24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Msajili awapa kina Zitto ACT yao

Zitto Kabwe
Zitto Kabwe

NA MICHAEL SARUNGI, DAR ES SALAAM

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imebariki mabadiliko ya uongozi yaliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa muda wa chama cha ACT-Tanzania, Samson Mwigamba na Kaimu Mwenyekiti wake, Shaaban Mambo.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya viongozi wa chama hicho kutuhumiana hadharani kuwa kila mmoja anakivuruga chama na kusababisha Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kuingilia kati.
Chama hicho kwa muda mrefu kimekuwa kihusishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kuwa ni mmoja ya waasisi wake, ingawa kwa sasa bado anatambulika kuwa mwanachama wa Chadema.
Katika barua yake yenye kumbukumbu namba HA.322/362/20/40 kwenda kwa Kadawi Limbu, aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Tanzania, Jaji Mutungi alisema anakubaliana na mabadiliko ya uongozi yaliyofanywa na Halmashauri Kuu kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho ibara ya 37(q) (iii), ambayo inaeleza kuwa Sekretarieti ya Kamati Kuu ndiyo yenye jukumu la kuandaa ajenda na nyaraka kwa ajili ya vikao na si vinginevyo.
“Ushauri wa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa mujibu wa Katiba ya ACT na mabadiliko yaliyowasilishwa na Samson Mwigamba na Kaimu Mwenyekiti Shaaban Mambo ndiyo halali,” ilisema barua ya msajili.

LIMBU AIBUKA

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana baada ya kukabidhiwa barua katika mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na vyama vya siasa, aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT, Limbu, alisema hakubaliani na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa na sasa anajipanga kwenda mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
“Demokrasia katika nchi hii kwa muda mrefu imekuwa ikigandamizwa na ofisi ya msajili kwa kushindwa kufuata misingi ya haki. Ofisi ya msajili haitakiwi kutumiwa na watu kwa masilahi yao binafsi, badala yake itumike kwa masilahi ya taifa.
“Nasema hivyo kwa sababu tangu kuibuka kwa mgogoro ndani ya chama chetu, ofisi ya msajili imeonyesha kuegemea upande mmoja na kusahau kuwa wao ni walezi wa watu wote.
“Ushahidi wa hili, ni kwamba kuna barua nimepewa kutoka ofisi hiyo ya msajili na ina baadhi ya viambatanisho ambavyo si vya kweli.
“Barua hiyo ya msajili kuna kiambatanisho cha barua ya kumbukumbu namba HA.322/362/20/21 ya tarehe 17 Desemba 2014 na nyingine yenye kumbukumbu namba HA.322/362/20/22 ya tarehe 23 Desemba hazijanifikia,” alisema Limbu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa muda wa chama hicho, Mwigamba, alisema kwa mujibu wa Katiba ibara ya 37(o), Mwenyekiti wa sekretarieti ya kamati kuu ni Katibu Mkuu na mwenyekiti wa taifa siyo mjumbe wa vikao vya sekretarieti ya Kamati Kuu na hakuna sehemu inayomtaja mwenyekiti.
Alisema kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Ofisi ya Msajili kwenda kwa Limbu tarehe 10, ofisi ya msajili imejiridhisha kuwa vikao vyote alivyokuwa akiviitisha havikuwa halali.
“Ofisi ya msajili imetupangia kufanya uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya chama kabla ya Mei 5, mwaka huu,” alisema Mwigamba.
Alisema wao kama viongozi hawatakuwa na kinyongo kwa mtu yeyote atakayejitokeza kutaka kuwania uongozi ndani ya chama, hata kama ni Limbu ambaye wana mgogoro naye.
Desemba 12, mwaka jana, ACT-Tanzania ilitangaza rasmi kuwa mwasisi wa chama hicho ni Zitto, ambaye kwa sasa bado anatambulika kuwa mwanachama wa Chadema.
Siri hiyo iliwekwa hadharani na Makamu Mwenyekiti wa ACT, Mambo, wakati akinadi kwa wananchi wagombea wa uenyeviti wa Serikali za Mitaa kupitia chama hicho kipya, katika mitaa ya Majengo pamoja na Nyasubi katika uwanja wa Lumambo.

Kutokana na kauli hiyo, alipotafutwa Zitto atoe ufafanuzi, alikataa kukiri wala kukanusha madai hayo ya ACT.
Hii si mara ya kwanza kwa Zitto kuhusishwa na chama hicho, ambapo Mei mwaka huu alipohojiwa na kituo cha redio cha Clouds Fm, alikaririwa akisema hawezi kukubali au kukanusha kuwa mwanachama wa ACT, hadi hapo kesi ya msingi dhidi ya uanachama wake Chadema itakapotolewa uamuzi mahakamani.
Aliulizwa swali hilo, baada ya Profesa Kitila Mkumbo ambaye alitimuliwa Chadema pamoja na Mwigamba, huku Zitto akikimbilia mahakamani kulinda uanachama wake, kumtaka rafiki yake huyo kuhamia ACT na kugombea nafasi ya uenyekiti.
Profesa Mkumbo katika maoni yake kwa Zitto, alikaririwa akisema kiongozi huyo kijana hawezi kupata mafanikio zaidi ya kisiasa ndani ya Chadema, isipokuwa kama ataamua kuhama chama hicho.
Zitto alipohojiwa na Clouds kuhusu kauli hiyo, alisema yeye na Profesa Mkumbo wana mrengo wa siasa unaofanana, unaoamini katika maendeleo na maslahi ya jamii kwa ujumla na sio chama wala watu wachache.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles