29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

SH BILIONI TISA KUJENGA SOKO LA KISASA KINONDONI


Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM   |

JUMLA ya Sh bilioni tisa zimetolewa na Serikali kujenga soko la kisasa eneo la Magomeni, Dar es Salaam.

Soko hilo ambalo awali lilitakiwa kujengwa kwa mkopo kutoka Benki ya TIB, sasa litajengwa na fedha za Serikali baada ya kuonekana kuwa na riba kubwa.

Akizungumza baada ya kutembelea soko hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo, alisema tayari Sh bilioni 3.5 zimekabidhiwa kwa Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Alisema ujenzi wa soko hilo utaanza ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa na utakamilika Desemba, mwaka huu.

“Soko hili litajengwa kwa ghorofa sita ambapo sehemu ya kuegesha magari 150 itajengwa ardhini,” alisema.

Aliwataka viongozi wa Manispaa ya Kinondoni kusimamia fedha hizo kwa uadilifu ili zifanye kazi inayokusudiwa.

“Nikuombe mkurugenzi na watumishi wako ili ustaafu kwa usalama mzisimamie vizuri fedha hizi zifanye kazi iliyokusudiwa kwa sababu katika fedha ambazo hazihitaji masihara ni hizi,” alisema.

Pia aliwashangaa wafanyabiashara wa soko hilo kwa kufanya kazi katika mazingira magumu yaliyojaa matope.

“Kweli wafanyabiashara wa soko hili mna roho ngumu kufanya kazi katika mazingira haya, hali ya soko ni mbaya na tope kila mahali,” alisema.

Aliwaonya viongozi wa manispaa hiyo kutowaondoa wafanyabiashara waliopo sasa wakati wa kugawa vizimba kwa kuwa soko linajengwa kwa ajili yao.

“Ninaondoka na majina ya wafanyabiashara 669 waliomo humu, kwa sasa sitaki nisikie mmewaondoa na kuingiza wengine kabla ya hawa waliopo hawajapata vizimba.

“Nina uzoefu wa hili kutoka katika masoko mengine kama Machinga Complex na Soko la Samaki la Ferry watu kuondolewa baada ya mazingira kuwa bora, hivyo naomba siku mnagawa vizimba mniite niwepo kuthibitisha hakuna malalamiko,” alisema.

Pia aliagiza halmashauri zote nchini kuondoa riba katika asilimia 10 ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanawake na vijana kwa kuwa zinatoka kwao.

“Fedha hizi zinakusanywa kutoka kwao halafu mnawezaje kuzitoza riba? Wapeni ni fedha za wavuja jasho, ili mradi tu wanarudisha kwa wakati,” alisema.

Aliwataka wafanyabiashara hao kulipa kodi kwa Serikali pindi soko hilo litakapokamilika.

Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa Manispaa ya Kinondoni, Zahoro Hanuna, alisema wametenga Sh bilioni 1.2 kuboresha masoko yake huku lile la Tandale litajengwa kwa Sh milioni 100.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles