24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Bosi TRA amkomalia bilionea wa IPTL

SeithNa Eliya Mboya, Arusha

KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade, amesema hatishwi na kauli ya mmliki wa Kampuni ya kufua umeme ya IPTL,  Herbinder Singh Seth ya kutaka akamatwe na kufikishwa mahakamani.

Kauli ya Kamishina Bade, imekuja siku chache baada ya Kampuni ya  Pan Africa Power Solutions (PAP) na  IPTL, kuitaka Bodi ya Rufaa ya Kodi nchini iamuru Kamishna Mkuu wa TRA, akamatwe na kupelekwa mahakamani kwa hatua yake ya kufuta hati za kuthibitisha ulipaji wa kodi wa kampuni hiyo katika ununuzi wa hisa za IPTL.

Akizungumza na MTANZANIA jijini Arusha jana, Bade alisema  siku zote mamlaka yake haimwonei mtu juu ya ulipaji wa kodi.

“Sitishwi na mtu, tunatakeleza majukumu yatu kwa mujibu wa sheria zilizopo. Kama ni Singasinga unayemsemea mimi simjui una maanisha nani? Kama ni yule wa IPTL najua ni mlipa kodi wangu, lazima alipe tu,” alisema Bade.

Alipoulizwa juu ya kauli ya Herbinder ya kutaka ashitakiwe mahakamani, Kamishna Bade alisema kauli hiyo hajaisikia.

“Hii kauli sijaisikia lakini kama ni kushitakiwa mimi nashitakiwa na kupelekwa  mahakamani kila siku. Hapa suala ni moja tu lazima kodi ilipwe.

“Mlipa kodi ambaye nimemwambia alipe kodi lazima alipe, hatuna mzaha katika kazi za taifa. Narudia na kusisitiza kauli yangu, hata huyu mfanyabiashara unayemsema lazima alipe kodi haina mjadala, kama nimesema alipe basi atalipa.

“Kama watu hawatalipa kodi basi sisi tutatumia mamlaka yote tuliyopewa kisheria kukusanya kodi husika,” alisema Bade.

Akizungumzia ushindi ilioupata  TRA katika shindano la ulinganishi wa taarifa za fedha, Kamishna Bade alisema ni mafanikio makubwa ambayo yanapaswa kuendelezwa.

“Siku zote taaluma ya uhasibu huleta maadili kwa taifa nawahimiza wahasibu na wakaguzi nchini kutanguliza maadili,”alisema Bade.

Hatua ya TRA kufuta hati hizo, ilitokana na udanganyifu uliofanywa na PAP kwa kuwasilisha nyaraka za kughushi za ununuzi wa hisa, hali iliyoiwezesha kukwepa kodi ya Sh bilioni 8.68.

“Tunaomba bodi imwamuru Kamishna Mkuu wa TRA kutekeleza amri iliyotolewa, pia bodi itoe amri ya kuondoa barua ya kamishna ya Novemba 27, mwaka huu ambayo ilifuta hati za kodi mpaka maombi ya msingi yatakaposikilizwa,” inadai hati hiyo ya maombi.

Awali Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima akifunga mkutano huo, alionyesha kusikitishwa na uchache wa wizara, taasisi za Serikali na halmashauri katika shindano la ulinganishi wa taarifa za fedha.

“Bodi ya Uhasibu (NBAA) wamefanya jambo jema kulinganisha taarifa za fedha. Hii inatupa utaratibu wa kuangalia wapi tumefanya vizuri na wapi tunatakiwa kuboresha.

“Kisheria NBAA si chombo kinachopelekewa hesabu kwa ajili ya kuzidhibitisha, isipokuwa nyinyi wenye fani mkitaka mjilinganishe mpo vizuri?

“Nadhani tutahimizana japo si jambo la lazima ni la hiari. Lakini ni jambo zuri kushindana kujua ubora wa hesabu zenu.

“Katika kundi la taasisi za Serikali nitawaomba NBAA watuandikie Wizara ya Fedha nasi tutamshauri waziri aandike barua kwa taasisi zote kusisitiza uzuri wa jambo hili.

MADAI YA IPTL

Katika madai yake,  IPTL ilisema hati hizo za PAP zilizofutwa ni zile zenye namba  0049656 na 0049657 ambazo zilitolewa kwa ajili ya uuzaji wa hisa kutoka Kampuni ya Mechmar na Piper Links Investment na kati ya Piper Links na PAP.

Katika hati ya kiapo, Chandrasakaran alidai Desemba 23 mwaka jana wadai walipata hati hizo za kuthibitisha walilipa kodi kwa ajili ya uuzwaji wa hisa hizo.

Alidai Novemba 19, walalamikiwa walitoa taarifa ya siku sita kwa BRELA wakionyesha nia ya kuziondoa hati hizo kwa mazingira kwamba walalamikaji walipata mkataba feki wa mauzo ya hisa hizo.

“Kamishna si tu anabanwa na mamlaka, pia anatakiwa kufuata sheria za nchi zikiwamo za bodi, kwa kukiuka amri anapoteza sifa za kuendelea kushikilia nyadhifa hiyo aliyonayo,” alidai Chandrasakaran katika hati ya kiapo.

Hata hivyo, kutokana na maombi hayo kuwasilishwa chini ya hati ya dharura, bodi hiyo mbele ya Katibu wake, Respicius Mwijage iliamuru yasikilizwe.

PAP na IPTL waliwasilisha rufaa pamoja na maombi ya zuio la muda ambapo Novemba 26, Katibu wa bodi hiyo, Mwijage, alitoa zuio la muda kwa Kamishna Mkuu wa TRA na Msajili wa Makampuni nchini (Brela) kuziondoa hati hizo na kuacha hali ilivyo sasa iendelee kuwa hivyo.

Pamoja na kutolewa kwa amri hiyo, Novemba 28 TRA waliandika barua wakionyesha walishaziondoa hati hizo.

Zitto

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za serikali (PAC), Zitto Kabwe, alisema kitendo kinachofanywa na mmiliki wa kampuni hiyo ni kuonyesha jeuri ya fedha na kuidharau Serikali.

“Ana kiburi cha kifisadi na ni dalili za kuidharua Serikali, jambo kama hilo linaweza kufanywa Tanzania tu, Serikali idhibiti dhihaka hii kwa kuchukua hatua dhidi ya mtu huyu,” alisema Zitto.

Azimio la kwanza la Bunge juu ya kashfa hii, lilitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), jeshi la polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi, dhidi ya Singh Seth ambaye ni mmiliki wa Kampuni PAP na wengine wote waliotajwa na taarifa maalumu ya Kamati, kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusu miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea.

MWIGULU: KODI LAZIMA ILIPWE

Akizungumza bungeni wakati wa kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), juu ya ukaguzi wa akaunti ya Tegeta Escrow, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema lazima kodi ya Serikali iliyokwepwa ilipwe.

Alisema kutokana na kutolipwa kwa kodi ya ongezeko la thamani, TRA ilikuwa ikose Sh bilioni 26.97 lakini baada ya kubaini imeanza kufuatilia na Sh bilioni 4 tayari zimelipwa.

“Niwahakikishie Watanzania kuwa kodi hii italipwa, hatuwezi kuacha kodi kwa tajiri,” alisema.

RIPOTI TA CAG NA KODI ILIYOKWEPWA

Kwa mujibu wa ripoti ya PAC, Septemba 9, 2012 Kampuni ya Mechmar iliuza hisa saba kwa Piper Links ilizokuwa inamiliki katika Kampuni ya IPTL kwa bei ya dola za Marekani milioni 6.

Hata hivyo, taarifa zilizowasilishwa TRA kwa ajili ya kukokotoa kiasi cha kodi ya ongezeko la mtaji ambacho Mechmar ilitakiwa kulipa, zinaonyesha hisa hizo zimeuzwa kwa Sh milioni 6 za Kitanzania badala ya dola za Marekani.

Kutokana na udanganyifu huo, kodi ya ongezeko la mtaji iliyolipwa ni Sh 596,500, badala ya Sh 1,919,988,800 iliyopaswa kulipwa.

Inasema hisa hizo kutoka Kampuni ya Piper Links kwenda PAP, ziliuzwa kwa gharama ya dola za Marekekani milioni 20, lakini taarifa zilizopelekwa TRA zilionyesha zimeuzwa kwa dola za Marekani 300,000.

“Kwa mantiki hiyo taarifa ya CAG inaonyesha  Piper Links ilitozwa na kulipa kodi ya ongezeko la mtaji Sh 47,940,000 na Sh 4,800,000 kama ushuru wa stempu (stamp duty),” ilisema taarifa hiyo.

Katika mahojiano, Kamishna Mkuu wa TRA aliifahamisha PAC kuwa kwa gharama ya dola za Marekani milioni 20, kiasi cha kodi ya ongezeko la mtaji kilichotakiwa kulipwa ni Sh 6,399,977,600 na si Sh 47,988,800, na kwa upande wa ushuru wa stempu kiasi kilichotakiwa kulipwa ni Sh 320,000,000 na si Sh 4,800,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles