27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

Pinda azungumza na Watanzania Japan

pindaNA MWANDISHI WETU, TOKYO
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema mauaji ya albino yanayojirudiarudia nchini yanachafua heshima na jina la Tanzania kwa kuwa yanakwenda kinyume na haki za binadamu.
Akizungumza na Watanzania wanaoishi Japan kwenye ubalozi wa Tanzania jijini Tokyo juzi, Pinda alisema kukosekana kwa hofu ya Mungu na elimu kwa baadhi ya watu nchini ndiyo chanzo cha mauaji hayo.
Alisema binadamu yeyote anayemwamini Mungu na kushika maagizo yake hawezi kudanganyika wala kushawishika kuwa kiungo cha albino kinaweza kuwa chanzo cha mafanikio yake.
Waziri Mkuu Pinda alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu risala ya Watanzania hao na kusema Serikali haijalifumbia macho tatizo hilo kwa kuwa watu kadhaa wamekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Hata kufunguliwa kwa vituo maalum vya kuwatunza watoto albino ili kuwalinda ni moja ya hatua ambazo Serikali imechukua kukomesha mauaji hayo.
“Lakini ushirikiano kati ya Serikali na wananchi ndiyo utakaokomesha tatizo hilo kwa kuwa wanaotenda uovu huo ni Watanzania wenzetu tunaoishi na kula nao kila siku.
“Mauaji haya yanafanyika usiku na wakati mwingine ndugu wa karibu au mzazi anatajwa kushirikiana kwa siri na wauaji kwani mara kadhaa yanapofanyika, baba mwenye mtoto anakuwa hayupo nyumbani,” alisema Waziri Mkuu.
Katika risala ya Watanzania hao iliyosomwa na Mwenyekiti wao, David Semiono, waliitaka Serikali ihakikishe mauaji hayo yanakomeshwa kwa vile yamekuwa chanzo cha kejeli, fedheha na aibu kwao.
“Wakati mwingine tunalazimika kujibu maswali mengi na magumu tunayoulizwa na wenyeji wetu Wajapan na wageni wengine kutoka nchi mbalimbali ambao wanaeleza kukerwa na mauaji hayo.
“Wengine wanasita hata kutembelea Tanzania kwa hofu kuwa huenda wauaji hao wakawafananisha na albino. Kwa hiyo tunaomba mauaji hayo yakomeshwe,” alisema Semiono.
Ziara ya Pinda inaendelea jijini Tokyo ambako alikutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wafanyabishara, washirika wa maendeleo na watendaji wa kampuni mbalimbali, ambao aliwaeleza fursa za uwekezaji zilizopo nchini na kuwafafanulia hali ya uchumi wa Tanzania na shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles