22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

Biteko aipongeza GGML kwa kuwezesha kongamano TMIF, awaita wawekezaji

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

NAIBU Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kuja nchini kuwekeza katika sekta ya madini kutokana na mazingira rafiki yanayoendelea kuwekwa kwa wawekezaji hao ili kufaidisha pande zote.

Pia ameipongeza Kampuni ya AngloGold Ashanti – GGML kwa kufadhili kongamano la Kimataifa la Madini na Uwekezaji 2023 (TMIF) ambalo linafanyika kwa siku mbili kuanzia Oktoba 25-26, jijini Dar es Salaam.

Makamu Rais wa AngloGold Ashanti anayesimamia miradi endelevu Afrika, Simon Shayo.

Dk. Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati ametoa kauli hiyo leo Jumatano Oktoba 25, 2023 kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati akifungua kongamano hilo ambalo limeshirikisha wadau zaidi ya 2,000 kutoka ndani ya nje ya nchi.

Amesema Serikali imeamua kuuboresha kongamano hilo ili liwe na hadhi ya kimataifa kwa lengo la kukuza sekta ya madini nchini jambo ambalo pia limeungwa na wadau wa sekta hiyo ikiwamo GGML.

Amesema ili kupata taarifa za kijiolojia Serikali imepanga kufanya utafiti kwa teknolojia ya kisasa “High Resolution Airborne Geophysical Survey” katika eneo kubwa zaidi nchi nzima ifikapo mwaka 2030.

“Upatikanaji wa taarifa za kijiolojia katika maeneo mengi ya nchi yetu utahamasisha kasi ya uwekezaji katika utafutaji wa kina wa madini nchini ambao ndio msingi mkubwa wa uanzishwaji wa migodi.

“Niwaase wote mliopo hapa kushiriki kwenye uvunaji madini kwa kuangalia masilahi ya nchi yetu na watu wetu. Bado tunakabiliwa na changamoto za taarifa za kijiolojia katika maeneo ya mengi hivyo Serikali imeamua kuwekeza kwenye utafiti wa hali ya juu ili kujua uwepo wa mashapo ya madini na kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde naye amesema ugunduzi wa mashapo utapelekea kufunguliwa kwa migodi zaidi hapa nchini na kuongeza mapato ya serikali na ajira kwa Watanzania.

“Hakutakuwa na urasimu litakapokuja suala la uwekezaji kazi yetu ni kuwawekea mazingira rafiki ili kuwe na faida kwa pande zote,” amesema.

Aidha, akizungumza katika kongamano hilo lililokuwa na mada zinazohusuhu umuhimu wa madini ya kimkakati, Makamu Rais wa AngloGold Ashanti anayesimamia miradi endelevu Afrika, Simon Shayo alibainisha mikakati mbalimbali ambayo kampuni hiyo imechukua kulinda mazingira.

Alisema GGML ni kampuni ya kwanza kuwekeza kwenye teknolojia za hali ya juu ya uchimbaji madini nchini hali inayoiwezesha kampuni hiyo kuzingatia kipaumbele cha afya na usalama maeneo ya kazi.

Ameaema kampuni hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2000 hapa Tanzania, imeboresha teknolojia hizo hali iliyoifanikisha GGML kushinda tuzo ya afya na usalama mahali pa kwaza kwa mara nne mfululizo na kuzibwaga nchi mbalimbali duniani ambako AngloGold Ashanti inamiliki migodi.

Ametoa mfano kuwa katika kuenenda na mpango wa Tanzania na dunia kupunguza hewa ukaa, kampuni hiyo ilisimika mtambo wa kuchenjua kaboni kutokana na shughuli hizo za uchimbaji. Pamoja na mambo mengine alisema kampuni hiyo imetumia zaidi ya asilimia 75 ya matumizi yake kununua bidhaa kwa wazabuni nchini ili kutekeleza matakwa ya mabadiliko ya sheria ya madini.

Amesema GGML kupitia mpango wa uwajibika wa kampuni kwa jamii (CSR), imewawezesha wananchi wanaozunguka mgodi huo mkoani Geita kupata huduma ya maji kwa zaidi ya asilimia 70. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles