22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Asilimia 15 ya Watanzania wana seli mundu

Dk. Deogratius Soka
Dk. Deogratius Soka

NA HADIA KHAMIS, DAR ES SALAAM

UTAFITI uliofanywa na wataalamu wa magonjwa ya damu unaonyesha kuwa asilimia 12 hadi 15 ya Watanzania wana vinasaba vya ugonjwa wa seli mundu (Sickle Cell).

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mratibu wa Idara ya Magonjwa ya Damu, Kitengo cha Seli mundu (Sickle Cell) wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS), Dk. Deogratius Soka, alisema tatizo la seli mundu kwa sasa ni kubwa hali inayosababisha ongezeko la wagonjwa siku hadi siku.

Alisema katika kliniki ya wagonjwa wa seli mundu, kwa siku wanapokea wagonjwa 60 wakiwemo watoto na watu wazima.

Dk. Soka alisema kutokana na utafiti huo, Tanzania imeshika nafasi ya tano duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa seli mundu ikifuatiwa na nchi za Nigeria na India.

“Bado tatizo la seli mundu ni kubwa hapa nchini kwani utafiti unaonyesha kuwa zaidi ya watoto 11,000 huzaliwa wakiwa na tatizo la seli mundu, kati yao asilimia 70 hufariki dunia,” alisema Dk. Soka.

Alisema ugonjwa wa seli mundu unatokana na vinasaba kutoka kwa wazazi wote wawili, ambavyo haviwezi kuonekana kwa macho hadi vitakapofanyika vipimo.

“Mtoto anarithi ugonjwa wa seli mundu kutoka kwa baba na mama kwa sababu wazazi wote wawili huwa na vinasaba lakini hawajijui,” alisema Dk. Soka.

Alisema kwa wazazi walio na vinasaba vya seli mundu huwa hawaumwi wala kuonyesha dalili yoyote, hivyo ni ngumu kumtambua mzazi aliye na vinasaba hivyo kwa kumwangalia kwa macho.

Dk. Soka alisema wapo watu wanaodai kuwa wagonjwa wa seli mundu hawana uwezo wa kuishi kwani hufariki pindi wafikishapo miaka miwili kitu ambacho si cha kweli.

Alisema mgonjwa wa seli mundu ana uwezo wa kuishi na kufanya kila kitu kama walivyo binadamu wengine.

Kutokana na hali hiyo na kwa kutambua changamoto hizo zinazoendelea kuwakumba wagonjwa wa seli mundu, Taasisi ya Chuo cha Afya Muhimbili imeandaa kongamano litakalowashirikisha wagonjwa wa seli mundu pamoja na wadau mbalimbali litakalofanyika Juni 17, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles