27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

ADHABU ISIWE SEHEMU YA KUMDHALILISHA MTOTO

NA AZIZA MASOUD,

HATUA za makuzi anazozipitia mtoto na changamoto zake ni wazi kuwa yapo makosa ambayo anayafanya na kuhitaji kukanywa, pia vipo vitu ambavyo anapaswa kuelekezwa.

 Mtoto anapokosea mzazi unapaswa   kutumia njia sahihi ya kumwelewesha na si kumtolea maneno machafu ama kumkanya mbele za watu, si sawa na huwezi kumsaidia.

Mara nyingi wazazi wanawaadhibu watoto mbele ya wenzao, jambo hilo si zuri pia linaweza likaonekana kama sehemu ya udhalilishaji.

Unapofanya hivyo kama mzazi unapaswa kutambua kuwa mtoto anakosa ujasiri mbele ya wenzake.

Unapomsema mtoto mbele za watu ni wazi kuwa anajisikia vibaya kwakuwa pamoja na yeye kuwa na umri mdogo lakini bado ni binadamu hivyo anahitaji kuelekezwa kwa utaratibu.

Kuwaaibisha watoto mbele ya wengine si sawa, hata kama mtoto ni mdogo ni vyema kumchukua na kumpeleka mahali pa faragha na kumweleza kosa.

Kabla ya kumwadhibu unapaswa kumpa nafasi ya kujitetea na endapo utagundua amekosea unapaswa kumwadhibu si mbele za watu.

Wazazi lazima tukumbuke kuwa watoto nao ni watu kamili walio na hisia, utashi, aibu nk, muhimu ni kuwaheshimu.

Mbali na hilo adhabu kali kupita kiasi, wazazi ni lazima wapime adhabu wanazotoa kwa watoto wao kulingana na kosa, jinsia, umri na mazingira pia.

Vile vile adhabu isitolewe kwa hasira, vinginevyo mtoto hataelewa kosa na anaweza akarudia kama hakuelewa.

Wapo ambao hawapendi kuwapa adhabu watoto wao hivyo anaamua kumkemea bila kuchukua hatua yoyote, mara nyingi utasikia kwa mama au baba akimwambia mtoto kwa mfano, “acha, nitakupiga wewe.” Mtoto anaendelea tu kufanya anachofanya na mzazi wala hamchapi.

Hali hii inamjengea mtoto kuona kuwa mzazi ana tabia ya kusema au kufoka tu, bila kuchukua hatua yoyote.

Kufanya hivyo ni mbaya sana kwa mtoto, kwanza unamtengenezea mazingira ya kuwa na kiburi, kutokuwa msikivu wala mtiifu kwa watu waliomzidi.

Ni vizuri mzazi akimwambia mtoto “acha” au “njoo” au “nenda” na mtoto asipotii kufanya unatakiwa umsaidie  kutekeleza aliloambiwa ili aumbike tabia ya kutii.

Jenga utaratibu mzuri wa kuongea na mtoto uweze kumjenga kuwa mtu mwenye tabia nzuri na heshima kwa wakubwa na watoto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles