23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Arusha wasafirisha mirungi kwa madumu

JANETH MUSHI-ARUSHA

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limekamata dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilo 140, ambazo zilikuwa zikisafirishwa kwa kuwekwa kwenye madumu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana, alisema wanashikilia watuhumiwa wawili ambao walikamatwa na dawa hizo.

Kamanda Shana aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Philipo Mungasi Lairumbe na Ngaruma Nairishoo wote wakazi wa Kijiji cha Lengijave wilayani Arumeru.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa jana saa 4.15 asubuhi katika eneo la Sakina jijini Arusha wakiwa na madumu nane waliyokuwa wameyapakia kwenye pikipiki aina ya King Lion zenye namba MC 772 BVT na MC 404 CEE. 

Kamanda Shana alisema siku ya tukio polisi waliokuwa katika doria waliyatilia shaka madumu hayo na walipowasimamisha watuhumiwa hao na kuwakagua, walibaini yalikuwa yamebeba dawa hizo.

“Madumu manne yalikuwa ya lita 40 huku mengine manne yakiwa ya lita 20, tumegundua kuwa watuhumiwa wamebaini mbinu mpya za kusafirisha mirungi kupitia madumu na kuyafunga kwenye pikipiki,” alisema.

Kamanda Shana alisema mara baada ya kuwahoji watuhumiwa hao, walikiri kujihusisha na usafirishaji wa mirungi kwa njia hiyo kwa ujira wa kulipwa kiasi cha Sh 80,000 baada ya kusafirisha mzigo kutoka Namanga hadi jijini Arusha.

Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi wa polisi kukamilika huku msako wa kuwatafuta wahusika wa mzigo huo ukiendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles