24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

ABDALLAH MAULID: SOKA LA ZANZIBAR LIMEPOROMOKA

UNAPOZUNGUMZIA mabeki wa zamani wa timu ya KMKM ya Zanzibar waliotamba na kuvuma wakiwa na timu hiyo, kamwe huwezi kuacha kulitaja jina la Abdallah Maulid ambaye alichezea kwa mafanikio makubwa kwa kipindi cha takriban miaka 11 kuanzia 1975 hadi 1985.

Nyota huyo pamoja na kuichezea klabu hiyo, pia ameichezea timu ya Miembeni kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 1986 hadi 1990 na timu ya Taifa ya Zanzibar kwa kipindi cha miaka miaka mitano kuanzia 1977 hadi 1981.

Maulidi ambaye alikuwa akicheza beki wa kulia alisifika kutokana na aina ya uchezaji wake, kwani alikuwa makini mno, anayetumia akili na nguvu pale inapohitajika hali iliyowafaya washambuliaji aliokuwa akikabiliana nao kupata wakati mgumu kumpita.

Hivi karibuni SPOTI KIKI lilimtafuta mkongwe huyo ambaye hivi sasa ni kocha  wa timu ya Tanzania All Stars ‘Maveteran’ na kufanya naye mahojiano kuhusiana na masuala ya soka ambapo anazungumzia kuporomoka kiwango cha soka Zanzibar.

Katika mahojiano hayo Maulid anasema kuwa hivi sasa Zanzibar haina viongozi mahiri wa kuendeleza mchezo huu wa soka na waliopo hawataki ushauri kutoka kwa wachezaji wa zamani ambao wameifanyia makubwa nchi hiyo toka enzi ya ‘Gossage Cup’ (sasa Kombe la Chalenji).

“Miaka ya 1960 timu ya Taifa ya Zanzibar ilikuwa inatoa upinzani mkubwa kwa timu ya Taifa ya Uganda ‘The Uganda Cranes’ ambao ni vinara katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki.

“Nakumbuka mwaka 1966 timu ya Taifa ya Zanzibar katika michuano ya Gossage Cup, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung ilitoka sare ya bila kufungana 0-0 na ‘The Uganda Cranes’, ambapo mwaka huo timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ ndiyo iliyotwaa taji hilo.

“Mwaka 1977 kizazi kilichofuata timu ya Navy (sasa KMKM), katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, iliyofanyika mjini Tanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani, iliifunga timu KCC ya Uganda bao 1-0.

“Pia mwaka uliofuata 1978 KMKM katika michuano ya Kombe la Washindi Barani Afrika (sasa Kombe la Shirikisho), iliifunga timu ya Jeshi la Uganda mabao 2-0 wakati wa enzi ya utawala wa Rais Idd Amin.

“Mwaka 1994 timu ya Malindi ya Zanzibar katika michuano ya Kombe la Hedex, iliyofanyika kwenye Uwanja wa Manispaa mjini Mombasa, Kenya, iliifunga timu ya KCC ya Uganda mabao 2-0.

“Hali kadhalika mwaka uliofuata 1995 timu ya Taifa ya Zanzibar ilitwaa Kombe la Chalenji baada ya kuifunga katika fainali ‘The Uganda Cranes’ bao 1-0, michuano iliyofanyika kwenye Uwanja wa Nakivubo, mjini Kampala, Uganda.

“Mafanikio ya mwisho yalifanyika mwaka 2003 wakati timu ya Taifa ya Vijana Zanzibar ilipoifunga timu ya Taifa ya Uganda bao 5-4 yaliyopatikana kwa mikwaju ya penalti, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Aman mjini Zanzibar.

 

“Hivyo historia hii inaonesha dhairi kuwa kiwango cha soka la Zanzibar miaka hiyo ya nyuma kilikuwa juu kutokana na kutoa upinzani mkubwa na kuwafunga Waganda ambao katika viwango vya Ubora wa Soka Duniani FIFA ‘ranking’ wako juu kulinganisha na Tanzania.

“Kuanzia mwaka 2003 mpaka leo hii 2017 soka la Zanzibar limeporomoka, hivyo tunahitaji mabadiliko ya uongozi bora, watu wenye uwezo wa kuongoza mchezo huu wa soka kusudi maendeleo yawe kama miaka ya nyuma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles