24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

Matumizi ya bangi yatangazwa kuongezeka nchini 2019

Ramadhan Hassan -Dodoma

SERIKALI imesema katika kipindi cha mwaka 2019, bangi ilitumika zaidi nchini huku kukijitokeza ongezeko la matumizi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya ikiwemo Tramadol.

Ongezeko hilo lilichangiwa na udhibiti wa dawa za kulevya zilizozoeleka kama vile heroin na cocaine unaofanywa na Serikali.

Katika kipindi hicho, kilogramu 55.35 za heroin, kilogramu 10.34 za cocaine, bangi tani 21.16 na tani za mirungi 9.07 zilikamatwa.

Hayo yalielezwa jana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Mavunde alisema kuna ongezeko la matumizi ya dawa ya ketamine, valium na nyingine kama mbadala wa heroin na cocaine.

“Waraibu wa dawa za kulevya wanapokosa dawa walizozizoea, hukimbilia kutumia dawa tiba zenye asili ya kulevya ili kupunguza makali ya ‘arosto’ wanayoipata,” alisema Mavunde.

Alisema kuwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya dawa hizo hapa nchini kwa mwaka 2019.

“Kwa kushirikiana na wadau wa nje na ndani ya nchi, imefanya operesheni mbalimbali ndani ya nchi ikiwemo mipakani na katika ukanda wa pwani na Bahari ya Hindi na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza uingizwaji wa dawa za kulevya nchini,” alisema Mavunde.

Aidha, alisema watuhumiwa waliokamatwa na dawa hizo kwa kipindi hicho ni 10,384 ambao kesi zao zipo katika hatua mbalimbali mahakamani.

Alisema dawa hizo zinazokamatwa huteketezwa kwa mujibu wa sheria kwa kushirikisha mamlaka mbalimbali za Serikali baada ya hukumu kutolewa.

“Mwaka 2019 tuliteketeza kilogramu 122.55 za heroin na kilogramu 71.507 za cocaine katika viwanda vya saruji Dar es Salaam na Mbeya,” alisema Mavunde.

Kuhusu tiba, Mavunde alisema huduma ya tiba hadi kufikia Desemba 2019 Serikali imeanzisha vituo sita vya kutolea matibabu kwa waraibu wa dawa hizo kwa kutumia Methadone.

“Vituo hivyo vilivyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Dodoma vilikuwa vimesajili waraibu 7,600,” alisema Mavunde.

Aidha, alisema inakadiriwa kuwa katika kila watu nane wanaojidunga, mmoja anaishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na maambukizi ya VVU na Ukimwi (Unaids), limekadiria kuwa mtu anayejidunga anaweza mara 22 zaidi kuambukizwa VVU.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kinga na Tiba wa DCEA, Dk. Peter Mfisi, alisema sheria iliyopo inaruhusu kilimo cha bangi nchini kwa matumizi ya kisayansi.

Alisema ipo sheria ambayo inampa mamlaka Kamishna kuruhusu kilimo cha bangi au koki kwa matumzi ya kisayansi kama tafiti au matumizi ya kutengenezea dawa.

“Kuna njia maalumu ambayo mtu anayetaka kulima bangi kwa ajili ya utafiti au kwa ajili ya kutengenezea dawa anapaswa kuitumia, ni pamoja na kupata kibali kutoka Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, waweze kuridhika kwamba mtu huyo akilima bangi ataitumia kwa ajili ya kutengenezea dawa na si vinginevyo,” alisema Dk. Mfisi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,249FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles