27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ugali wa muhogo waua mama, watoto wanne  

ugali-wa-muhogoEDITHA KARLO NA FLORIAN MASINDE-MULEBA

MAMA na watoto wake wanne wakazi wa Kijiji cha Nyamilanda, Kata ya Kyebitembe, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, wamefariki dunia jana baada ya kula ugali unaosadikiwa kuwa na sumu.

Kumekuwapo na taarifa za kukanganya juu ya tukio hilo, wakati nyingine zikidai kuwa unga uliotumiwa kupikia ugali huo ulitoka kwa mama mkwe wa mama huyo anayeishi jirani naye, nyingine zilidai kuwa alitengeneza mwenyewe na kabla ya kupika alikuwa ameuanika na kisha kuuchekecha.

Akizungumza na mmoja wa waandishi wa habari hizi ambaye alikuwepo eneo la tukio, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Damasen Kalori, aliitaja familia iliyofikwa na tukio hilo la kusikitisha kuwa ni ya mke mdogo wa Julius Gerald.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Yulitha Julias (35) ambaye ni mke wa Gerald na mama wa watoto; Aujen Julius (14) Siteus Julius (10) Gebora Julius (4), Pascal Julius (miezi mitano).

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata zinadai kuwa watu hao kabla ya kufikwa na mauti walikula ugali huo saa tisa mchana na mara moja wakaanza kutapika mfululizo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo watu hao walifariki wakati wakipelekwa Kituo cha Afya cha Kimeya kilichopo jirani na kijiji hicho.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinadai kuwa kabla ya kufikwa mauti hayo, mama huyo aliandaa mboga aina ya dagaa na kisha kuchekecha unga ambao alikuwa ameuanika kwa ajili ya kupika ugali.

Hata hivyo, taarifa nyingine zinadai kuwa baada ya kuandaa mboga alikwenda kwa mama mkwe wake nyumba jirani kwa ajili ya kuchukua unga wa muhogo ambao aliutumia kupika ugali huo.

“Walipoanza kula wakatapika na kuanza kuhangaika hatimaye wananchi wakafika lakini juhudi za kuokoa maisha yao hazikuzaa matunda, nilipofika nilikuta hali ni mbaya walikuwa wakitapika sana na tulitoa taarifa polisi lakini walipofika wakati wanawakimbiza hospitali ndogo ya Kimeya kwa bahati mbaya wakafariki,” alisema mmoja wa majirani.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kijijini hapo, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kyebitembe, Mohamed maarufu kama ‘Mabomu’, alisema baada ya kupata taarifa hizo alifika katika nyumba hiyo na kukusanya vielelezo vyote ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi kwa hofu ya kutokea vurugu.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Agustino Olomi, alikiri kupokea taarifa ya tukio hilo.

Olomi alisema hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo ambalo alisema tayari limefikishwa kwa wataalamu kwa ajili ya uchunguzi.

“Uchunguzi wa wataalamu wa afya unaendelea ili kujiridhisha na kutambua aina ya sumu iliyotumika hadi watu hao wakapoteza maisha yao.”

 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhandisi Richard Ruyango, alisema uchunguzi umeonyesha watu hao walikula chakula chenye sumu.

Kwa mujibu wa Runyango, hata hivyo sumu hiyo haikubainika kwa haraka hivyo sampuli imechukuliwa na kupelekwa ofisi ya Mkemia Mkuu Dar es Salaam.

Mkuu huyo wa wilaya amewataka wananchi katika Tarafa ya Kimwani kuwa makini na vyakula wanavyokula kwani hilo ni tukio la tatu la familia kula vyakula vyenye sumu na kupoteza maisha.

“Kitendo hiki kinasikitisha na si mafundisho ya Mungu licha ya waliofanya hivyo kuwa miongoni mwa waumini wa kiroho kwani wangetumia sheria kushtakiana kama hakuna usalama,” alisema Ruyango.

Ruyango alisema Jeshi la Polisi na kamati za ulinzi na usalama za kijiji na kata zimepewa jukumu la kufanya uchunguzi na kubaini waliohusika ili wachukuliwe hatua za kisheria kwani wametenda kosa kubwa la mauaji kinyume cha sheria.

Wakati mkuu huyo wa wilaya akisema hayo, taarifa kutoka eneo la tukio zinadai kuwa mke huyo mdogo kabla ya kufikwa na mauti hayo alikuwa na mgogoro na mke mwenzake kuhusiana na fedha ambazo zimekuwa zikitolewa na Tasaf katika kaya za watu masikini.

“Mke mdogo ndiye alikuwa ameandikishwa kuchukua fedha za Tasaf  na mgogoro ulianza pale mgawo wa kwanza ambapo mke mkubwa alilalamika kupata fedha kidogo, lakini baadaye mke mdogo aligundua kuwa mke mwenzake hahusiki katika mgawo huo hivyo fedha zilizofuata za mwezi wa tisa hakumpa,” alisema Mwenyekiti wa kijiji hicho, Damasen Kalori ambaye pia ni kaka wa marehemu.

Tukio kama hilo lilitokea mwaka jana Kata ya Kasharunga, Tarafa ya Kimwani Jimbo la Muleba Kusini ambapo watu wanne wa familia moja walifariki dunia baada ya kula chakula chenye sumu.

Katika tukio hilo watu watatu walisalimika baada ya kukimbizwa kituo cha afya na kupatiwa matibabu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles