22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

Azam yaishusha Yanga kileleni

Pg 32 feb 12NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), Azam FC, jana walirejea kuongoza ligi kwa kishindo baada ya kuibamiza bila huruma Mtibwa Sugar mabao 5-2 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Kwa matokeo ya jana, Azam imefikisha pointi 25 sawa na Yanga lakini zikiwa zimetofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Azam ilianza kupata karamu hiyo ya mabao kupitia kwa mshambuliaji wake wa kimataifa, Didier Kavumbagu dakika ya 19, aliyeunganisha vema pasi ya ndefu ya Brian Majegwa.
Kiungo Frank Domayo aliyerejea uwanjani baada ya kuwa majeruhi muda mrefu, aliwainua mashabiki wa Azam dakika ya 29 alipofunga bao la pili akimalizia mpira wa krosi iliyochongwa na Majegwa.
Kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime, alifanya mabadiliko ya kumtoa Henry Joseph na kumwingiza Ally Sharifu ambaye alitengeneza pasi iliyozalisha bao lililofungwa na mshambuliaji Mussa Mgosi dakika ya 35.
Dakika ya 40, Kavumbagu aliandika bao la tatu kwa timu yake akiunganisha vema krosi iliyopigwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na kuifanya Azam kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao matatu.
Kipindi cha pili kilianza kwa Mtibwa Sugar kumtoa Ally Lundenga na nafasi yake kuchukuliwa na Vicent Barnabas huku Azam ikimtoa Michael Bolou na kumwingiza Mudathir Yahaya.
Domayo aliongeza bao la nne dakika ya 58 baada ya kutokea piga nikupige langoni kwa Mtibwa ambao walizinduka na kupata bao la pili dakika ya 70 kupitia kwa Ame Ally.
Mwamuzi wa mchezo huo aliwaonya kwa kadi za njano, Majaliwa Mbaga na Shabani Nditi wa Mtibwa kwa kumchezea madhambi Kipre Tchetche wa Azam.
Azam ilihitimisha karamu yake ya mabao dakika ya 86 baada ya Tchetche kufunga bao la tano akimalizia pasi ndefu ya Shomari Kapombe.
Mtibwa Sugar ilifanya tena mabadiliko ya kumtoa Ally Lundenga na Mussa Mgosi na nafasi zao kuchukuliwa na Vicent Barnabas na Abdallah Juma na Azam kuwatoa Bolou, Erasto Nyoni na Kavumbagu na nafasi zao kuchukuliwa na Mudathir Yahaya, John Bocco na Hamis Mcha.
Azam: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni/John Bocco, Sid Moradi, Serge Wawa, Michael Bolou/Mudathir Yahaya, Kipre Tche tche, Frank Domayo,Didier Kavumbagu/ Khamis Mcha, Salum Abubakar na Brian Majegwa.
Mtibwa: Said Mohamed, Andrew Vicent, Majaliwa Mbaga, Ally Lundenga/Vicent Barnabas, Salim Mbonde, Shabani Nditi, Ramadhani Kichuya, Mussa Nampaka, AMe Ally, Henry Joseph/Ally Sharif na Mussa Mgosi/Abdallah Juma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles