23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Bado hakuna mifumo ya utatuzi wa migogoro kazini -Ripoti

Na Judith Siaga (TUDARco), Mtanzania Digital

RIPOTI mpya ya Haki za Binadamu na Biashara ya mwaka 2020 imebainisha kuwa bado hakuna mifumo ya utatuzi wa migogoro ya kampuni hasa kwenye maeneo ya kazi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki Binadamu(LHRC), imebeinisha kuwa ni asilimia 53 pekee ya makampuni yalidai kuwa na mifumo ya utatuzi wa migogoro ya kazi.

Ripoti hiyo imefafanua kuwa, baadhi ya wafanyakazi waliohojiwa walilalamika kuhusu kutokuwepo mifumo ya utatuzi wa migogoro katika ngazi ya kampuni.

“Ni 53% pekee ya makampuni yalidai kuwa na mifumo ya utatuzi wa migogoro ya kazi, sababu kuu za migogoro katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni pamoja na kukataliwa/kunyimwa likizo, kutolipwa baada ya kufanya kazi muda wa ziada.

“Pia kutowasilisha michango ya hifadhi ya jamii, kucheleweshewa malipo ya mishahara, kuchelewesha malipo ya fedha za kujikimu wakati wa safari (hasa kwa madereva wa mabasi na malori), kukiuka mkataba, makato ya mishahara, kufanya kazi zaidi ya muda wa juu wa kufanya kazi, na likizo bila malipo,” imeeleza ripoti hiyo.

Aidha, imeendelea kufafanua kuwa, migogoro ya kazi iliyosajiliwa na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) iliongezeka kutoka 14,777 mwaka 2018/2019 hadi 16,269 mwaka 2019/2020, huku makampuni 5 kati ya 10 yana mifumo ya utatuzi.

“Utafiti uligundua kwamba Janga la Korona lilichangia kuongezeka kwa migogoro, kwa kuwa waajiri walichukua hatua mbalimbali kukabiliana na hasara iliyosababishwa na janga hilo, ikiwemo kushuka kwa uzalishaji, faida, na uhitaji ya bidhaa na huduma.

“Migogoro mingi ya kazi iliyosajiliwa na CMA kwa kipindi cha 2018/2019 na 2019/2020 iliwahusisha wafanyakazi katika sekta za usafirishaji, ulinzi binafsi na ukarimu.  Migogoro mingi ya kazi iliyosajiliwa na CMA katika miaka ya 2018/2019 (38.5%) na 2019/2020 (39.5%) ilihusu mwisho au usitishaji wa ajira,” imeeleza ripoti hiyo ya LHRC.

Wakati ripoti hiyo ikibainisha hayo, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 na Sheria ya Taasisi za Kazi, pia ya mwaka 2004, zilianzisha na kutambua mifumo ya utatuzi wa migogoro ya kazi, hususan Tume ya Usuluhishi na Uamuzi na Kitengo cha Kazi cha Mahakama Kuu.

Aidha, ukiacha mifumo hiyo ya utatuzi wa migogoro ya kazi, ambayo ni ya Serikali, kuna mifumo isiyo ya kiserikali ya utatuzi wa migogoro hiyo, ikiwemo katika ngazi ya kampuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles