22.7 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Bima ya afya iwe kipaumbele kwa kila mtu

Na YOHANA PAUL -MWANZA

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) hivi karibuni ulitangaza kupanua wigo wake wa mafao kwa kuanzisha vifurushi vipya kutoa fursa kwa kila mwananchi kadiri ya uwezo wake kujiunga na kunufaika na huduma za bima ya afya nchini.

Vifurushi hivyo vimegawanywa katika makundi matatu kwa maana ya kifurushi cha Najali Afya, Wekeza Afya pamoja na Timiza Afya ili kumpa nafasi mtu mmoja mmoja, familia au makundi mbalimbali ya wananchi kujiunga na huduma hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga, alisema vifurushi vimegawanywa katika makundi hayo kwa kuzingatia hali ya uchumi ya wananchi ili kuwawezesha kukabiliana na gharama za matibabu ambazo zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku na wakati mwingine kushindwa kuzimudu na kuangukia katika janga la umasikini au kifo.

Kulingana na mkurugenzi huyo, kuanzia umri wa miaka 18 hadi 35 mtu binafsi ni Sh 192,000 (Najali Afya), Sh 384,000 (Wekeza Afya), Sh 516,000 (Timiza Afya).

Kwa umri wa miaka 36 hadi 59 kwa kifurushi cha mtu binafsi ni Sh 240,000 (Najali Afya), Sh 444,000 (Wekeza Afya), Sh 612,000 (Timiza Afya).

Kwa umri wa miaka 60 na kuendelea kwa kifurushi cha mtu binafsi ni Sh 360,000 (Najali Afya), Sh 660,000 (Wekeza Afya), Sh 984,000 (Timiza Afya).

Hata hivyo bei za vifurushi hivyo uweza kuongezeka kulingana na idadi ya familia yaani mke, mume na mtoto mmoja hadi wanne.

Mkurugenzi huyo alisema mipango inafanyika ili kupitia vifurushi hivyo kila mwananchi apate fursa ya kuangalia ni kifurushi gani anaweza kujiunga nacho ili kuwa na uhakika wa kupata matibabu wakati wote.

Mbali na hayo pia vifurushi hivi vimetoa fursa kwa makundi maalumu kama bodaboda, waandishi wa habari, machinga, wanafunzi na watumishi wengine wa umma ili kuwapa nafasi ya kuweza kutimiza majukumu yao kwenye maeneo yao ya kazi pasipokuwa na hofu ya huduma za kiafya.

Makundi maalumu kuguswa na NHIF ni ukombozi mkubwa hasa kundi la waendesha bodaboda ambalo kutokana na kazi hiyo hugharimu maisha ya vijana wengi hali inayosababishwa na ajali wanazopata na kushindwa kukidhi gharama za matibabu.

Ujio wa vifurushi hivi unatoa nafasi kwa kila kundi kupata kadi ya bima na kuweka dhamana ya huduma bora za afya nyakati zote misukosuko ya afya inapotokea.

Ni wazi kwamba vifurushi hivi vya bima vimeondoa kasumba iliyokuwepo awali ambapo bima ya afya iliangaliwa kama kitu cha watumishi wa umma pekee lakini sasa NHIF wameifanya kuwa suala la kijamii na la muhimu kwa kila mtu.

Hivyo wazazi wajenge utamaduni wa kulipia bima ya afya ya watoto kama si familia ili kuwajengea watoto uhakika wa huduma za afya kwa kuwa afya bora ndiyo mhimili kwa mtoto kutimiza ndoto zake.

Katika kipindi hiki ambacho dunia inakumbana na ongezeko la magonjwa ya mlipuko na yale yasiyoambukizwa  kila mwananchi atambue thamani ya kuwa na bima ya afya bila kujali cheo au aina ya kazi anayofanya kwa kuwa itampa uwezo wa kupima na kutambua mustakabali wa afya yake bila kusubiri mpaka aelemewe na magonjwa.

Wakati sasa umefika Watanzania tubadili mitazamo na kuliona suala la kuwa na bima ya afya ni jambo la msingi kama ilivyo kwa simu ya mkononi au kadi ya benki kwani itatuwezesha kutimiza majukumu yetu ya kiuchumi tukiwa na uhakika wa matibabu pale tunapokumbwa na magonjwa.

0768864097

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,580FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles