23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Asasi hewa 3,000 za kiraia, kidini zabainika

Mary Komba
Mary Komba

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

UCHAMBUZI uliofanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), umebaini kuwako kwa asasi hewa za kiraia na kidini zaidi ya 3,000.

Asasi hizo zinajumuisha zile zenye kasoro mbalimbali ikiwamo kutokuwa na bodi ya wadhamini, kubadilisha majina bila kutoa taarifa na kuhamisha makao makuu.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi ripoti ya uchambuzi huo, Kaimu Msajili wa Asasi za Kirai na Kidini wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Mary Komba, alisema kati ya asasi 16,000 zilizosajiliwa 3,000 zilikutwa na mapungufu hayo.

“Tangu mwaka 1954, Wizara imekuwa ikisajili asasi za kidini na kiraia, tumepitia vyama 3,000 na kukuta havina sifa ya kuendelea kutambulika kwenye usajili, 1,500 navyo bado vipo kwenye hatua ya uchunguzi,” alisema.

Alisema kati ya asasi nyingi za kidini kumekuwa na migogoro mingi na hivyo kuifanya wizara kuwa na jukumu kubwa la kusuluhisha.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Kalomba, alisema wamebaini asasi 500 zinajiendesha bila ya kuwa na bodi za wadhamini jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Uhakiki ulifanyika kipindi cha miezi mitatu, jumla ya bodi za wadhamini 1,944 kati ya 5,262 ziliwasilisha taarifa zao, majalada 5,262 yalichambuliwa na kati ya hayo 4,287 tumeyahifadhi kwenye kanzi data yetu na hapo ndipo tukabaini kuwa bodi 500 za wadhamini ni mfu,” alisema.

Alisema Mei 17, mwaka huu walizitaka taasisi 200 kuwasilisha taarifa zao ndani ya siku 30 kabla hawajazifuta lakini taasisi 20 pekee ndizo zilitekeleza agizo hilo.

“Kwa msingi huo tunakusudia kuzifuta taasisi 180 ambazo hazikuleta taarifa zake. Pamoja na hizo zipo nyingine 320 ambazo zitafutwa baada ya kukutwa na mapungufu mengi,” alisema.

Alisema katika uchambuzi huo walibaini baadhi ya taasisi kushindwa kujiendesha kwani zilikuwa zikitegemea fedha za wafadhili.

“Nyingine hazikuwa na vyanzo vya mapato, mfano vyama vingi vya wakulima wa kahawa vilianzishwa kwa kupata mikopo Benki ya CRDB, mikopo ilipositishwa vikashindwa kujiendesha, vikafa,” alisema.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Baraka Leonard, alisema mashirika zaidi ya 2,000 kati ya 7,800 waliyosajili hayajawasilisha taarifa zao.

Akipokea ripoti hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema asasi zote zilizobainika kuwa na mapungufu zitafutiwa usajili wake.

“Tumebaini kuwa zipo asasi nyingi za kidini na kiraia ambazo zimesajiliwa ni hewa, mara nyingi zimekuwa zikijitokeza wakati wa uchaguzi mkuu, jambo hili si sahihi, tutazifuta zote zitakazokuwa zimeainishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles