25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

Balozi Amina: Kutoka Zanzibar hadi Marekani kutunukiwa tuzo

Na Dennis Luambano, Dar es Salaam
KUNA baadhi ya majina ya wanawake Watanzania yamewahi kutamba katika anga za kimataifa kutokana na kazi zao.
Mathalan, Profesa Anna Tibaijuka wakati akiliongoza Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN Habitat), kabla ya hivi karibuni kukumbwa na kimbunga cha kashfa ya kupokea fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow kutoka kwa mbia wa Kampuni ya IPTL, James Rugemalira.
Mwingine ni Dk. Asha-Rose Migiro aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa UN inayoongozwa na Ban Ki Moon.
Wakati Dk. Migiro na Profesa Tibaijuka wakiwa wameacha kutekeleza majukumu ya kimataifa na kurudi nyumbani, yupo mwanamke mwingine Mtanzania ambaye kwa sasa anatikisa medani za kimataifa.
Mwanamke huyo si mwingine bali ni Amina Salum Ali, ambaye kwa sasa ni Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) nchini Marekani. Ukisoma wasifu wake uliosheheni majukumu mbalimbali aliyowahi kuyafanya katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa mbunge na nafasi mbalimbali serikalini, utagundua kwamba nafasi aliyonayo sasa hakuipata kwa bahati mbaya.
Wasifu wake ni mrefu lakini japo kwa ufupi ni kwamba licha ya kuiwakilisha AU nchini Marekani kupitia nafasi yake aliyoteuliwa Aprili, 2007 pia jukumu lake jingine ni kuendelea kujenga ushirikiano mwema kati ya Marekani na Bara la Afrika.

Majukumu mengine kati ya mengi ya Balozi Amina ambaye ni mzaliwa wa Zanzibar na msomi wa Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara na Masoko, ni kuboresha shughuli za kiuchumi kati ya Afrika na Marekani na kuendelea kuimarisha amani na mshikamano.
Kutokana na majukumu hayo machache hapo juu na mengine, ndiyo maana wiki iliyopita alitunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya Uongozi ya Taasisi ya GB Group Global ya Marekani ya mwaka 2015.
Hafla ya tuzo hiyo ambayo hutolewa kila mwaka ilifanyika katika Jiji la Washington, pia ilihudhuriwa na Rais wa zamani wa Malawi, Joyce Banda.
Taasisi ya GB Group Global ilisema kwa mwaka huu tuzo hiyo ilijikita zaidi kwa ajili ya wanawake wa Afrika.
“Tunaheshimu mchango wa wanawake ambao kwa sasa wana ushawishi mkubwa katika sera za Serikali kupitia ushiriki wa kisiasa, maendeleo ya kiuchumi kupitia ujasiriamali na mikakati ya maendeleo ya biashara kupitia uongozi wa mashirika,” ilisema taarifa ya Taasisi ya GB.
Nchi zilizowakilishwa katika tuzo hiyo ni Angola, Guinea ya Ikweta, Ivory Coast, Nigeria, Burkina Faso, Senegal na Tanzania.
Washindi wa nyuma wa tuzo hizo ni pamoja na Mwenyekiti wa AU, Dk. Nkosazana Zuma na Rais wa zamani wa Burkina Faso, Blaise Compaoré.
“Tunahisi hakujafanyika juhudi za kutosha kuunda majukwaa ambayo uongozi wa Afrika na mafanikio yake yanatambulika,” inasema.
Taasisi ya GB Group Global inasema inatambua mustakabali ujao wa Afrika unategemea hekima ya viongozi wa sasa pamoja na uwezeshaji zaidi wa wanawake na vijana. Inasema inatumia tuzo kama kichocheo cha kuonyesha, kuheshimu na kusherehekea wale ambao ni sehemu ya lulu ya baadaye ya Afrika.
Inasema kazi yake ni kuakisi dira ya Dk. Gloria B. Herndon’s ambaye ni Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wake pia ni kilele cha miaka zaidi ya 45 ya kukuza uhusiano mwafaka wenye kuvuka mipaka, wenye kujenga imani ya kibinadamu, kubakia kujitoa kwa ajili ya jamii na kuwezesha uwezeshaji wa wengine.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Balozi Amina anasema ndoto yake ni siku moja kuiona Tanzania na Afrika kwa ujumla, ikipiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali na kutoka ilipo hivi sasa.

“Nataka tuone tukipiga hatua kubwa kutoka hapa tulipo na kuendelea mbele katika maendeleo ya watu wetu wa Afrika.
“Naamini iko siku inakuja ya mabadiliko hayo, naamini hivyo na tukiamua hilo litawezekana ikiwa sisi wote tutashirikiana,” anasema Balozi Amina.
Naye, Rais Banda alipozungumza katika hafla hiyo aliwataka wanawake wapendane na wasichukiane.
“Mimi naomba kuendelea kusisitiza upendo kati yetu, baadhi ya wanawake wa Afika tumekuwa hatupendani.
“Nataka tupendane na tushikamane, maana kwa muda mrefu hatuna umoja na mimi walioniangusha ni wanawake wenzangu licha ya kupambana kuwasaidia na nilipokuwa rais kwa muda mchache tu, niliweza kujenga wodi za uzazi zitakazosaidia kujifungua katika mahali salama zaidi lakini wao ndiyo waliniangusha,” anasema Rais Banda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles