KAMPUNI ya Pan Africa Power Solutions (PAP) na ile ya Independent Power Tanzania (IPTL), imeitaka Bodi ya Rufaa ya Kodi nchini iamuru Kamishna Mkuu wa TRA, akamatwe na kupelekwa gerezani kwa kufuta hati za kuthibitisha ulipaji wa kodi wa kampuni hiyo katika manunuzi ya hisa za IPTL.
Hatua ya TRA kufuta hati hizo, ilitokana na udanganyifu uliofanywa na PAP kwa kuwasilisha nyaraka za kughushi za ununizi wa hisa, hali iliyoiwezesha kukwepa kodi ya Sh bilioni 8.68.
Maombi ya kampuni hiyo inayomilikiwa na Harbinder Singh Seith, yaliwasilishwa jana chini ya hati ya dharura yakiambatana na kiapo kilichoapwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa IPTL, Parthiban Chandrasakaran.
Maombi hayo yaliyowasilishwa dhidi ya Kamishna Mkuu wa TRA na BRELA, yanadai kamishna huyo alikaidi amri halali iliyotolewa na bodi Novemba 26 iliyokuwa ikimzuia kwa muda kuziondoa hati hizo, hivyo akamatwe na bodi iamuru apelekwe gerezani.
“Tunaomba bodi imwamuru Kamishna Mkuu wa TRA kutekeleza amri iliyotolewa, pia bodi itoe amri ya kuondoa barua ya kamishna ya Novemba 27 mwaka huu ambayo ilifuta hati za kodi mpaka maombi ya msingi yatakaposikilizwa,” inadai hati hiyo ya maombi.
Hati hizo za PAP zilizofutwa ni zile zenye namba 0049656 na 0049657 ambazo zilitolewa kwa ajili ya uuzaji wa hisa kutoka Kampuni ya Mechmar na Piper Links Investment na kati ya Piper Links na PAP.
Katika hati ya kiapo, Chandrasakaran alidai Desemba 23 mwaka jana wadai walipata hati hizo za kuthibitisha walilipa kodi kwa ajili ya uuzwaji wa hisa hizo.
Anadai kwamba Novemba 19, walalamikiwa walitoa taarifa ya siku sita kwa BRELA wakionyesha nia ya kuziondoa hati hizo kwa mazingira kwamba walalamikaji walipata mkataba feki wa mauzo ya hisa hizo.
“Kamishna si tu anabanwa na mamlaka, pia anatakiwa kufuata sheria za nchi zikiwamo za bodi, kwa kukiuka amri anapoteza sifa za kuendelea kushikilia nyadhifa hiyo aliyonayo,” alidai Chandrasakaran katika hati ya kiapo.
Hata hivyo kutokana na maombi hayo kuwasilishwa chini ya hati ya dharura, bodi hiyo mbele ya Katibu wake Respicius Mwijage imeamuru yasikilizwe leo.
PAP na IPTL waliwasilisha rufaa pamoja na maombi ya zuio la muda ambapo Novemba 26, Katibu wa bodi hiyo, Mwijage, alitoa zuio la muda kwa Kamishna Mkuu wa TRA na Msajili wa Makampuni nchini (Brela) kuziondoa hati hizo na kuacha hali ilivyo sasa iendelee kuwa hivyo.
Pamoja na kutolewa kwa amri hiyo, Novemba 28 TRA waliandika barua wakionyesha walishaziondoa hati hizo.
Zitto
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za serikali (PAC), Zitto Kabwe, alisema kitendo kinachofanywa na mmiliki wa kampuni hiyo ni kuonyesha jeuri ya fedha na kuidharau Serikali.
“Ana kiburi cha ufisadi na ni dalili za kuidharua Serikali, jambo kama hilo linaweza kufanywa Tanzania tu, Serikali idhibiti dhihaka hii kwa kuchukua hatua dhidi ya mtu huyu,” alisema Zitto.
Azimio la kwanza la Bunge juu ya kashfa hii, lilitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya Ulinzi na Usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi, dhidi ya Harbinder Singh Seth ambaye ni mmiliki wa Kampuni PAP na wengine wote waliotajwa na Taarifa Maalumu ya Kamati, kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusu miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea.
MWIGULU: KODI LAZIMA ILIPWE
Akizungumza bungeni wakati wa kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), juu ya ukaguzi wa akaunti ya Tegeta Escrow, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema lazima kodi ya Serikali iliyokwepwa ilipwe.
Alisema kutokana na kutolipwa kwa kodi ya ongezeko la thamani, TRA ilikuwa ikose Sh bilioni 26.97 lakini baada ya kubaini imeanza kufuatilia na Sh bilioni 4 tayari zimelipwa.
“Niwahakikishie Watanzania kuwa kodi hii italipwa, hatuwezi kuacha kodi kwa tajiri halafu tukakimbizana na mama mjane anayeuza mchicha barabarani,” alisema.
Alisema kwa upande wa kodi iliyokosekana kutokana na nyaraka batili zilizowashilishwa na PAP kwa TRA, barua ya kuzifuta imeshaandikwa na kuwa Serikali iko makini kwa suala hilo.
“Kuna watu wasio waaminifu, kuna mtu badala ya kuandika dola za Marekani milioni sita, akaandika Sh milioni sita, na badala ya kuandika dola za Marekani milioni 20, ameandika Sh milioni 20, naagiza mamlaka ifanye uwajibishaji wa ndani,” alisema.
RIPOTI TA CAG NA KODI ILIYOKWEPWA
Kwa mujibu wa ripoti ya PAC, Septemba 9, 2012 Kampuni ya Mechmar iliuza hisa saba kwa Piper Links ilizokuwa inamiliki katika Kampuni ya IPTL kwa bei ya dola za Marekani milioni 6.
Hata hivyo, taarifa zilizowasilishwa TRA kwa ajili ya kukokotoa kiasi cha kodi ya ongezeko la mtaji ambacho Mechmar ilitakiwa kulipa, zinaonyesha hisa hizo zimeuzwa kwa Sh milioni 6 za Kitanzania badala ya dola za Marekani.
Kutokana na udanganyifu huo, kodi ya ongezeko la mtaji iliyolipwa ni Sh 596,500 badala ya Sh 1,919,988,800 iliyopaswa kulipwa.
Kwa upande wa ushuru wa stempu, Mechmar ilipaswa kulipa Sh milioni 96 na siyo Sh 60,000 ilizolipa.
“Jumla ya kodi iliyopotea kwa maana ya kodi ya ongezeko la mtaji na ushuru wa stempu ni Sh 2,015,988,800,” inasema taarifa ya PAC.
Inasema hisa hizo kutoka Kampuni ya Piper Links kwenda PAP, ziliuzwa kwa gharama ya dola za Marekekani milioni 20, lakini taarifa zilizopelekwa TRA zilionyesha zimeuzwa kwa dola za Marekani 300,000.
“Kwa mantiki hiyo taarifa ya CAG inaonyesha kuwa Piper Links ilitozwa na kulipa kodi ya ongezeko la mtaji Sh 47,940,000 na Sh 4,800,000 kama ushuru wa stempu (stamp duty),” ilisema taarifa hiyo.
Katika mahojiano, Kamishna Mkuu wa TRA aliifahamisha PAC kuwa kwa gharama ya dola za Marekani milioni 20, kiasi cha kodi ya ongezeko la mtaji kilichotakiwa kulipwa ni Sh 6,399,977,600 na si Sh 47,988,800, na kwa upande wa ushuru wa stempu kiasi kilichotakiwa kulipwa ni Sh 320,000,000 na si Sh 4,800,000.
Kwa maana hiyo jumla ya kodi iliyopotea kwa maana ya kodi ya ongezeko la mtaji na ushuru wa stempu ni Sh 6,667,188,800.
Jumla ya kodi iliyopotea kutokana na uuzaji wa hisa za Mechmar kwenda Piper Links na za Piper Links kwenda PAP ni Sh 8,683,177,600,” inasema taarifa ya PAC.