25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Bajeti ya tano Serikali ya JPM leo

Nora Damian -Dar es salaam

BAJETI Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2020/21 inatarajiwa kusomwa leo bungeni jijini Dodoma, huku ikitazamiwa kutoa mwanga wa kuongeza au kupunguza makali ya maisha.

Bajeti hiyo ya tano ya Serikali ya Awamu ya tano, itajadiliwa kwa siku tatu kisha wabunge watahitimisha kwa kuipitisha kwa kupigia kura za ndio za wazi.

Ratiba ya Bunge inaonyesha kabla ya kusomwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango ataanza kusoma taarifa ya hali ya uchumi.

Mwaka 2019/20 Bajeti Kuu ya Serikali ilikuwa Sh trilioni 33.1 na kwa mwaka huu kiwango hicho kitaongezeka kutokana na maoteo yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango.

Makadirio ya awali ya bajeti ya 2020/21 yaliyowasilishwa bungeni na Dk. Mpango yalikuwa Sh trilioni 34.88. 

Bajeti hiyo ambayo ni ya mwisho katika kipindi cha kwanza cha uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, inatazamiwa kuleta matumaini mapya kwa wananchi kuhusu namna ya kujikwamua kiuchumi, hasa kutokana na janga la Covid–19 lililoikumba nchi kwa miezi kadhaa sasa.

Ugonjwa wa corona umeathiri sekta mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zina mchango mkubwa katika kuchangia pato la taifa na ukuaji wa uchumi.

Mathalani katika sekta ya utalii, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla alikaririwa akisema janga hilo limeathiri kwa kiwango kikubwa sekta hiyo na hivyo kuathiri uchumi wa nchi pia.

Hata hivyo, alisema wameweka mwongozo ambao unaelekeza hatua muhimu za kufanya ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona na kuwataka watalii na wananchi wanaohudumia watalii kuufuata ili kujilinda. 

Itakumbukwa pia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ililazimika kutoa nafuu ya viwango vya riba kama jitihada mojawapo katika kukabili athari za corona.

BoT ilitangaza kushusha viwango vya riba inayotozwa kwa benki kukopa BoT kutoka asilimia 7 hadi 5 na kushusha kiwango cha chini cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu kutoka asilimia 7 hadi 6.

Wadau mbalimbali wa masuala ya uchumi wanatarajia kuwa Bajeti Kuu ya Serikali itatoa mwanga, hasa kutokana na madhara yaliyotokana na corona na namna bora ya kusaidia sekta zilizoyumba ili ziweze kuinuka na kuendelea kuchangia uchumi wa nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Equality for Growth (EfG), Jane Magigita, alishauri nguvu kubwa katika bajeti hiyo ielekezwe zaidi katika sekta isiyo rasmi ambayo imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na corona.

“Sekta isiyo rasmi huko ndiko kwenye watu wengi, kuna wajasiriamali, wafanyabiashara, mama lishe, wakulima na wengine wengi, kwa hiyo mnyororo ni mkubwa na wengi wameumizwa na janga hili.

“Nashauri bajeti ijikite kuangalia zile sekta ambazo zimeyumba ili ziweze kuinuka na kuendelea kuchangia uchumi wetu,” alisema Jane.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles