24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Aliyetobolewa macho na ‘Scorpion’ hataona tena

pg-1*Madaktari wasema mishipa ya fahamu iling’olewa

*Jitahada za mama yake kutaka atolewe jicho moja ampe zakwama

*Makonda aahidi matibabu, ampa Sh milioni 10 za biashara

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MADAKTARI waliokuwa wakimfanyia uchunguzi wa kitabibu kijana Said Mrisho ambaye alishambuliwa na kutobolewa macho yake yote mawili na Salum Henjewele anayefahamika pia kwa jina la Scorpion, wamesema hataweza kuona tena.

Ripoti ya uchunguzi wa kitabibu ya madaktari iliyotolewa jana kwa waandishi wa habari na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ofisini kwake ilieleza kubaini kuwa Mrisho hataweza kuona tena kwa sababu Scorpion aliharibu kabisa mishipa ya fahamu.

Makonda aliwaambia waandishi wa habari amewaita kuwatangazia matokeo ya utafiti wa kitabibu yaliyofanywa na madaktari baada ya Mrisho na familia yake kuridhia itolewe kwa umma.

Alisema Mrisho alifanyiwa vipimo siku mbili mfululizo na timu ya madaktari bingwa wa macho, mishipa ya fahamu, mboni na ubongo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

“Shauku yetu sote ilikuwa kumsaidia Mrisho aweze kuona tena kama hapo awali lakini majibu si mazuri. Kwa mujibu wa madaktari hatuna namna ya kufanya kwa sababu yule mtu aling’oa na kuharibu kabisa mishipa ya fahamu.

“Jambo linalosikitisha ni mama yake ambaye alitamani angalau kutoa jicho moja kumsaidia mwanawe aweze kuona tena lakini haiwezekani tena.

“Serikali hatuna namna lazima tukubali matokeo, tutamsaidia Mrisho kupata macho ya bandia ambayo atawekewa Jumatatu ijayo ili kutengeneza ‘shape’ ya uso wake, tutamsaidia aweze kujifunza lugha za alama ili aweze kuwasiliana na kupata taarifa kama wengine.

“Tutampatia fimbo ili imsaidie kutembea, tutampa wataalamu wamfundishe jinsi ya kutambua kitu kilichopo mbele yake ‘sense’, tutampatia gari na dereva wa mkoa ambaye atakuwa akimpeleka kila mahali hadi atakapokuwa ameweza kuwasiliana.

“Tutampatia pia Sh milioni 10 ili aweze kuimarisha mtaji wake na ziisaidie familia yake na tutatangaza mfumo mzuri wa kumchangia kwa sababu tayari kuna watu wameanza kutumia namba yake kufanya utapeli,” alisema Makonda.

Mkuu huyo wa mkoa aliwataka wananchi kuwapuuza watu wanaotumia namba ya Mrisho kuomba msaada bali wasubiri hadi Serikali itakapotangaza namna ya kumsaidia.

“Matapeli wameanza kutapeli. Wananchi naomba msitume fedha yoyote subirini tutatangaza mfumo mzuri ili fedha hiyo iwe inamfikia Mrisho mwenyewe iweze kumsaidia kwenye maisha yake na familia yake,” alisema Makonda.

Mrisho mwenyewe alipopewa nafasi ya kuzungumza na wanahabari alisema ripoti ya kitabibu ya madaktari imemsikitisha lakini hana jinsi nyingine ya kufanya isipokuwa kumshukuru Mungu.

“Ni taarifa mbaya kwangu, nimeipokea kwa masikitiko, imenipa majonzi, nimefanyiwa vipimo mara mbili mfululizo Muhimbili lakini haiwezekani tena kuona.

Ripoti imezima ndoto zangu nyingi, nimeumia sana, naumia kusikia mama yangu akitamani kutoa jicho lake angalau moja anipe, wataalamu wamesema haiwezekani kwa sababu mishipa ya fahamu imeharibika kabisa,” alisema Mrisho.

Pia alimshukuru Makonda kwa kuahidi kumsaidia kupata matibabu na kuimarisha biashara na alitumia nafasi hiyo kuomba amjengee nyumba.

“Naiamini familia yangu, mdogo wangu ndiye anayenisaidia kwenye biashara zangu, ninapoishi nimepanga, nashukuru Mkuu wa Mkoa umeahidi kunisaidia kuimarisha biashara lakini naomba nisaidiwe nyumba maana biashara inaweza kuyumba lakini nikiwa na nyumba itanisaidia.

“Sijui Mungu amenipangia nini kwenye maisha yangu, ana mipango yake, lakini siwezi kusahau, napitia maisha magumu, naona giza,” alisema huku akilia.

Hali hiyo ilifanya kila aliyekuwa ndani ya ofisi ya mkuu wa mkoa huyo kujawa na huzuni ambapo baadhi ya waandishi na Makonda mwenyewe walianza kutokwa na machozi.

Hata walipotoka nje ya ukumbi huo, wananchi kadhaa waliofika katika ofisi hizo kupata huduma nao walionekana kuwa na majonzi huku wakieleza kusikitishwa na tukio hilo.

Mama mzazi wa Mrisho aliyejitambulisha kwa jina moja la Halima, awali alishindwa kuzungumza na waandishi wa habari kutokana na majonzi aliyokuwa nayo.

“Nimehuzunika mno kwa kitendo hiki, naiomba Serikali imsaidie kupata nyumba mimi naishi kijijini haitakuwa rahisi kuwa naye karibu, kitendo hiki kimeniumiza mno moyo wangu,” alisema.

Mke wa Mrisho aliyejitambulisha kwa jina la Stara Sudi, alisema majibu hayo ya madaktari yamempa majonzi kwa sababu hakuyatarajia kwa kuwa awali walielezwa kuwa inawezekana kupona.

“Sikutegemea majibu haya, naiomba Serikali isimwachie yule jamaa (Scorpion) wamfunge maisha yake yote kwa sababu wakimwachia ipo siku atakuja kurudia tena kitendo hiki kwa kuwafanyia wengine,” alisema.

Alisema hadi mumewe anakutwa na mkasa huo alikuwa akisimamia uendeshaji wa saluni moja iliyoko eneo la Tabata Sanene.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles