27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

MCHAWI MPE MTOTO AKULELEE

SIKU chache nilipita barabara ya Kinondoni ambayo inakatiza Ali Hassan mwinyi. Nilishtushwa sana kuona watu wengi wamekaa chini pembeni ya barabara wanaomba. Baadhi yao walikuwa watoto wengi sana. Wamejazana kama makole ya nazi.

Hivi hii tabaka ya kuomba omba imetoka wapi? Kila sehemu nyingi unazopita Dar unakuta kuna baadhi ya wananchi wanaomba. Wengine kwenye barabara unaona hali yao ile ya kusikitisha sana. Unajiuliza ni wapi tumekosea mpaka unakuta hali kama hii. Ni kweli ombaomba wapo sehemu nyingi duniani sio Tanzania tu.

Hata hivyo nachanganyikiwa kwani mila na desturi zetu ni kwamba tunasaidiana sana kijamii. Jamii yako haiwezi kukutelekeza na kukuacha unaomba mitaani. Sababu ya watu, saa zingine unakuta familia nzima wanaomba, kuwa katika hali hii inawezekana jamii wanapotoka wameshindwa kujipanga na kuweza kuwasaidia hawa wanaopoteza mwelekeo na kuwapa huduma ya aina yoyote. Katika mfumo huu utakuta jukumu la kwanza ni wanafamilia kuwasaidia ndugu wa karibu. Baada ya hapo wakishindwa basi jukumu linawaangukia jamii wa karibu na matatizo yanaweza kumaluizika kama kila mtu akitimiza wajibu wake.

Lakini unakuta maisha ya kisasa ni kwamba kila mtu abebe msalaba wake. Ndugu marafiki na Majirani watasaidiana sana kwenye arusi, kipaimara, ugonjwa, vifo na mazishi lakini kwa wale ambao wana hali ambayo ni ya kudumu kama kilema au kipofu jamii haina muda nao. Hawa wanaachwa na ni juu yao wenyewe waweze kujilisha na kutafuta riziki jinsi wanavyofahamu wao wenyewe.

Ni kwa sababu gani jamii za karibu za hawa vilema na vipofu wameshindwa kujipanga kuweza kuwasaidia watu wao wa karibu? Picha ambayo inanijia mie ni kwamba ule mfumo uliokuwapo hapo awali umemomonyoka na kutawanyika katika matabaka ya kibinafsi. Nguvu ambayo ingeweza kusaidia kwenye jamii hizo, imehama na kupandikizwa kwenye jamii ambayo miundombinu imekamilika. Na haya yote ni kwa jina la maendeleo.

Kama huduma hazitoshelezi na kukidhi mahitaji ya wananchi basi watahama na kwenda sehemu ambayo huduma hizo zipo. Huku nyuma wanaacha wale wasiojiweza. Hii inadhoofisha ushirikiano ndani ya jamii na maisha yanazidi kuwa magumu kwani ule ukaribu wa ubinadamu uliokuwa karibu ndani ya jamii polepole unabadilika na badala yake kuingia kwenye uhusiano wa kifedha. Kama huna chanzo au njia ya kukuwezesha upate huduma katika jamii yako na wewe ni mlemavu wa macho au kimwili basi utalazimika utoke katika mazingira hayo na kutafuta hela ambazo zitakuwezesha ununue hizo huduma ambazo unahitaji kurahisisha maisha yako. Utakimbilia mjini kuomba.

Sababu wewe upo katika hali na mazingira hayo ni kwamba miundombinu ambayo ni ya kiasili haipo tena. Ule moyo na utu umebadilishwa na badala yake kuwekwa thamani ya shilingi na senti.  Kwa mtu mmoja kubeba mzigo wote huo ni vigumu sana. Utamsaidia yupi na kumuacha nani? Hawa wanaomba wote wametoka wapi? Ufumbuzi ni kwenye jamii. Kama jamii inapata msaada katika kutengeneza jamvi ambalo linasaidia katika kuweka mazingira ambayo inawasaidia vilema na vipofu basi changamoto haitaangukia sehemu moja tu wala katika sehemu moja ya jamii.

Ni muhimu uvumbuzi upatikane pale tatizo lipo. Ni mikoa gani ambayo inayo watu ambao wapo mitaani na kuomba, ni tabia yao au ni matatizo katika hizo sehemu? Je, jamii katika hizo mikoa, wilaya wakipata msaada wa kuanzisha miradi tofauti kwa wale ambao wanaweza kujihudumia? Je, hii inaweza kupunguza wanaomba mitaani? Uzee na magonjwa yanachangia katika hali tunayoiona mitaani?

 

Wazee wengi hawana mahali pa kwenda na baadhi hawana chakula.  Kulima hawawezi  pensheni  hawana. Je, hii hali itabadilika vipi? Kupitia jamvi la jamii pale jamii nzima inachukua majukumu yake? Na kupitia hiyo jamii Serikali inaweza kutoa msaada? Hapa ni moja ya shughuli  diaspora wanaweza kufanya. Ukifunguliwa mfuko wa Serikali au taasisi ambayo inatengeneza miundombinu ya kusaidia wazee na vilema na watekelezaji wakawa diaspora wenyewe pamoja na ofisi ya Waziri Mkuu na Ustawi wa Jamii matatizo kama haya yatakuwa ni hadithi tena. 

Haihitaji hela nyingi kutoka kwa kila Mtanzania na watu wenye asili ya Kitanzania wakawa kila mwezi wanatoa hela na kuweka kwenye huo mfuko wa kijamii. Diaspora wanaweza na huu mchango kwa jamii za nyumbani. Ikiwekwa mipango madhubuti hili suala la watu kuomba mitaani kwa sababu ya matatizo au uzee tutalimaliza. Kila jamii inafahamu ni watu gani wanahitaji msaada na itaweza kuangalia na kuona kwamba hawa watu wanapata msaada unaotakiwa. Kwa ujmla ni suala la ushirikiano kati ya diaspora, taasisi yao na Serikali. 

Kwenye hili jamvi la jamii liwepo kwenye kila sehemu wilaya zipewe uwezo wa kuamua ni sehemu gani inahitaji msaada sana, lakini lengo liwe kusaidia wazee na vilema, moja kwa moja au kupitia shughuli za katika jamii. Baadhi yetu wataona hii ni kama kuazima jamvi kilioni.

Ukisha fahamu hilo, iliyobaki ujipange na kutimiza malengo yako.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles