24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka 54 ya uhuru, Watanzania hawakuwa huru

NA ELIZABETH HOMBO
ELIZA2.indd

LEO Watanzania  wanasherehekea  miaka 54 baada ya Taifa hili kujinasua kutoka kwenye minyororo ya wakoloni wa Uingereza.

Historia inaonyesha kuwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Umoja wa Mataifa(UN) uliwapa dhamana Uingereza kuitawala Tanganyika mpaka hapo wananchi wake watakapopata ufahamu wa kudai uhuru wao.

Kabla ya Uingereza kupewa dhamana ya kuiongoza Tanganyika, nchi hii ilikuwa chini ya himaya ya koloni la Ujerumani.
Uhuru wa Taifa hili umepita katika mapito mbalimbali na dhana kadha wa kadha za kifikra na kimfumo kuanzia sera za ujamaa na kujitegemea hadi sasa ambapo Taifa lipo katika mfumo mseto kuelekea ubepari.
Mwanzoni mwa uhuru wa Tanganyika, kila mmoja alitarajia kujengwa kwa Taifa lenye mgawanyo sawa wa rasilimali ili kuwanufaisha wananchi wote.
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius  Nyerere, baada ya Tanzania kuwa huru, alihaha kuhakikisha Watanzania wananufaika na uhuru walioupata, akianza na kuhubiri mfumo wa maisha ya Ujamaa na Kujitegemea.

Sambamba na hilo, alihakikisha kila Mtanzania anapata elimu ili kuondokana na ujinga alioutambulisha kama ni adui mkubwa wa maendeleo ya Taifa letu, hivyo kuanzisha kampeni ya elimu ya watu wazima, huku kwa wale waliokuwa kwenye mfumo rasmi wa elimu, wakisoma bure.

Ili kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri, Mwalimu Nyerere alijenga misingi ya utu na usawa miongoni mwa Watanzania ambayo ilikemea aina zote za ubaguzi, kuanzia wa rangi, dini, kabila, ukoo, majimbo na mengineyo.
Lakini pia, Mwalimu Nyerere tangu Tanzania ilipopata uhuru hadi alipofariki dunia, alichukia watu ambao walitanguliza mbele maslahi yao binafsi, huku walio wengi wakiishi maisha ya kutaabika.

Katika mambo aliyoyaamini na kuyatilia mkazo, ni pamoja na masuala ya haki na usawa miongoni mwa Watanzania.
Alipinga mianya ya unyonyaji aliyoiita ‘mirija’, ikiwa ni pamoja na kupinga sera zozote zinazoweza kuzalisha matabaka ya kiuchumi hasa kundi la walionacho na wasionacho.

Mwasisi huyo wa Taifa la Tanzania, alihakikisha ubinafsi na ufisadi ambao leo hii umekithiri miongoni mwa viongozi na watendaji serikalini katika taasisi binafsi, hauna nafasi.
Hayo ni baadhi ya matarajio ya Watanzania waliyokuwa nayo mara baada ya kupata uhuru ambao Mwalimu Nyerere alipambana vilivyo kukabiliana nayo.
Leo hii tukiadhimisha siku ya Uhuru wa Tanzania, kuna mambo ambayo yanaonekana kwenda kinyume na matarajio ya wengi kama Taifa lilivyokuwa likihubiriwa na waasisi wake wakati nchi ilipotoka mikononi mwa wakoloni.

Baadhi ya mambo ambayo ndiyo makubwa zaidi ni ufisadi uliokithiri, ukifanywa zaidi na watendaji wa taasisi za umma wanaoshirikiana na wafanyabiashara binafsi.
Mengine ni kuwapo kwa pengo kubwa kati ya matajiri na masikini, matabaka katika huduma mbalimbali kama elimu, afya na nyinginezo kama hizo.

Hali hiyo imewafanya baadhi ya Watanzania kujiona kama hawapo huru ndani ya nchi yao iliyopata uhuru kutokana na kuhangaika katika kupata huduma mbalimbali za kijamii kama vile elimu, afya, maji safi, ajira, ardhi na nyinginezo.

Na baada ya Watanzania kuonekana kukata tamaa ya kupata kiongozi ambaye angeonyesha nia ya dhati kabisa kupigania maisha ya walio wengi na kuwabana watendaji wanaotanguliza maslahi yao mbele, hatimaye amepatikana ambaye angalau ameanza kuonyesha dalili ya kutekeleza yale waliyokuwa yakitarajiwa na wananchi mara baada ya kupata uhuru.

Huyo si mwingine, bali ni Dk. John Magufuli ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

SIKU 33 ZA MAGUFULI
Ndani ya siku zake 33 alizokuwapo madarakani, Rais Magufuli ameonyesha wazi shauku ya Watanzania kuyaona au kuyapata yale waliyokuwa wakiyategemea baada ya kupata uhuru ambao sherehe zake zinaadhimiswa leo.
Ndani ya siku zake hizo chache, angalau ameanza kurejesha nidhamu ya kazi miongoni mwa watendaji, baada ya kuhimiza suala zima la kila mmoja kufanya kazi kadiri ya uwezo wake kwa manufaa ya Taifa la Tanzania.

Kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ imeonekana kueleweka katika ofisi zote za Serikali na hata binafsi kwani kwa sasa watendaji wameonekana kujituma na kutanguliza utu mbele tofauti na ilivyokuwa miaka ya hivi karibuni.
Kubwa zaidi, Rais Magufuli ameonyesha uzalendo wa kweli ambao ndio hasa Mwalimu Nyerere aliokuwa akiupigania baada ya kupata uhuru kutokana na Rais huyo wa Awamu ya Tano kuonyesha dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi, sambamba na rushwa.

Katika hilo, amepiga marufuku matukio yoyote yenye kuambatana na matumizi makubwa ya fedha za umma kama safari za nje kwa viongozi zisizo za lazima, sherehe za matukio mbalimbali kama maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, makongamano pamoja na kuagiza semina zote za taasisi za serikali kufanyika katika kumbi za ofisi husika badala ya kwenye hoteli za kifahari.

Lakini pia, Rais Magufuli ameigusa siku ya leo ya maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania baada ya kuagiza tukio hilo kuadhimishwa kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali badala ya gwaride pekee ambalo lilikuwa likitumia kiasi kikubwa cha fedha za umma ambazo zingesaidia katika mambo mbalimbali kama vile elimu, afya, maji, barabara na mengineyo.

Kwanini tunasherehekea uhuru?

Tunasherekea uhuru ikiwa ni alama inayodhihirisha kukumbuka namna Hayati Mwalimu Nyerere na wenzake walivyopigania uhuru wa Tanzania kutoka kwa mkoloni.

Hivyo kilicho muhimu hapo ni kumbukumbu na kuenzi na si kwa kutumia fedha kwa ajili ya sherehe wakati taifa letu ni masikini.

Kabla ya uamuzi wa Rais Magufuli kufuta sherehe za uhuru, maadhimisho yalikuwa yakiambatana na gwaride linalojumuisha vikosi vyote vya halaiki na kuvuta viongozi mbalimbali wa ulinzi na usalama, ngoma, muziki na wageni kutoka nchi za nje ambao baadaye jioni yake walijumuika kwenye dhifa ya kitaifa inayoandaliwa na mkuu wa nchi.

Maandalizi na sherehe hizo vimekuwa vikitumia mabilioni ya fedha za walipa kodi katika kulipa posho askari wanaoshiriki kwenye gwaride hilo, watumishi wa umma na watoto wanaocheza halaiki, kununua fulana na vitenge, vyakula, vinywaji, mafuta ya magari, vipeperushi, mapambo na gharama nyingine kwa ajili ya wageni wa ndani na nje ya nchi.

Baada ya kufuta sherehe hizo, Rais Magufuli aliagiza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo kutumika kupanua Barabara ya Mwenge hadi Morocco, jijini Dar es Salaam, yenye urefu wa kilometa 4.3 kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami.

Kwa haya machache ambayo Rais Magufuli ameyafanya hadi sasa, angalau ameonyesha kuwa mzalendo wa kweli anayeweza kuwafanya Watanzania walio wengi kufurahia kuwa huru tofauti na ilivyokuwa awali.
Mwenendo huu wa uongozi wa Rais Magufuli alioanza nao iwapo utaendelea, itadhihirisha pasipo shaka kwamba huko nyuma tulikosa uongozi bora.

Haiwezekani kiongozi mwenye nia ya dhati ambaye anashuhudia namna Watanzania wanavyoteseka na ugumu wa maisha, aruhusu mabilioni ya fedha kutumika kwenye sherehe ambazo hazina tija kwa taifa letu.

 

 

Magufuli akosa gwaride la kwanza

Kwa kawaida sherehe za uhuru huwa zinatoa fursa kwa Rais aliyeingia madarakani kukagua gwaride lake la kwanza, hivyo kutokana na Rais Magufuli kufuta sherehe hizo, kitendo hicho kimemkosesha kupigiwa gwaride la kwanza.
Pia, historia inaonyesha kwamba tangu Taifa hili lipate uhuru hakuna rais ambaye alipata kuahirisha sherehe hizo isipokuwa Magufuli.

Magufuli awagusa wengi

Tangu Rais Magufuli alipotangaza kuwa sherehe za uhuru zitafanyika kwa ajili ya kufanya usafi huku akiagiza kuwa fedha hizo zitumike kwa ajili ya kujenga barabara, wapo wengi waliofurahia uamuzi huo wakisema pengine sasa Tanzania mpya inakuja.

Pamoja na hilo pia wapo ambao walisema hiyo itakuwa ni nguvu ya soda huku wakifananisha na utawala wa Jakaya Kikwete kwamba hata wakati wake alianza hivyo lakini baadaye akawa kimya.

Edwin Mtei anena

Mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edwin Mtei ambaye pia alikuwapo wakati wa harakati za uhuru, anasema ni miaka mingi Taifa limekuwa likichezea fedha kwenye sherehe za uhuru, hivyo kitendo cha Rais Magufuli kufuta sherehe hizo kitakuwa na faida kubwa kwa wananchi.

“Sasa tunaokoa fedha za walalahoi, kwa sababu miaka yote serikali imekuwa ikichezea fedha za walipa kodi kwa gwaride, kula, kunywa na kulewa huku Watanzania wengine wakikosa hata mlo moja kwa siku.
“Haiwezekani fedha zichezewe kwenye mambo ya sherehe wakati Watanzania wengi ni masikini. Tunaomba huyu rais mpya aendelea hivyo asipotee njiani,”anasema Mtei.

Pius Msekwa

Kwa upande wake mwanasiasa mkongwe na aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali tangu wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, Pius Msekwa anasema uamuzi wa Rais Magufuli ni wa kuungwa mkono na kila mmoja ambaye analitakia mema taifa hili.

“Maadhimisho miaka yote yalikuwa yakifanyika kwa shamrashamra ambapo imekuwa ikifanyika Dar es Salaam tu, lakini mwaka huu ni nchi nzima kwa kufanya usafi. Tunamuombea Magufuli aendelee hivi hivi ili Watanzania waweze kuondokana na umasikini kwani kwa kufuta sherehe hizi tunaokoa mabilioni ya fedha,”anasema Msekwa ambaye pia alipata kuwa Spika wa Bunge.

Profesa Lipumba

Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba anashauri kuwa sherehe kubwa kama uhuru ifanyike mara moja ndani ya miaka mitano.

“Kwa mfano mwaka huu tunakumbuka siku ya uhuru kwa kauli mbiu ya uhuru na kazi kusherekea kwa kufanya usafi, lakini pia tunaweza tukajiwekea utaratibu katika sherehe kubwa ya kumbukumbu ifanyike mara moja kwa miaka mitano.

“Yaani shamrashamra iwe mara moja kwa kipindi cha miaka mitano na miaka mingine ifanyike kwa utaratibu kama wa mwaka huu,”anasema mtaalamu huyo wa uchumi.
Dk. Bana
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana anasema uamuzi alioufanya Rais Magufuli ni wa tija kwa sababu haiwezekani kusherehekea kwa kula na kunywa huku wananchi wakiwa wanafariki kwa kipindupindu.

“Lazima tutafakari kwamba tangu tulipopata uhuru je umetusaidiaje? Lazima twende na wakati kwamba zama za kutumbua zimepita na sasa hapa tulipo ni zama za kutafakari kwa njia ya tija kwamba nchi yetu tunaifanyia nini.
“Kwanini tusononeke wakati watu wanakufa na kipindupindu. Sherehe yoyote ni kumbukumbu. Unasherekea nini wakati tunaumia, tunasononeka,” anahoji Dk. Bana.

Hakika utendaji kazi huu wa Rais Magufuli, ukiendelea hadi mwisho wa utawala wake utaondoa miaka ile 54 ya ‘uhuru bandia’ na kuwaletea wananchi uhuru halisi, ambao wanafurahia utu na matunda ya rasilimali zao.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles