29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

AG MASAJU: Nitaanza na mikataba ya gesi

DSC_2303NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, amesema anataka muda zaidi ili aweze kuzungumzia suala la Kampuni ya Kufua Umeme Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na mikataba ya gesi ambayo imekuwa ikitakiwa kuwekwa wazi.
Masaju aliyasema hayo jana, Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete kuchukua nafasi ya Jaji Frederick Werema, aliyejiuzulu nafasi hiyo kutokana na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Baada ya Masaju kuapishwa, wanahabari walitaka kujua maoni yake juu ya suala hilo la IPTL lililozaa kashfa ya akaunti hiyo ya Tegeta Escrow na lile la usiri wa mikataba ya gesi.
“Nipeni muda zaidi kuzungumzia masuala hayo ya IPTL na mikataba ya gesi kwa sababu inahitaji muda zaidi wa kuipitia. Pia kwa sasa tupo Ikulu kwa rais, hivyo siwezi kuzungumzia jambo hilo, ningependa mnitafute ofisini, baada ya kupitia taarifa mbalimbali nitakuwa na majibu mazuri,” alisema.
Alisema ugumu wa suala la mikataba ya gesi unatokana na mikataba hiyo kugawanyika katika sehemu mbili, moja ikiwa ni ile ya siri na nyingine ya wazi.
“Kinachotakiwa ni kuisoma mikataba hiyo na baada ya muda naamini nitakuwa na jibu la uhakika la kuwapa, kinachotakiwa ni uvumilivu kama nilivyosema hapo awali,” alisema.
Masaju alitoa wito kwa wananchi kurudisha imani kwa Serikali ili kumwezesha kuwatumikia ikiwamo na kusaidia shughuli za uchumi kuendelea.
“Nashukuru mamlaka iliyoniteua na wananchi kwa kuniamini kuwa mtumishi wao kutokana na kuonyesha kuthamini mchango nilioutoa wakati nikiwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alisema Masaju.
Uteuzi wa Masaju ulifanyika Januari 2, 2015 ambapo kabla ya uteuzi wake alipata pia kushika wadhifa wa Mshauri wa Sheria wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwishoni mwa mwaka jana, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), iliamuru kutiwa mbaroni kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Michael Mwande na Kaimu Mkurugenzi wa shirika hilo, James Andilile kutokana na kukiuka amri ya kamati hiyo iliyotaka kukabidhiwa mikataba 26 ya gesi kwa takribani miaka mitatu bila mafanikio.
Vigogo hao walikamatwa kwenye ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, walipokutana na kamati hiyo ambayo ilikuwa imekaa kama mahakama.
Hatua hiyo ilichukuliwa chini ya Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, Makamu wake Deo Filikunjombe na Mwanasheria wa Bunge, Nenelwa Mwinambi.
Mwinambi alianza kwa kuwaapisha viongozi hao wa TPDC kabla kuanza kuwasomea vifungu vya sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge.
Baadhi ya vifungu walivyosemewa ni pamoja na vile vinavyolipa Bunge ama Kamati ya Bunge haki ya kupata taarifa kutoka kwa taasisi yoyote ya sheria.
Mwinambi alisema kwa nyakati tofauti tangu mwaka 2012 kamati hiyo imekuwa ikiomba kupewa miaka 26 ya gesi jambo ambalo halijawahi kutekelezwa.
Alisema nyaraka ambazo haziruhisiwi kutolewa ni zile zinazohusu mambo ya jeshi na usalama pekee.
“Kamati imekuwa ikiomba mikataba 26 ya gesi na mapitio yake kwa kipindi chote hiki (tangu 2012) hawajawahi kusema kama inahusiana na masuala ya kijeshi ama usalama,” alisema Mwinambi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles