22.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Bilionea Bloomberg mwenye utajiri mara 17 ya Trump ajitosa rasmi kuwania urais Marekani

NEWYORK, MAREKANI

BILIONEA mfanyabiashara, Michael Bloomberg mwenye utajiri mara 17 ya alionao Rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump tayari ameingia kwenye kinyang’anyiro cha kuteuliwa kuwania urais kupitia chama cha Democratic baada ya wiki kadhaa za uvumi.

Mfanyabiashara huyo tajiri na Meya wa zamani wa Mji wa New York, amezindua rasmi kampeni yake ya kuwania kuteuliwa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha Democratic.

Mwanachama huyo wa zamani wa chama cha Republican mwenye umri wa miaka 77 alitangaza kuwania urais kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake akijisifu kuwa kwenye nafasi madhubuti ya kumshinda Rais Donald Trump.

Bloomberg amesema, Marekani haiwezi kuvumilia miaka minne zaidi ya utawala wa Rais Trump alioutaja kujaa vitendo vya kijinga na vilivyokosa maadili.

Kujiunga kwa Bloomberg kwenye kinyang’anyiro hicho kunatokea wiki kumi kabla ya kufanyika kura za mchujo, hatua inayoashiria wasiwasi uliopo ndani ya chama cha Democratic juu ya wagombea waliopo hivi sasa.

Kabla ya hatua ya sasa, kwa mujibu wa jarida linalofuatilia watu wenye ukwasi duniani, utajiri wa Bloomberg unafikia dola bilioni 52 (£40bn), hii ni mara 17 zaidi ya utajiri wa Trump mwenye ukwasi utajiri wa dola bilioni 3.1.

Awali Bilionea huyo alikaririwa akisema ana wasiwasi kama wagombea waliojitokeza kupitia chama hicho ni wazuri kuweza kumgalagaza  Trump ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2020 atakuwa anawania kipindi cha pili.

Bilionea huyo mwenye umri wa miaka 77  akiwa amempita miaka minne tu Trump alitangaza kuanza mchakato rasmi  kuwania nafasi hiyo wiki takribani mbili zilizopita.

Hadi sasa jumla ya wagombea 17 wamejitokeza kuwania nafasi ya kuteuliwa na chama cha Democrat kugombea urais dhidi ya Trump.

Wanaoongoza hadi sasa katika kinyang’anyiro hicho ndani ya Democrat ni Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden,  Seneta wa Massachusetts, Elizabeth Warren  na Seneta wa Vermont, Bernie Sanders.

Kura za maoni zilizotolewa hivi karibuni zimeonyesha kuwa Warren na Sanders ambao wamekuwa wakichukuliwa kama wapinzani wa Biden wanaweza kushindwa kumkabili Trump iwapo watapitishwa na chama chao.

Hadi sasa, wana-Republican watatu wamesema watajitokeza kupambana na Trump katika uchaguzi wa ndani wa chama chao wa kuwania kusimamishwa kugombea nafasi hiyo ya urais 2020.

Mkosoaji wa muda mrefu Trump naye amejiunga na mbio za kusaka nafasi hiyo kupitia Republican.

Lakini inaonekana kuwa ni ngumu kwa mtu yeyote ndani ya Republican kuchukua vazi kutoka kwa rais anayewania kipindi cha pili.

Wiki takribani mbili zilizopita, mshauri wa Bloomberg, Howard Wolfson alisema: ” Sasa tunahitaji kumaliza kazi na kuhakikisha kwamba Trump anashindwa.

“Lakini Mike (Bloomberg) ana wasiwasi zaidi kuwa wagombea waliojitokeza sasa hawana nafasi nzuri ya kufanya hivyo.

“Kulingana na rekodi yake ya kufanikisha, uongozi na uwezo wake wa kuleta watu pamoja ili kuendesha mabadiliko, Mike (Bloomberg) angeweza kuchukua pambano kwa Trump na kushinda,” alisema Wolfson.

BLOOMBERG NI NANI?

Bloomberg alikuwa ni mfanyakazi wa benki wa Wall Street kabla ya kupata ufalme wa kuzalisha fedha ambao umebeba jina lake.

Mhisani huyo  amechangia mamilioni ya dola kwenye elimu, huduma za afya na mambo mengine.

Kwa asili ni Democrat,  alikuja kuwa Republican  kwa ajili ya kufanikisha kampeni za kuusaka umeya wake wa New York  mwaka 2001.

Alitumikia vipindi vitatu vya kama meya hadi mwaka 2012, alijiunga tena na chama cha Democratic mwaka jana tu.

Ikizingatiwa kama Mwanademokrasia wa wastani, amekuwa akiangazia mabadiliko ya hali ya hewa kama suala muhimu, lakini alipoulizwa kuhusu mbio za urais mapema mwaka huu alikanusha .

Bloomberg  ni mfadhili mkubwa wa kundi la kudhibiti ‘Everytown for Gun Safety’, ambalo alisaidia kulianzisha mwaka 2014.

Kundi hilo na Bloomberg, limeonekana kuwa nyuma ya ushindi wa Democrat Virginia katika uchaguzi wa majimbo mapema wiki hii.

Kundi hilo  na lile linalojulikana kama National Rifle Association la Virginia –lilichangia dola milioni 2.5 katika uchaguzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,526FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles