24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Profesa Baregu: Ni utawala wa kijeshi

bareguNA ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kuteua wakuu wa mikoa wapya, mtaalamu wa sayansi ya siasa, Profesa Mwesiga Baregu, ameibuka na kusema kuwa kuwapo kwa wanajeshi wengi wastaafu katika uteuzi huo inadhihirisha wazi kuna dalili za utawala wa kijeshi nchini.

Mbali na Profesa Baregu, baadhi ya wachambuzi na wanasiasa nao wamekosoa uteuzi huo.

Akizungumza na MTANZANIA kupitia simu yake ya kiganjani jana, Profesa Baregu alisema kwa kawaida wanajeshi huwa hawana hulka ya kidemokrasia.

“Kitu kimoja kinachojitokeza kwenye uteuzi huu ni kuwepo kwa wanajeshi wastaafu, na mimi ninavyoelewa wanajeshi huwa hawana hulka za kidemokrasia. Hii inaonyesha wazi kwamba utawala huu ni wa kijeshi,” alisema.

Profesa Baregu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema haileti picha nzuri kuwapo kwa wanajeshi wengi katika utawala kwa sababu tawala za mikoa na wilaya ni saula la kiraia na demokrasia zaidi.

Alisema rasimu ya katiba ambayo yeye alikuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ilipendekeza kupitia upya tawala za mikoa na kupunguza idadi yake.

“Kutokana na hilo, mamlaka ya wananchi inamezwa kwa sababu wakuu wa mikoa na wilaya ni wengi na kunakuwepo na mgongano mkubwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ali, alisema uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya ni wa rais na wanaoteuliwa ni watu mchanganyiko.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Ruco), Profesa Gaudence Mpangala, alisema kila anapoingia kiongozi mpya anaunda timu ambayo anaona ataendana nayo.

 

JUVICUF

Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Wananchi (JUVICUF), imekosoa uteuzi huo na kudai kuwa ni mkakati wa CCM kuwatumia wakuu hao wa mikoa kuvuruga wapinzani.

Katika taarifa yao iliyosainiwa na Mwenyekiti wa JUVICUF, Hamidu Hassan Bobali, walitolea mfano uteuzi wa aliyewahi kuwa Katibu wa Jumuiya ya Vijana CCM (UVCCM), Martin Shigela pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kuwa wamepelekwa maeneo yanayoongozwa na upinzani (halmashauri) ili kuwadhibiti.

“Paul Makonda ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kapewa ukuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni zawadi ili atumie kivuli cha Serikali kupambana na wapinzani ambao ndio wataunda halmashauri ya jiji hilo,” alisema.

Juzi, Rais Magufuli alifanya uteuzi wa wakuu wa mikoa, huku majenerali wanne wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) akiwapangia kazi katika mikoa ya mipakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles