23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

BIASHARA YA VIROBA YASHAMIRI UPYA MOROGORO


Na MWANDISHI WETU-MOROGORO   |

LICHA ya Serikali kupiga marufuku uzalishaji na uuzaji wa pombe za viroba nchini, biashara hiyo imeshamiri upya mkoani Morogoro, katika maduka na biashara ya vileo.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA Jumapili katika maeneo ya kata 29 Manispaa ya Morogoro kupitia waendesha pikipiki, maarufu kwa jina la bodaboda, umebaini kuwa, biashara hiyo imerudi kwa kasi kubwa katika maeneo mengi.

Malingo Msike, mwendesha bodaboda katika eneo la Mawenzi, Manispaa ya Morogoro, alidai kwa sasa viroba hivyo vinauzwa bila kificho na kwa bei ya juu.

Gazeti hili katika uchunguzi wake limebaini kiroba chenye ujazo wa milimita 100 kinauzwa kwa Sh 1,000 badala ya Sh 500.

Sharif Manola, mkazi wa Kata ya Mji Mpya, amevitupia lawama vyombo vya dola kwa kushindwa kudhibiti biashara hiyo, licha ya kuwafahamu wafanyabiashara wakubwa wanaoendelea na biashara hiyo katika maduka makubwa ya jumla.

“Nina imani kubwa vyombo vya dola vinatambua wafanyabiashara wakubwa walio na shehena za viroba katika stoo zao na ndiyo maana biashara hiyo imeshamiri upya Manispaa ya Morogoro,” alisema Manola.

Alisema, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipiga marufuku   uuzaji wa pombe hiyo Machi mwaka jana, baada ya Serikali kujiridhisha uwepo wa athari kubwa kwa watumiaji wa pombe hiyo, hasa vijana.

Katika hilo, Manola alishangaa kauli hiyo kupuuzwa na waliopewa mamlaka ya kusimamia uvunjwaji wa sheria na hivyo kuruhusu tena biashara hiyo kushamiri.

“Hakuna kificho tena uuzwaji wa pombe hiyo katika Manispaa na tumeshuhudia hata wafanyabiashara wa pombe hizo wakiuza bila vificho katika maduka ya rejareja na jumla, huku Jeshi la Polisi likijua,” alisema Manola.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wazazi wameiomba Serikali kuliangalia upya suala la uzalishaji na uingizaji wa pombe hizo za viroba, kwani vijana wao wameendelea kulewa na kushindwa kufanya shughuli za kuwaingizia kipato.

Wamesema kuwa, kushamiri kwa biashara ya viroba katika Manispaa kumeibua upya baadhi ya matukio ya ajali za barabarani, hasa kwa waendesha bodaboda ambao ni miongoni mwa watumiaji wakubwa.

Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro ,Ulrich Matei ,amekiri uwepo wa wafanyabiashara wasiotii amri na hivyo kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano dhidi ya wale wote wanaoendelea kusambaza pombe hiyo ya viroba .

Alisema jeshi la polisi linaendelea na operesheni kwenye maduka yanatajwa kujihusisha na biashara za viroba na kwamba wale ambao watapatikana na hatia watafikishwa mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles