliyofanyika siku ya ufunguzi na akafanikiwa kusepa na kijiji kwa burudani.

Nyota huyo ambaye alitii wito wa Waziri mwenye dhamana na sanaa Dk. Harrison Mwakyembe uliomtaka kushiriki kwenye JAMAFEST, alitumbuiza katika tamasha hilo asubuhi saa chache baada ya kutoka Iringa alipokuwa na onyesho la Wasafi Festival.

Diamond maarufu kwa jina la Mondi alitua katika Uwanja wa Uhuru akiwa na walinzi binafsi wapatao 12, ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya ile iliyozoeleka jambo lililoongeza mvuto zaidi kwa mashabiki waliomshangilia mwanzo mwisho.

Wasanii wengine  waliotumbuiza ni Barnaba Classic, Marioo, Dj D  Ommy, Jux, G Nako, Joh Makini, Mbosso, Enock Bella, Navy Kenzo, County Boy, TMK Wanaume Family, Sinaubi Zawose, Maua Sama, Ben Pol, mwimbaji wa Injili Joel Lwaga huku Rayvanny na Ruby wakitarajiwa kutumbuiza kesho Jumapili.

Mbali na wasanii wa Tanzania kufanya vizuri katika tamasha la JAMAFEST, makundi ya ngoma za asili na wabunifu wa sanaa za ufundi kutoka Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani ya Kusini na kundi la vichekesho la Vitimbi kutoka Kenya walinogesha onyesho hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles