25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Asilimia 92 wajawazito Simiyu wanajifungulia vituo vya Afya

Na Derick Milton, Simiyu

Mkoa wa Simiyu umefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuongeza idadi ya wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya, hali ambayo imepunguza kwa vifo vitokanavyo na uzazi.

Takwimu zinaonyesha kuwa idadi hiyo imeongeza kufikia asilimia 92 ndani ya kipindi cha miaka minne kutoka asilimia, 68 Mwaka 2017.

Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Boniphace Marwa, wakati wa mkutano wa kuhitimisha mradi wa Uzazi Uzima awamu ya pili mkoani humo, ambao ulikuwa unatekelezwa na Shirika la Amref Health Africa Tanzania kwa Ufadhili wa Serikali ya Canada.

Dk. Marwa amesema kupitia mradi huo ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2017 mkoani hapa, Amref wamewezesha kuboreshwa kwa mazingira ya utolewaji wa huduma za uzazi tofauti na ilivyokuwa awali.

Amesema kupitia mradi huo, Amref wamekarabati na kujenga vituo vya kutolea huduma 24 ikiwa pamoja na kuchimba visima 10 kwenye vituo hivyo pamoja na kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watoa huduma za Afya.

“Kabla ya mradi mazingira kwa wajawazito hayakuwa rafiki, lakini kupitia Uzazi uzima mazingira yameboreshwa kwa kiwango kikubwa, wahudumu wamejengewa uwezo wa kutoa huduma rafiki kwa wateja, lakini huduma za upasuaji kusogezwa karibu.

“Maboresho haya yamefanya wajawazito kuongezeka wenyewe maana mazingira yanatunza usiri wakati wa kujifungua, lakini pia kupitia mradi huo huduma za upasuaji zinapatikana hadi kwenye vituo vya Afya tofauti na mwazo zilipatikana hospitali za Wilaya tu,” aliongeza Dk. Marwa.

Amesema kuwa kwa sasa wajawazito hawatembei umbali mrefu kwenda kujifungua hata kufuata huduma za upasuaji, hatua ambayo imepunguza kwa kiwango kikubwa vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga.

“Kupitia mradi huu ambao leo Ok unafikia mwisho, Amref wamewezesha kupata vifaa vya kisasa vya upasuaji, huduma bora za usingizi, mafunzo kwa wahudumu, pamoja na kuboresha mazingira ya wodi za wajawazito,” alisema Dk. Marwa.

Awali, akiongea katika Mkutano huo Mkuu wa Miradi Amref, Dk. Aisa Muya alisema kuwa kufikia mwisho wa utekelezaji wa mradi huo kuna mafanikio makubwa yamepatikana ikiwemo wajawazito wenyewe kwenda kujifungulia hospitali.

Dk. Muya alisema kuwa lengo kubwa la Amref ni kuendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha huduma za afya hasa katika maeneo yenye changamoto za ukosefu wa huduma pamoja na magonjwa mbalimbali.

Alisema kuwa kupitia mradi huo ambao umefadhiliwa na serikali ya Canada, wamewezesha kuboresha huduma za upasuaji kwa kuweka vifaa vya kisasa, kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za Afya pamoja na kuwajengea uwezo zaidi watoa huduma.

Mwakilishi wa Serikali ya Canada, Richard Manirabona ambao ndiyo wafadhili wa mradi huo alisema kuwa serikali ya Canada itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha huduma za Afya kwa wananchi zinaendelea kuboresha.

Alisema kwa mradi huo umekuwa unatekelezwa katika mikoa mitano hapa nchini na Simiyu ikiwemo, kutokana na maeneo yake kuwa na changamoto kubwa kwenye suala la vifo vitokanavyo na uzazi.

“Kutokana na viashiria hivyo Serikali ya Canada tulisukumwa kuamua kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuboredha huduma kwenye mikoa hiyo na tumeona kuna mafanikio makubwa ikiwemo vifo kupungua sana,” amesema Manirabona.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles