24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 30, 2023

Contact us: [email protected]

Ajali yaua wawili, yajeruhi 10 Dar

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

WATU wawili wamefariki dunia na wengine 10 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea juzi usiku maeneo ya Kimara Bucha, Dar es Salaam baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupoteza mwelekeo na kutumbukia kwenye mtaro.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Christopher Fuime, alisema basi linalomilikiwa na Kampuni ya Leina Tours lililokuwa likitokea Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kwenda Dar es Salaam liliacha njia na kutumbukia kwenye mtaro.

“Dereva alipofika maeneo ya Kimara alihama njia na kutumia barabara ya mabasi yaendayo kasi na kusababisha kukutana uso kwa uso na gari ndogo aina ya Rav4 ndipo ilipomlazimu dereva kuhamia barabara ya mabasi yanayotoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na kutumbukia kwenye mtaro,” alisema Fuime.

Wakati huo huo, Meneja Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminieli Eligaesha, alisema walipokea miili miwili ya watu ambao hawajafahamika majina yao hadi sasa na majeruhi 10 ambao kati yao watatu waliruhusiwa baada ya afya zao kutengamaa.

Alisema majeruhi watano walihamishiwa Kitengo cha Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) kutokana na hali zao kuwa mbaya.

Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Shija Sando (47), Rodiana Alex, Sadik Maungwa (44), Siwema Alex (20), Salum Hussein (17), Steven Mashija (4), Aloyce Mpyalemi (47), Michael Fabiam (25), Saidi Mussa (27) na Deograus Mgomba (35).

Salum Hussein ambaye ni miongoni mwa marejuhi hao, aliomba ndugu zake popote walipo wafike Muhimbili.

“Nilikuwa natokea Singida nakuja Dar es Salaam na sijawahi kufika katika mkoa huu, dada yangu ambaye alitakiwa aje kunipokea anaitwa Salma Ramadhani na baada ya ajali kutokea nilipoteza mawasiliano yake na sijui anakaa wapi,” alisema Hussein.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,285FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles