Baba adaiwa kumuua mwanawe wa miaka saba kwa kupoteza ng’ombe

0
419
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga

Walter Mguluchuma-Katavi

MTOTO wa miaka saba, Lusambaja Bundala, mkazi wa Kitongoji cha Luhafwe, Kata ya Ntongwe, Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, amedaiwa kuuawa na baba yake kwa kupigwa kichwani na kitu chenye ncha kali kwa madai ya kupoteza ng’ombe aliokuwa akiwachunga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga,  alisema tukio hilo la mauaji lilitokea juzi saa nne asubuhi katika Kitongoji cha Luhafwe.

Alisema wakati wa uhai wake, marehemu alikuwa akiishi nyumbani kwa baba yake mdogo, Juma Lusambaje (28) ambaye ndiye mtuhumiwa wa mauaji hayo.

Kamanda Kuzaga alidai kuwa kabla ya kuuawa mtoto huyo, akiwa na mtoto mwenzake aitwaye Ibrahimu  Lusambaja (13), Septemba 12 walitumwa na mtuhumiwa kwenda kuchunga ng’ombe.

Alisema toka siku hiyo alipokwenda kuchunga, Bundala hakuonekana hadi juzi saa nne asubuhi alipokutwa amefariki dunia kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani na kuchomwa kisu chini ya kidevu.

Kamanda Kuzaga alidai kuwa chanzo cha mauaji ya  mtoto huyo ni hasira za mtuhumiwa baada ya  kupotelewa na ng’ombe alizokuwa akizichunga.

Alidai baada ya mtoto huyo kupoteza ng’ombe,  mtuhumiwa alichukua sheria mkononi na kuamua kumpiga kwa kutumia chuma chenye ncha kali na  kumchoma na kisu hadi kuuawa kisha hakutoa taarifa kwa mtu yeyoye.

Kamanda Kuzaga alisema mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili

 Mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu zake kwa mazishi baada ya kuufanyia uchunguzi wa kidaktari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here