26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 5, 2023

Contact us: [email protected]

Azam FC watekeleza agizo la Rais

picha pg 32NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

TIMU ya Azam FC jana ilitekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli la kufanya usafi wakati wa maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika.

Katika kutekeleza agizo hilo, Azam saa 12.30 asubuhi ilitembelea Zahanati ya Chamazi na kufanya usafi kwa muda wa takribani saa mbili na nusu.

Wachezaji wa Azam kwa kushirikiana na wafanyakazi na viongozi walishiriki zoezi hilo, ambapo watu mbalimbali wanaoishi maeneo ya karibu na zahanati hiyo walionekana kufurahia kitendo cha usafi uliofanywa na timu hiyo.

Katika mtandao wa klabu hiyo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba, alisema wanamshukuru Mungu kwa hatua waliyofikia na kuelezea furaha yake kutokana na kufanikiwa kwa jambo hilo ambalo walilipanga.

“Tulipanga kufanya jambo hili tangu siku ambayo Rais alitangaza kuwa leo (jana) siku ya Uhuru wa Tanganyika itakuwa ni usafi, tukaona sisi Azam tuna jukumu la kushiriki katika kampeni hiyo na tukachagua kwa majirani zetu badala ya kwenda shule au sokoni.

“Tunashukuru shughuli yetu imekwenda vizuri kwa kiwango tulichotarajia, nafsi zetu zimeridhika kwa kujitolea kwenye jamii na ukizingatia kwamba timu ya Azam inacheza mpira kutokana na mashabiki.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Zahanati hiyo, Mohamed Hassan, aliipongeza na kuishukuru Azam FC kwa kufika hospitalini hapo na kufanya usafi.

“Azam wana tabia ya kuangalia kwanza maeneo ya majirani zao ndiyo maana hawakuona sababu ya kwenda sehemu nyingine kwa kuwa wanapita hapa na pia wachezaji wao wakiugua watawaleta hapa,” alisema.

Naye Salim Juma ambaye ni mchezaji wa timu ya Azam Academy, alisema wanajisikia furaha kuwajibika kufanya usafi ili kuhakikisha usafi unatawala katika nchi yetu.

“Napenda kutoa wito kwa vijana wengine kuwa tushirikiane kuhakikisha tunasafisha jiji letu, ili kuepuka magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles