29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaahidi mazingira bora kwa wawekezaji sekta ya madini

*Zanzibar nayo kuanzisha Utalii wa Madini

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Serikali imeahidi kuwa itaendelea kuimarisha mazingira bora na rafiki ya uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini ili kuchochea mchango wake katika pato la taifa.

Hayo yamebinishwa Dar es Salaam leo Jumatano Oktoba 25, 2023 na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko alipomwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Jukwaa la Madini na Uwekezaji Tanzania 2023 jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

Dk. Biteko amesema kuwa Sekta ya Madini inafungamanishwa na Sekta nyingine za Kiuchumi kama vile viwanda na kilimo ili kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotumia madini kama malighafi mfano mbolea, betri za magari, simu, kompyuta na bidhaa nyingine.

“Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa lengo mahususi la kuvutia uwekezaji zaidi kwenye nyanja hii, haya yote ni kutokana na umuhimu wa sekta hii katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.

“Pamoja na ahadi hiyo ya Serikali lakini wote ni mashahidi kuwa mazingira ya uwekezaji katika sekta ya madini nchini yameendelea kuboreshwa na kuwa rafiki, hadi sasa jumla ya kampuni tisa za Kimataifa za uchimbaji mkubwa wa madini zimeingia ubia na Serikali katika uchimbaji wa madini mbalimbali ikiwemo madini ya nikeli, kinywe, heavy mineral sands, Rare Earth Elements, dhahabu na almasi,” amesema Dk. Biteko.

Katikika hatua nyingine, Dk. Biteko amesema Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa miundombinu mbalimbali inaboreshwa ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika pamoja na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

Awali, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema kuwa ili kuhakikisha nchi ya Tanzania inanufaika na rasilimali madini, wizara itaendelea kuimarisha usimamizi wa shughuli za sekta ya madini ili kuhakikisha inawanufaisha wananchi na serikali inapata mapato stahiki.

“Wizara itaendelea kuimarisha usimamizi wa shughuli za sekta ya madini ili kuhakikisha kuwa mchango wake unakua hadi kufikia asilimia 10 ya Pato la Taifa kufikia mwaka 2025 kama ilivyo katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025. Tutashirikiana na wadau mbalimbali wa sekta kuhakisha lengo hilo linafikiwa,” amesema Mavunde.

Zanzibar na Utalii wa Madini

Akizungumza katika Mkutano huo, Waziri wa Maji, Nishati na Madini-Zanzibar, Shaib Hassan Kaduara, amesema katika kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakua visiwani humo wanatarajia kuanzisha utalii wa madini ambao utaenda sambamba na kufungua soko la madini.

“Tunategemea kuanzisha utalii wa madini ambapo katika hilo tutakuwa na soko la madini Zanzibar hivyo kwa kila atakayekuwa na dhahabu yake anataka kuthaminisha anakaribishwa,” amesema Kaduara.

Mkutano wa Madini 2023 umehudhuriwa na mawaziri kutoka nje ya nchi, Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini, Makatibu Wakuu na Manaibu Wakuu kutoa Tanzania Bara na Visiwani, Waheshimiwa Mabalozi, Viongozi wa Serikali, Vyama vya siasa na Wakuu wa Taasisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles