29 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri wa Z’bar leo kuongoza maandamano ya CUF Dar

MINOLTA DIGITAL CAMERANA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimetangaza maandamano yanayofanyika leo jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Waziri wa Miundombinu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Juma Duni Haji.
Duni ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CUF, anatarajiwa kuwaongoza wafuasi wa chama hicho katika maandamao hayo licha ya Jeshi la Polisi kuyazuia.
Mbali ya Waziri Duni, maandamano hayo pia yataongozwa na viongozi wengine waandamizi wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa CUF (JUVCUF), Hamidu Bobali, alisema lengo la maandamano hayo ni kupinga uvunjwaji wa haki za binadamu na kuishinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), iongeze muda wa uandikishaji wapigakura.
Alisema hatua ya Jeshi la Polisi kutumia nguvu dhidi ya raia, inastahili kupingwa na kila mpenda amani kwani imekuwa ni mazoea yao kuwadhalilisha viongozi wa vyama vya upinzani pamoja na raia pindi wanapokuwa katika maandamano.
Bobali alipoulizwa kama maandamano hayo yamepata baraka za Jeshi la Polisi, alisema wao kazi yao ni kutoa taarifa na wamefanya hivyo, lakini katika hali ya kushangaza waliitwa na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kutakiwa kuyaahirisha.
“Tulitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuwa leo tunafanya maandamano kwenda NEC na lengo kubwa ni kuwataka waongeze siku za uandikishaji wapigakura kutoka 7 kwa kila mkoa na kuwa 14. Pia maandamano haya yatafikisha ujumbe wa kulaani ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na polisi nchini.
“Lakini katika kikao kilichoongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi wa Kanda Maalumu, Simon Sirro, aliwataka Naibu Katibu Mtendaji wa JUVICUF, Maulid Said na ofisa wa chama, Masoud Said, kusitisha maandamano hayo kwa kile walichodai Ijumaa ni siku ya kazi.
“Kamishna Sirro alisema maandamano hayo yatasababisha msongamano wa magari na watu pamona na kuathiri huduma mbalimbali za kijamii.
“Lakini kutokana na umuhimu wa hoja tunazotaka kuwasilisha, tunatamka kuwa tutaendelea na maandamano kama tulivyopanga na tunawakaribisha vijana wa vyama vingine vya Ukawa pamoja na Watanzania wapenda haki wajitokeze kwa wingi.
“Polisi wajipange waje na mabomu na risasi, sisi tutaendelea na maandamano. Hatuna nguvu za kupambana nao, lakini tutajitetea,” alisema Bobali.
Alisema maandamano hayo yataanza saa nne asubuhi eneo la Buguruni Rozana na kupitia barabara ya Uhuru, Bibi Titi, Mtaa wa Ohio hadi Makao Makuu ya NEC.

KAULI YA POLISI
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesisitiza kuwa hawatoruhusu maandamano ya Jumuiya ya Vijana CUF (JUVICUF).
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salam, Kamishna Suleimani Kova, alisema wameyazuia maandamano hayo kwa sababu ni siku ya kazi na yanaweza kusababisha msongamano mkubwa wa magari na watu.
“Barua yao ya maombi ilieleza kuwa maandamano hayo yangetakiwa kuanzia Buguruni kupitia Shule ya Uhuru, Mnazi Mmoja kisha kupitia katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi, kuingia barabara ya Ohio hadi Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Wizara ya Mambo ya Ndani.
“Baada ya kupata taarifa hiyo, uongozi wa jeshi uliwaita viongozi wa JUVICUF Taifa na Naibu Katibu wa Vijana CUF Taifa, Masoud Said na ofisa wa chama hicho ili waongozane na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Constantine Masawe, kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupata ufumbuzi wa maoni yao,” alisema Kova.
Alisema waliwaita viongozi wa CUF na kufanya mazungumzo ya namna ya kupata ufumbuzi wa maandamano hayo, lakini walikataa ushauri waliopewa na uongozi wa polisi.
“Inaonekana lengo la maandamano hayo ni kuleta fujo na kuvuruga amani na utulivu uliopo katika jiji hili na tuliwaandikia barua yenye kumbukumbu namba DSMZ/SO.7/2/A/VOL.XIII/3 ya kuwataka kusitisha maandamano,” alisema.
Kamanda Kova alisema suala la kulaani ukiukwaji wa haki za binadamu ni la kisheria na linashughulikiwa kwa mujibu wa sheria, pia alizungumza kwa msisitizo kuwa ni marufuku kufanyika kwa maandamano hayo.
Januari 27, mwaka huu Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahimu Lipumba pamoja na wafuasi 32 walikamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kufanya maandamano yasiyo halali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles