Agizo la Lugola lamtia mbaroni mchungaji

0
698

LEONARD MANG’OHA – DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ameagiza kukamatwa kwa Mchungaji wa Kanisa la Pentecostal Power Ministries la Dar es Salaam, Elia Mahela, kwa kukaidi maagizo ya Serikali ya kuzuia kutopiga muziki na kufanya mahubiri yanayosababisha kelele na kero kwa wananchi.

Waziri Lugola alitoa agizo hilo Dar es Salaam jana mchana wakati wa ziara ya kutatua kero zitokanazo na kelele zinazosababishwa na nyumba za starehe, baa na ibada katika eneo la Mbezi Temboni wilayani Ubungo.

Kutokana na agizo hilo, mchungaji huyo alikamatwa na polisi walioongozana na waziri huyo katika ziara hiyo wakiongozwa na Mpelelezi Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kipolisi Kimara (OCSID), Chassa Magai na kwenda naye kituoni kwa hatua zaidi za kisheria.

“Kwa sababu huyu amekaidi muda mrefu, mumkamate alafu akashtakiwe ili iwe fundisho kwa wakaidi kama hawa, na huyu ambaye amesema ndiye mmiliki wa haya makanisa ajisalimishe katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kipolisi Kimara.

“Yeye mwenyewe ajisalimishe kwa OCD aje atoe maelezo na ninyi ma-OCD wote nchi nzima nimeelekeza tumieni kifungu cha 42 cha sheria yetu ya Jeshi la Polisi na polisi wasaidizi sura ya 322,” alisema Lugola.

Awali asubuhi akiwa katika eneo la Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni kushughulikia mgogoro wa baa ya Bus La Vida inayolalamikiwa na wananchi wa eneo hilo kusababisha kelele kutokana na kupiga muziki kwa sauti kubwa wakati wa usiku, Lugola aliapa kula sahani moja na wakuu wa polisi wa wilaya (OCDs) katika wilaya zote nchini watakaoshindwa kuwadhibiti wamiliki wa sehemu hizo.

Awali Lugola alisema haiwezekani wananchi wakiwamo wagonjwa na wazee washindwe kupumzika katika mazingira tulivu kutokana na kelele hizo ambazo sheria imeelekeza wazi namna ya kudhibitiwa.

“Sasa ije itokee leo hii niambiwe na mwananchi yeyote kwenye kona hii ya Tanzania kwamba kuna mahala hapa yako makelele tunayolalamika hayajamwelewa Rais Magufuli, kwenye simu hii huyo OCD huyo ama zake ama zangu naomba nirudie, kuna wanaodhani ni mchezo kwenye simu hii kwenye hiki kilio cha Watanzania cha muda mrefu.

“Mwananchi anipigie simu kwamba bado wapo ambao wanatingisha tingisha kiberiti cha JPM (Rais Magufuli) wanadhani hakijajaa, huyo OCD nimesema ama zake ama zangu, na huko kuna makamanda wa mikoa, ” alisema Lugola.

Akizungumza na wananchi katika eneo hilo, mwananke mmoja anayedaiwa kuwa mmiliki wa baa hiyo, muda mfupi baada ya kumweleza waziri kuhusu mgogoro huo alianguka na kuzua taharuki miongoni mwa watu waliohudhuria tukio hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here