24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Ujenzi majengo ya utawala utaongeza tija utoaji huduma

Na Ismail Ngayonga

UTAWALA bora ni nyenzo muhimu katika kuharakisha maendeleo endelevu ya nchi kwa kuzingatia misingi ya sheria, uwazi na uwajibikaji ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Ofisi ya Rais – TAMISEMI inasimamia utekelezaji wa shughuli za utawala bora kwa kuzingatia matakwa ya  Ibara  ya  146 (1)  ya  Katiba  ya  Jamhuri  ya  Muungano  wa  Tanzania  ya  mwaka  1977 inayohusu ugatuaji wa madaraka kwa wananchi ili kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na maendeleo.

Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Ofisi ya Rais – TAMISEMI iliendelea kuimarisha utawala bora ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majengo ya utawala katika mikoa, halmashauri, tarafa, kata, mitaa na vijiji ili kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.

Aidha ili kufikia malengo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wake, Serikali imeendelea kuwajengea uwezo viongozi na Watendaji kwenye mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuimarisha misingi ya uwazi, uwajibikaji na usawa katika matumizi ya fedha kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Tangu mwaka 1984, Serikali iliporejesha mfumo wa Serikali za Mitaa, jitihada kubwa zimekuwa zikifanyika katika kujenga mfumo imara wa kitaasisi ili kusimamia na kuratibu shughuli za utawala, utendaji na maendeleo katika ngazi ya mikoa, wilaya, halmashauri, tarafa, kata, kijiji, mtaa na kitongoji.

Agenda ya kuziimarisha Serikali za Mitaa iliyoidhinishwa mwaka 1996, ina lengo la kukidhi mahitaji ya kuwawezesha wananchi kushiriki kwa ukamilifu katika shughuli za maendeleo na kutanzua changamoto kadhaa zilizozikumba Serikali za Mitaa kwa muda mrefu.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo, alisema Ofisi ya  Rais – TAMISEMI  imeendelea kutimiza jukumu  la  msingi  la  kuzijengea uwezo Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Alisema katika katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, Tawala za Mikoa zimetumia Sh bilioni 31.64 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa ofisi na nyumba za viongozi katika mikoa, wilaya na tarafa.

“Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 20.6 zimetumika kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa ofisi za wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na tarafa na Sh bilioni 11.04 zimetumika kukarabati na ujenzi wa nyumba za viongozi kwenye mikoa, wilaya na tarafa,’’ alisema Waziri Jafo.

Waziri Jafo alisema ujenzi na ukarabati wa ofisi za wakuu wa mikoa umefanyika katika Mikoa ya Katavi, Simiyu, Njombe, Geita, Pwani, Arusha, Ruvuma, Dodoma na Singida kwa gharama ya Sh bilioni 7.2 na pia ujenzi na ukarabati wa ofisi za wakuu wa wilaya umefanyika katika wilaya 29 sambamba na kujenga ofisi 60 za za maofisa tarafa kwa gharama ya Sh bilioni 3.3.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo, katika mwaka 2018/19, Serikali ilijenga nyumba za viongozi 72 katika mikoa na wilaya kwa ajili ya wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa wilaya, makatibu tawala wasaidizi wa mikoa, makatibu tawala wa wilaya na maofisa tarafa na hadi kufikia Februari 2019 ujenzi na ukarabati wa nyumba hizo umegharimu Sh bilioni 11.04.

Akifafanua zaidi alisema halmashauri 78 zimeendelea na ujenzi wa majengo ya utawala zikiwemo halmashauri 55 zilizotengewa bajeti ya Sh bilioni 61.7 kuanzia mwaka wa fedha 2015/16 hadi 2017/18, ambapo ujenzi wa majengo hayo upo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.

“Halmashauri 23 zilizoanzishwa mwaka 2014 ziliidhinishiwa Sh bilioni 52.9 katika mwaka wa fedha 2018/2019 za ujenzi wa majengo ya utawala ya halmashauri. Hadi Februari, 2019 Halmashauri 23 zilipokea Sh bilioni 23 sawa na asilimia 43.4 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa majengo ya utawala,” alisema Jafo.

Aidha katika kuzijengea uwezo Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Serikali katika mwaka 2018/19 ilitoa mafunzo kwa wakuu wa wilaya 27 walioteuliwa Oktoba, 2018 katika nyanja za mifumo, taratibu za mawasiliano Serikalini na mahusiano baina ya taasisi za Serikali.

Mafunzo hayo yameimarisha utendaji kazi wa wakuu wa wilaya katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, utawala bora na utatuzi wa kero za wananchi na Desemba 2018, wakuu wa mikoa 26na makatibu tawala wa mikoa 26, wakurugenzi wapya wa halmashauri 39walioteuliwa walifanyiwa mafunzo juu ya utawala bora.

Vilevile, makatibu tawala wasaidizi wa mipango na uratibu 26wa mikoa na maofisa mipango 185wa halmashauri walipatiwa mafunzo kuhusu mipango na bajeti na mafunzo hayo yamesaidia kuboresha utendaji ndani ya Serikali na kutatua kero za wananchi ili kuboresha utoaji wa huduma.

Mamlaka za Serikali za Mitaa ni vyombo vya wananchi vinavyowawezesha wananchi kuwa na sauti katika maamuzi mbalimbali ama kwa kushiriki moja kwa moja au kupitia kwa wawakilishi wao katika shughuli za maendeleo na utawala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,476FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles