32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge lataka hifadhi ya Nyerere iwe na mamlaka yake

ANDREW MSECHU – DODOMA

BUNGE limepitisha azimio kurudhia upandishaji hadhi wa sehemu ya Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Nyerere, wakipendekeza iundwe mamlaka maalumu inayosimamia uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori katika hifadhi hiyo.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii jana, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Kemilembe Lwota (CCM),  alisema kamati hiyo imeridhia kubadilishwa hadhi kwa hifadhi hiyo ya Selous, lakini kwa kuzingatia pia gharama za utunzaji wake.

Alisema ili kulipa uzito eneo hilo la Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, ni vyema eneo lote la pori la Akiba la Selous na maeneo jirani ya Pori Tengefu la Kilombero na Bwawa la Kufua Umeme Maji la Nyerere  yote yajumuishwe katika hifadhi hiyo na iwe mamlaka kama ilivyo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Lwota alisema faida ya uamuzi huo ni kuipa Serikali wigo mpana wa kupanga matumizi ya ardhi ikiwemo utalii wa picha, uwindaji wa kitalii, uvuvi wa kitalii ambavyo kwa pamoja vitachangia kukuza pato la taifa.

“Utaratibu huu wa kuliweka eneo hili chini ya mamlaka moja utaepusha mgongano wa menejimenti kwani eneo lote litasimamiwa na menejimenti moja tofauti na pendekezo la sasa la Serikali ambapo eneo hilo linakuwa chini ya mamlaka mbili, yaani kilometa za mraba 30,893 sawa na asilimia 62 zinakuwa chini ya Tanapa na sehemu inayobakia yenye kilometa za mraba 18,971 sawa na asilimia 38 zinakuwa chini ya Tawa.

“Aidha bwawa la kufua umeme la Rufiji nalo linasimamiwa na taasisi mbili, yaani sehemu moja ya bwawa hilo itakuwa chini ya Tawa na sehemu nyingine itakuwa chini ya Tanapa,” alisema.

Alisema kuanzishwa kwa Hifadhi mpya ya Taifa ya Nyerere kutalifanya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kuwa na hifadhi 20, hivyo kuwa na mzigo mkubwa ikilinganishwa na uwezo wake wa kuzihudumia.

“Kutokana na hatua ya hivi karibuni kwa Serikali kupandisha hadhi mapori ya akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika na kuanzisha hifadhi za taifa tatu za Burigi-Chato, Ibanda-Kyerwa na Rumanyika-Karagwe, tayari Tanapa inasimamia jumla ya hifadhi 19.

“Kati ya hizo ni hifadhi tatu tu, yaani Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro ndizo zinazozalisha ziada kwa ajili ya kujiendesha na kusaidia hifadhi nyingine 14 ambazo ni tegemezi,” alisema.

Awali, akiwasilisha azimio hilo ambalo lilipitiwa na wabunge kisha kupitishwa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala alisema hatua ya kuridhia azimio hilo italinufaisha taifa kwa kuimarisha uhifadhi wa maliasili, hasa wanyamapori, mimea, mazalia na makuzio ya samaki na viumbe wengine kwenye maji.

Alisema pia itasaidia kuongeza pato la taifa kwa msingi kuwa ubadilishaji hadhi huo wa sehemu ya pori hilo utasababisha hifadhi hiyo kuwa kivutio cha utalii.

Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa,  alisema kambi ya upinzani haina mgogoro wala haipingi dhamira njema ya Serikali ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa kutumia jina lake katika vitu vyenye wasifu wa kitaifa, kama hifadhi hiyo mpya inayoanzishwa.

“Hata hivyo, kwa muktadha wa pori la Akiba la Selous, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona ingekuwa na mantiki zaidi kubadili hadhi ya pori hilo kwa ujumla wake na siyo kukata vipande,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles