24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Msako wa polisi wanasa kete 446 za cocaine

Naibu Kamishna Hezron Gyimbi
Naibu Kamishna Hezron Gyimbi

Na ASIFIWE GEORGE – DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema polisi wamefanikiwa kukamata kete 446 zinazodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya  aina ya cocaine.

Akizungumza na waandishi wa habari  jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna Hezron Gyimbi, alisema dawa hizo zimekamatwa katika operesheni ya kupambana na kuzuia dawa za kulevya iliyofanyika katika Wilaya ya Kipolisi Temeke.

Alisema kete hizo zilikamatwa pamoja na watu ambao hakuwataja majina yao kwasababu za kiupelelezi na kwamba sampuli ya dawa hizo imepelekwa kwa mkemia kwa ajili ya uchunguzi.

“Operesheni hii ni endelevu na watuhumiwa sitawataja kwa sasa kwa lengo la kutopoteza ushahidi na upelelezi unaendelea, utakapokamilika jalada litapelekwa kwa mwanasheria wa Serikali,” alisema Gyimbi.

Katika hatua nyingine jeshi hilo linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za ujambazi wa kutumia silaha pamoja na bunduki aina ya Mark IV yenye namba za usajili LA-227725A ikiwa na risasi sita.

“Agosti 18 mwaka huu katika eneo la Chamazi, Mkoa wa Kipolisi Temeke tuliwakamata watu watatu wakiwa na bunduki na tulipowahoji walikiri kufanya matukio ya ujambazi katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Tanga, Morogoro na Mtwara,” alisema Gyimbi.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Uswege Seleman (23) mkazi wa Magandaga Kilwa Chamazi, Hassan Abdalah (73) mkazi wa Hotel tatu Lindi, Saidi Kiwambu (39) mkazi wa Mnyagala Lindi na Hamadi Badrilu (28)  mkazi wa Chamazi.

Pia polisi wanawashikilia jumla ya watuhumiwa sugu 310 kwa makosa mbalimbali ambayo ni unyang’anyi wa kutumia silaha,   unyang’anyi wa kutumia nguvu, wizi wa kutumia pikipiki, wapiga debe, watengenezaji na wauzaji wa pombe haramu ya gongo, wauzaji na wavutaji wa bangi.

Gyimbi alisema watuhumiwa hao walikamatwa nyakati tofauti na maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na upelelezi utakapokamilika watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles