33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi ya dawa za kulevya inayowakabili Hariri, mkewe yaanza kunguruma Mahakama ya Uhujumu Uchumi

Kulwa Mzee -Dar es salaam

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi imeanza kusikiliza kesi ya kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya inayomkabili Mohammed Hariri na mkewe Muna Said.

Kesi hiyo inasikilizwa mbele ya Jaji Emaculata Banzi, na mashahidi wawili wametoa ushahidi akiwemo SSP Neema Mwakagenda kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).

SSP Neema katika ushahidi wake alidai mshtakiwa Hariri alishuhudia ufungaji wa kielelezo cha kesi hiyo na kuandika maandishi juu ya bahasha ya kielelezo hicho.

Alidai kielelezo hicho ni pakiti ya nailoni angavu ambayo ndani ilikuwa na dawa zinazodhaniwa kuwa za kulevya na kuwekwa ndani ya bahasha ya kaki ya A4.

SSP Neema alidai Machi 3 mwaka 2018 akiwa ofisi za DCEA, alipokea pakiti yenye unga udhaniwao dawa za kulevya kutoka kwa Inspekta Hassan Msangi kuihifadhi.

Pakiti hiyo anadai ilikuwa ya kifungashio cha nailoni angavu ikiwa imewekwa ndani ya nailoni ngumu ya mistari meusi na meupe na kusajili katika daftari la usajili wa vielelezo na kukipa namba DCEA/AR/11/2018.

SSP Neema alidai kuwa aliandaa bahasha kwa ajili ya kufunga kwa lakili, na katika ufungaji alikuwepo mtuhumiwa Hariri, shahidi huru Yahaya Abubakari, Stesheni Sajenti Juma Suleiman na maofisa wengine.

“Kielelezo hicho kiliwekwa katika bahasha mbili, A4 na A3, niliandika majina yangu, majina ya mtuhumiwa, shahidi na kusaini, nilimuomba mtuhumiwa Hariri aandike majina yake na kusaini, aliandika maandishi  ‘Mimi Hariri Mohamed sitambui nini kilichowekwa kikanifanya nisaini,” alidai shahidi huyo.

Alidai katika bahasha ya pili A3 ambayo pia iliwekwa kielelezo hicho, mshtakiwa huyo alisaini kwa hasira na kufanya bahasha hiyo kuchanika kidogo sehemu ya sahihi yake.

SSP Neema alidai kuwa Machi 5 mwaka 2018 bahasha hiyo ya kielelezo ilikabidhiwa kwa Stesheni Sajenti Juma Suleimaji kwa kupeleka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi wa kitaalamu na kukirudisha jioni siku hiyo hiyo.

“Machi 27, mwaka 2018 nilipokea ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali kutoka kwa Konstebo Razalo Muhegele na Juni 8 mwaka huu nilitoa kielelezo hicho baada ya kupokea hati ya wito kama shahidi katika kesi hii na baada ya kufika mahakamani kielelezo hicho nilikikabidhi kwa mwendesha mashtaka wa Serikali,” alidai shahidi huyo.

Katika kesi hiyo inayoendelea kusikilizwa mfululizo, washtakiwa hao wanadaiwa Machi 2 mwaka 2018, eneo la Mtitu, Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam, walisafirisha gramu 214 za Heroin.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles