27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Upasuaji watoto wenye vichwa vikubwa wasuasua

Mtoto mwenye kichwa kikubwa
Mtoto mwenye kichwa kikubwa

Hadia Khamis na Mwantum Saadi, Dar es Salaam

TAASISI ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), imekumbwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya upasuaji wa watoto wenye vichwa vikubwa na uti wa mgongo ulio wazi.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA ofisini kwake Dar es Salaam jana, Meneja Ustawi wa taasisi hiyo, Almas Jumaa, alisema  kukosekana kwa vifaa hivyo kumesabisha wazazi wengi ambao watoto wao wana matatizo hayo, kushindwa kupata huduma kwa wakati unaofaa.

“Vifaa vya kutolea maji kwenye vichwa vikubwa vinavyojulikana kitaalamu kama ‘Shunt’ ni vichache, na kila mtoto anapoletwa hospitalini hapa anatakiwa atumie kifaa chake jambo ambalo tumeshindwa kulimudu,” alisema.

Alisema kifaa kimoja cha Shunt kinauzwa kati ya Sh 100,000 hadi milioni 1 kulingana na ubora wake.

Jumaa alisema miongoni mwa changamoto kubwa wanayopambana nayo ni uhaba mkubwa wa watalaamu na nyenzo.

“Tuna tatizo kubwa la tatizo la uhaba wa wataalamu wa kufanya upasuaji, hadi sasa taasisi yetu ina wataalamu sita tu, wakati inapokea watoto 200 kila mwaka wenye matatizo haya,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Jumaa amewataka wasamaria wema na makampuni wajitokeze kusaidia taasisi hiyo ili ifikie malengo yake.

“Nawaomba wasamaria wema wajitokeze kutoa misaada ya hali na mali ili kufanikisha huduma kwa wagonjwa.

“Wazazi wengi ambao watoto wao wanakumbwa na tatizo hili ni masikini, hawana uwezo wa kufika Dar es Salaam kupata matibabu.

“Takwimu zinaonyesha watoto wanaozaliwa na tatizo hili kwa mwaka ni zaidi ya 4,600 na wanaofika hospitalini hapa ni 200 tu, hii inaonyesha wazi wengi wao wanabaki maeneo ya vijijini bila kupata tiba.

“Takwimu zinaonyesha karibu asilimia 60 ya watoto wenye matatizo haya wazazi wao hawana uwezo wa kumudu gharama,” alisema Jumaa.

Alisema kutokana na uzito wa tatizo hilo, timu ya madaktari ipo tayari kuweka kambi mkoa wowote endapo wafadhili watajitokeza.

“Wataalamu wetu wapo tayari kwenda mikoani kama tutawezeshwa, naamini watasaidia kutoa msaada wa vipimo na upasuaji,” alisema.

Alisema taasisi yake hadi sasa inatoa huduma za upasuaji bure kwa watoto wenye matatizo hayo.

Alisema watoto wanaozaliwa na vichwa vikubwa sio walemavu kama watu wengi wanavyodhani, bali ni ugonjwa ambao unaweza kutibika.

“Huu si ulemavu, ni ugonjwa kama yalivyo magonjwa mengine… tayari tumefanya upasuaji kwa baadhi ya watoto na wamepona kabisa,” alisema Jumaa.

Aidha amewaasa wajawazito kufuata ushauri wanaopewa na madaktari ili kuepuka  tatizo hilo. Aliwataka kula vyakula vyenye madini aina ya Folic Acid.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles