25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

AZIMIO LA ARUSHA TASWIRA YA UJAMAA, KUJITEGEMEA

Na BALINAGWE MWAMBUNGU


WIKI iliyopita, kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu tathmini ya miaka 50 ya Azimio la Arusha. Chini ya Kavazi la Mwalimu Julius Nyerere, lakini lilikosa msisimko kwa sababu viongozi waliokaa kule Zanzibar mwaka 1992 na kuamua kulitosa Azimio la Arusha kabla ya kuvuka Kisiwa cha Chumbi, hawakuhudhuria. Kongamano hilo lilikuwa mahali mwafaka kuwauliza, ni sababu gani zilizowafanya kulifuta.

Aidha, tulitegemea kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kinajitapa kwamba ni mrithi wa TANU (Tanganyika African National Union), kingepeleka ujumbe mzito ili kuonesha kwa vitendo, kwamba CCM bado kinaamini katika misingi ya TANU.

Hata gazeti la chama, Uhuru la Ijumaa, Februari 24, 2017, ambalo lilikuwa chombo kikuu cha uhamasishaji wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, halikuona umuhimu wa kuchapisha taarifa za yaliyojiri kwenye kongamano hilo.

Mwalimu Julius Nyerere alistaafu mwaka 1985, CCM wakampa kutembea nchi nzima kutekeleza programu ya kukiimarisha chama. Lakini mwaka 1992, miaka saba baadaye, kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho kilichokaa Zanzibar, ikatangazwa kwamba kikao hicho kilikubaliana kuifuta miiko ya uongozi iliyokuwa inawazuia viongozi wa kisiasa na watendaji wakuu serikalini na mashirika ya umma kujihusisha na mambo ya kujipatia kipato cha ujanja ujanja na biashara. Hadi leo hii, haijawahi kutolewa tamko rasmi, kwamba Siasa ya Ujamaa na Kujitengea imefutwa. Ujamaa ndio ulikuwa msingi wa mustakabali wa nchi.

Kwa kuutazama uongozi wa kitaifa wa CCM, unaweza kusema kwamba sehemu kubwa ya viongozi, ukimwondoa Philip Mangula (Makamu Mwenyekiti), hawalijui Azimio la Arusha. Kama wanalijua, hawakuwa waumini wake. Maana kama alivyofundisha Mwalimu Julius Nyerere, Ujamaa ni imani kama ilivyo imani za dini. Wanachama walitakiwa waijue kikamilifu imani na kuishika, kama wanavyoshika imani zao za kidini. Wakrito kwa mfano, kila wanapofanya ibada, ni lazima wakiri imani ya Kikristo. Hakuna uhakika kuwa wapo wanaCCM hivi sasa, ambao wako kama askari wa mstari mbele kukiri imani ya Ujamaa na ambao wako tayari kulitetea Azimio la Arusha na siasa yake ya Ujamaa na Kujitegemea.

WanaCCM hawasikiki hata katika mikutano yao—wakilitaja Azimio au Ujamaa. Maneno ‘Azimio na Ujamaa’ hayamo tena katika msamiati wao wa kisiasa. Kama alivyowahi kusema Horace Kolimba (marehemu),  CCM kimepoteza dira. Wanasema ‘itikadi ya chama’—lakini wanapatwa na kigugumizi kutaja ni ipi.

Huko nyuma, ili kujenga kada ya waumini wa Ujamaa, CCM kilirithi toka TANU, vyuo vya kanda vya uongozi na Kivukoni kilikuwa kama Chuo Kikuu cha Itikadi. Viongozi wengi wa mashirika ya umma, wakuu wa idara za Serikali na makatibu wakuu, ilikuwa lazima wapitie Kivukoni—wapikwe na kupewa mbinu za namna watakavyosimamia utekelezaji wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Lakini baada ya Azimio la Zanzibar, hakuna kada mmoja wa CCM au Serikali wakati ule, aliyejitokeza na kupinga uamuzi wa Zanzibar. Hii inaonesha kwamba wengi wao, ama waliogopa kutupwa nje ya mfumo mpya wa utawala, au hawakuwa waumini wa siasa ya Ujamaa.

Mwalimu aliliweka vizuri kwamba ili tuendelee, tunahitaji vitu vinne—watu, ardhi (chanzo kikuu cha utajiri), siasa safi (mpangilio mzuri wa maisha ya wananchi), na uongozi bora, uliojengwa juu ya msingi ya Itikadi ya Ujamaa. Ni wazi kwamba nchi haiwezi kuwa nchi kama haina watu. Haiwezi kuitwa nchi kama hakuna ardhi. Vitu hivi viwili ndio msingi mkuu wa nchi kuitwa nchi. Baada ya hapo, watu wanatafuta mustakabali wao—wakae vipi na wajiongoze vipi. Hapa ndipo linakuja suala la uongozi na namna wananchi wanavyotaka kuongozwa. Chini ya Azimio la Arusha, Watanzania walijenga taswira na liliwapa na tumaini kwa kuwa  lililenga kuwakomboa wanyonge.

Katika ujenzi wa Ujamaa—walitakiwa viongozi (si bora viongozi), ambao wanakiri kwamba Ujamaa ni utu, kama walivyo viongozi wa kidini, wanakiri kwamba uongozi ni kuonesha njia. Kiongozi hawezi kuonesha njia kama hakuandaliwa. CCM miaka ya hivi karibuni, walitangaza kwamba wana nia ya kuvifufua vyuo vyao vya itikadi, lakini hawakusema watafundisha itikadi ipi—maana Serikali ya chama chao inatekeleza sera ya soko huria na kuwavutia uwekezaji hasa wa kutoka nje kwa kuwa wawekezaji wa ndani hawana mitaji mikubwa.

Azimio liliwe na masharti ya viongozi. Kiongozi alikuwa yule aliyeikubali siasa ya Ujumaa na alitakiwa aishi maisha yake kwa kufuata misingi ya Ujamaa. Kiongozi alitakiwa kuwa mkulima au mfanyakazi, hakutakiwa kushiriki katika jambo lolote la kibepari, au kuwa na hisa katika kampuni yoyote au kuwa na hisa katika kampuni ya kibepari, hakutakiwa kuwa na mishahara miwili au nyumba za kupangisha.

Viongozi wa sasa wanautafuta uongozi kupitia siasa, ili wajitajirishe. Wana kampuni zao au wamenunua hisa katika kampuni za ndani na nje. Wanashiriki katika biashara za kimataifa na kuweka fedha zao kwenye baenki zinazokwepa kodi (Off Shore banks). Kwa walio wengi, siasa imekuwa mtaji au ngazi ya kuutafuta utajiri.

Wapo wasomi wanaosema ‘Ujamaa ni ‘itikadi mfu’, lakini hawasemi ni namna gani tutapata mustakabali wa nchi yetu. Azimio la Arusha ndilo lilikuwa suluhisho kwa kuwa liliwapa Watanzania taswira na tumaini. Sasa hivi wananchi wanyonge wamekata tama, matajiri ambao ni wachache wanazidi kutajirika na maskini wanazidi kuzama katika umaskini. Nini suluhisho?

Wanataja ndoto ya ‘Tanzania ya Viwanda’ lakini hawachanganui, hawasemi tutafikaje huko na kwa mustakabali upi. Tunawezaje kujenga taifa moja wakati hatuna nia moja, hasa ikitiliwa maanani kwamba chama kilicho madarakani hakitaki mwelekeo mpya, kujenga misingi ya dhati ya haki na demokrasia kwa kuunda Katiba na sheria zitakazosimama na kufuatwa na chama chochote kitakachochaguliwa kushika dola.

Rais aliyetangulia, Jakaya Kikwete, aliliona hili, akaitisha Bunge la Katiba, lililowashirikisha  wasomi, makundi ya kijamii, wafanyakazi, sekta binafsi na wakulima. Lakini bahati mbaya Bunge la Katiba likavurugwa, likatekwa nyara na Kikwete badala ya kusimamia yale aliyokuwa amekusudia, akaamua kwenda na upepo wa matakwa ya chama chake.

Matokeo yake nchi sasa iko katika mkwamo wa kisiasa na kiuchumi. Walio madarakani wanasema suala la Katiba Mpya kwao si kipaumbele. Sasa nchi itakwendaje bila mfumo unaoeleweka. Kabla ya kuua Azimio la Arusha, ulikuwapo mfumo. Tulijua Taifa letu lilikuwa linaelekea wapi. Sasa tunapapasa gizani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles