27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

KENYA ISILAUMU IMEVUNA ILICHOPANDA

NA MARKUS MPANGALA,

TANGU kutangazwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), kumeibuka mjadala mkali juu ya kushindwa kwa mgombea aliyetoka katika ukanda wa Afrika Mashariki, Balozi Amina Mohammed.

Ndiyo kusema wakati Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Idris Deby, Rais wa Chad akimaliza muda wake, nchi hiyo imefanikiwa kupiga hatua nyingine kwa mgombea wake kuibuka mshindi wa kumrithi Dk. Nkosazana Dlamini-Zuma ambaye hakugombea tena nafasi hiyo aliyodumu kwa miaka mitano.

Balozi Amina ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, alikuwa akiwania nafasi hiyo pamoja na Moussa Faki Mahamat (Chad), Dk. Pelonomi Venson-Moitoi (Botswana), Agapito Mba Mokuy (Guinea ya Ikweta) na Profesa Abdoulaye Bathily (Senegal). Katika uchaguzi huo mshindi ni Moussa Faki Mahamat raia wa Chad aliyepata kura 38.

Mjadala huo umekuwa kwenye makundi makuu mawili; kundi la kwanza linaloongozwa na watu wanaoamini kuwa Kenya imefanyiwa usaliti kwa madai kuwa Tanzania na Uganda ilimtosa Balozi Amina.

Kundi la pili ni lile linaloongozwa na watu wanaomini kuwa Balozi Amina hakuwa na sifa ya kushika wadhifa huo. Miongoni mwao ni mwanasiasa mashuhuri, Nazlin Umar wa Kenya.

Mwanasiasa huyo amekuwa gumzo kutokana na kumpinga Balozi Amina na kulalamikia hatua ya nchi yake kutumia kiasi kikubwa cha fedha kumpigia kampeni mwanamama huyo.

Katika mtandao mmoja wa kijamii, Wakenya takribani 65 wamepongezana huku wakidai kuwa kushindwa kwa Balozi Amina ni hatua nzuri na ujumbe kwa Serikali ya Jubilee inayoongozwa na Uhuru Kenyatta.

Kwanini Balozi Amina alitoswa?

Awali, Serikali ya Uganda ilimwondoa mgombea wake, Dk. Specioza Wandira Kazibwe kutoka Uganda na kwamba Serikali ya Uganda ilisema itamuunga mkono Balozi Amina.

Aidha, Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo ilikubali kwa kauli moja kumuunga mkono Dk. Pelonomi Venson-Moitoi (Botswana), lakini taarifa za baadaye kupitia Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Augustine Mahiga, alisema wangemuunga mkono Balozi Amina kutoka EAC.

Mosi, nafasi finyu kwa mwanamke Tunafahamu kuwa nafasi hiyo imetoka kwa mwanamke (Dk. Dlamini) sidhani kama ‘kisaikolojia’ Umoja wa Afrika walikuwa wanataka tena kiongozi mwanamke. Hilo pekee lilikuwa kikwazo kabla ya kuilaumu Tanzania na Uganda kama nchi zilizoongoza kumkataa mwanamama huyo.

Pili, ajenda ya Kenya ni moja tu, ICC Hapakuwa na mtazamo wowote mpana juu ya kuijenga Tume ya Umoja wa Afrika. Suala la kung’oka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita (ICC), linatukumbusha mwaka 2014 ambapo waliingiza ajenda hiyo kuungwa mkono.

Safari hii walitaka nafasi hiyo kuongeza ushawishi, licha ya nchi wanachama wa AU kwa kauli moja kuunga mkono mpango wa kujiondoa katika Mahakama ya ICC ambayo mataifa mengi ya Afrika yanahisi inawalenga viongozi wa Bara la Afrika pekee.

Nje ya ICC, Kenya haikuwa na ajenda nyingine wala mkakati wenye masilahi kwa Afrika zaidi ya kujenga taswira ya diplomasia yao kimataifa.

Tatu, Kenya imejikosesha ushindi

Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake, William Ruto, walifanya kampeni kubwa katika nchi 54 za Afrika kutafuta uungwaji mkono, inadaiwa kuwa walitumia takribani Sh bilioni 4 ya Kenya.

Rais Uhuru aliahidi kuisafisha nyota ya Kenya huku akisahau kuwa makamu mkuu wa tume hiyo alikuwa Mkenya, Erastus Mwencha, ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Comesa (Common Market for Eastern and Southern Africa).

Mwencha ni mzoefu katika siasa na uongozi wa Kiafrika. Uzoefu wake ulikuwa na faida zaidi kuliko mgombea mpya aliyeletwa (Balozi Amina).

Kenya walitakiwa kujifunza kwa Chad, Faki anafahamika uwezo wake na wakuu mbalimbali wa Afrika kutokana na kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Uchumi, Jamii na Utamaduni la AU.

Nne, nafasi ya ukanda na kambi hesabu zinamnyika ushindi

Balozi Amina anatoka Kenya iliyopo ukanda wa Afrika Mashariki. Kukosa kura za Tanzania, Burundi na Uganda ina maana alibakiwa na kura za Rwanda na Sudan Kusini.

Katika nchi zinazozungumza Kifaransa (Francophone) zipo 20 ambazo zinaweza kuamua mshindi wao. Nchi hizo ni Mali, Senegal, Guinea, Ivory Coast, Burkina Faso, Benin, Togo, Gabon, Cameroon, DRC, Jamhuri ya Kati, Shelisheli, Comoro, Djibouti, Madagascar, Niger, Chad, Rwanda, Burundi na Congo-Brazzaville.

Tayari Senegal na Chad walikuwa na wagombea wao, kwa vyovyote wasingeichagua Kenya. Kwenye taswira ya ukanda, Senegal na Chad wasingeipigia kura Kenya na wala wenzake (Ecowas) wasingefanya hivyo.

Kundi la nchi zinazozungumza Kiingereza yaani Anglophone zipo 12, Gambia, Liberia, Ghana, Nigeria, Sierra Leone, Sudan Kusini, Namibia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Zambia, Botswana, Lesotho na Malawi. Kusini mwa Afrika kuna Afrika Kusini, Zambia, Botswana, Lesotho, Malawi, Swaziland na Zimbabwe

Katika idadi hiyo tukizitoa nchi tano (Gambia, Sierra Leone, Nigeria, Ghana, Liberia) zinabaki 7. Si rahisi kwa nchi 5 hizo kumpa kura mgombea wa Kenya na kuwaacha wagombea wa ukanda wao wa Afrika Magharibi. 

Nchi 7 zinazobaki hapo juu ni wanachama wa SADC ambao walikubaliana kwa kauli moja kumchagua mgombea wao (kutoka Botswana). Isingekuwa rahisi Kenya kuzipata kura zao. Kihesabu upo uwezekano Kenya ilikosa kura 14 katika kundi hili pamoja na nyingine 20 (Francophone) za kundi la awali ili kufikisha theluthi moja yaani kura 36 kumpata mshindi. Ukijumlisha utaona Kenya inakosa kura 34.

Mfano mwingine ni nchi zinazozungumza Kiarabu (Arabphone); Misri, Libya, Sudan, Morocco, Algeria, Tunisia, Mauritania na Chad. Tayari Chad imo kwenye makundi mawili; Arabphone na Francophone kitu ambacho kiliipatia faida nyingine kuliko Kenya. Ingewezekana vipi Chad kunyimwa kura na Mauritania? Palibaki kura 5 tu hapa za kunyang’anyana, kwa kuwa Morocco hakuwa mwanachama.

Kundi la mwisho ni nchi zinazozungumza Kireno (Lusophone); Cape Verde, Guinea Bissau, Sao Tome and Principe, Angola na Msumbiji. Mataifa ya Angola na Msumbiji ni wanachama wa SADC, hivyo uwezekano wa Kenya kuzikosa kura zao ulikuwa mkubwa mno.

Chukulia mfano, kundi la Arabphone, Chad ilikuwa na uhakika wa kura ya Mauritania na Francophone, sidhani nchi za Afrika Magharibi zingekubali kushindwa kirahisi kulingana na wingi wao.

Akizungumzia sakata hilo, Ofisa wa zamani wa Umoja wa Afrika, Marubu Munyaka, alisema: “Nimefanya kazi Umoja wa Afrika kati ya mwaka 2003 hadi 2004. Unatakiwa kukubaliana na siasa za ukanda kwenye bara hili. Jumuiya ya Afrika Mashariki katika uchaguzi uliopita kwenye nafasi ya Msaidizi wa Mkuu wa Tume ya Umoja huo ni Erastus Mwencha ambaye ni raia mwenzetu wa Kenya. Amekuwa msaidizi tangu Dk. Dlamini Nkosazana-Zuma, achukue madaraka ya Ukuu wa Tume hiyo.

“Kiukweli lilikuwa kosa kwenda kwenye uchaguzi huo kuomba nafasi ya Ukuu wa Tume. Mazingira halisi yanaonyesha nafasi ilitakiwa iende kanda nyingine. Wakati Nigeria ikitangaza kuwa haitajitoa uanachama wake kwenye Mahakama ya ICC, ulikuwa ujumbe wa dhihiri kuwa haimpigii kura mgombea wa Kenya (Balozi Amina).”

Mgawanyo wa kura uliinyima ushindi Kenya kwa kuwa haikuwa na uhakika wa kura za wanachama wa SADC ambao walikuwa na mgombea wao, halafu Senegal na Guinea Ikweta walikuwa na mgombea wao, Kenya isingepata kura zao.

Tuhesabu, Kenya ilipoteza kura EAC (3), Guinea ya Ikweta (1), SADC (7), Ecowas (20) Lusophone (2) kwa kuwa kura 5 zilikuwa za Gambia, Liberia, Ghana, Nigeria na Sierra Leone.

Tano, pembe ya Afrika uhusiano kati ya Kenya na Somalia ni mbaya

Uhusiano kati ya Kenya na Djibouti ni mbaya. Mataifa hayo mawili tayari Kenya ilikosa kura 2 hapa kati ya 36 zilizohitajika. Ikumbukwe Somalia imefungua kesi juu ya mipaka yake na Kenya, hivyo tayari uhusiano wao ulikuwa na doa.

Kwa mantiki hiyo huwezi kuilaumu Tanzania, Burundi na Uganda kwa kushindwa Balozi Amina Mohammed. Nchi pekee ambazo zingetegemewa ni Ethiopia na Eritrea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles