23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

ASKOFU MALASUSA KUJADILIWA LEO

Na Mwandishi wetu – Dar es Salaam


KIKAO cha Halmashauri Kuu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, inatarajiwa kukutana leo kujadili hatima ya Askofu Dk. Alex Malasusa, ambaye ametengwa na Baraza la Maaskofu wa kanisa hilo.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kanisa hilo, jana kililiambia gazeti hili kuwa maamuzi ya baraza hilo ndiyo yatatoa hatima ya uaskofu wa Malasusa.

Mkutano huo baadhi ya wajumbe wake ni wachungaji wa makanisa yaliyo ndani ya dayosisi na uamuzi wake hufanyika kwa kupiga kura.

Gazeti hili lilimtafuta Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Godfrey Nkini, ili kuweza kuthibitisha taarifa hizo, lakini simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa.

Mwishoni mwa wiki, Baraza la Maaskofu wa kanisa hilo lilifikia uamuzi wa kumwadhibu Askofu Malasusa kwa kumtenga na kuwapa masharti maaskofu wengine wawili kuomba msamaha kwa tuhuma za usaliti.

Maaskofu ambao wametakiwa kuomba msamaha hadi Septemba mwaka huu pamoja na Malasusa, ni Askofu wa Dayosisi ya Kusini na Mashariki, Lukas Mbedule na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini na Kati, Solomoni Massangwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya dayosisi wanazoziongoza kutousoma waraka wa Pasaka ulioandaliwa na maaskofu wapatao 27 wa kanisa hilo.

Wakati Mbedule akiitumia Jumapili ya juzi kuomba radhi waumini wake na hivyo kunusurika mtego wa kutengwa, dayosisi inayoongozwa na Askofu Malasusa inajiandaa kukutana ili kulimaliza jambo hilo.

Gazeti hili limedokezwa kikao hicho ndicho ambacho kinaweza kutoa mwanga kuhusu hatima ya uaskofu wa Dk. Malasusa.

“Unajua kwa utaratibu wa KKKT, dayosisi zake zote 25 zinaongozwa na ama katiba au kanuni, sasa zipo dayosisi ambazo zina katiba na nyingine hazina, zile ambazo hazina zinafuata katiba mama ya kanisa.

“Sasa Dayosisi ya Mashariki na Pwani yenyewe haina katiba, inategemea ile ya kanisa, ina kanuni tu na ndiyo maana unaona hata uamuzi wa Baraza la Maaskofu dhidi yake umefanyika tofauti na maaskofu wale wengine wawili ambao hawajatengwa bali wamepewa adhabu,” alisema mchungaji mmoja aliyezungumza na gazeti hili.

Mchungaji huyo alisema pamoja na utaratibu huo, kikao ambacho  wametaarifiwa kinatarajiwa kuitishwa na Halmashari Kuu ya Dayosisi, kitajadili uamuzi huo wa Baraza la Maaskofu na kimsingi ndicho ambacho kinaweza kuja na majibu zaidi kuhusu hatima ya Dk. Malasusa na nafasi yake.

Chini ya utaratibu wa kanisa hilo, inaelezwa pamoja na kwamba linaongozwa na Baraza la Maaskofu, lakini uamuzi wa kumvua uaskofu Dk. Malasusa uko chini ya dayosisi anayoiongoza.

Jana gazeti hili liliwasiliana na Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Nkini, kuhusu kuwapo maandalizi ya kikao hicho cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi, lakini alisema bado hawajaitisha.

Alipoambiwa gazeti hili limesikia kwamba tayari baadhi ya wachungaji wanafahamu kuhusu maandalizi ya kikao hicho, Nkini alihoji mtu anayetoa taarifa hizo na kisha akakata simu.

Jumapili, gazeti hili liliandika juu ya uamuzi huo uliofikiwa na Baraza la Maaskofu wa KKKT kuwa pamoja na mambo mengine unamweka Askofu Malasusa katika wakati mgumu zaidi, ikiwa hata kuupoteza uaskofu wake iwapo hatatimiza sharti la kuomba msamaha.

Inaelezwa iwapo Askofu Malasusa atapuuza suala la kuomba radhi, huenda akakumbana na kukataliwa na wachungaji wa dayosisi yake, ambao kimsingi baadhi yao ndio waliopeleka taarifa za kumshtaki kwenye kikao cha Baraza la Maaskofu, wakidai kuzuiwa kuusoma waraka huo.

Jana kwa mara nyingine tena, gazeti hili lilimtafuta Askofu Malasusa ili kufahamu iwapo ataliomba radhi kanisa kama alivyoelekezwa na kikao hicho cha Baraza la Maaskofu baada ya kupewa muda wa kujitafakari, lakini hakupatikana.

Ingawa inaelezwa katika kikao cha Baraza la Maaskofu alijaribu kuomba msamaha, lakini alikataliwa na kupewa muda wa kutafakari zaidi hadi  Septemba, mwaka huu.

mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles