27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

NI MAKOSA KUMLAUMU NEYMAR KUONDOKA

NA BADI MCHOMOLO

IDADI kubwa ya mashabiki wa klabu ya Barcelona wamechukizwa sana na kitendo cha mshambuliaji wao hatari, Neymar de Santos, kuondoka katika kikosi chao ikiwa msimu uliopita aliongeza mkataba wa miaka mitano kuitumikia klabu hiyo.

Wengi wao waliamini kuwa mchezaji huyo ataendelea kuwa kwenye timu yao kwa kipindi chote hicho, lakini wamesahau kwamba mchezaji huyo alisajiliwa ili awafanyie biashara, lakini na yeye alikuwa anafanya biashara ili kuendesha maisha yake.

Kwa upande wake katika kipindi cha miaka minne aliyokaa ndani ya Camp Nou, aliweza kuwafanyia biashara kubwa zaidi ya ile fedha waliyomsajili kutoka klabu ya Santos, hivyo kazi yake ilibaki ni kujitengenezea mazingira mazuri ya maisha yake ya baadaye.

Aliweza kuitumia vizuri akili yake katika kuwashawishi mashabiki na wadau wa soka duniani kuwa yeye ni miongoni mwa wachezaji ambao wanaweza kuwa wafalme wa soka.

Wachezaji wengi kutoka Amerika Kusini wanadaiwa kutokea kwenye maisha ya chini, hivyo wanaamini soka ni sehemu mojawapo ya kuondoa umasikini wao, wanapambana sana kuhakikisha hilo linakaa sawa.

Wakiwa wanapambana ili kuondoa umasikini wanajikuta wakicheza soka la kiwango cha hali ya juu na majina yao kutawala ulimwengu. Nchini Brazil, kumetoa wachezaji wengi wenye vipaji vya hali ya juu na kutwaa tuzo ya mchezaji bora duniani, Ballon d’Or.

Baadhi ya wachezaji walioweka historia nchini humo ni pamoja na Romario Faria, alishinda taji la mchezaji bora dunia 1994, Ronaldo de Lima, akichukua mara tatu, 1996, 1997 na 2002. Rivaldo alichukua 1999, Ronaldinho Gaucho 2004 na 2005 na Kaka akichukua 2007.

Kaka ni mchezaji wa mwisho kutoka Brazil kuchukua tuzo hiyo kabla ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kutawala tangu 2008.

Neymar ametokea kwenye kizazi kigumu cha kutwaa tuzo hiyo kwa sasa kutokana na wafalme aliowakuta Messi na Ronaldo, anahitaji zaidi ya miaka miwili mbele kupata nafasi ya kutwaa tuzo hiyo.

Neymar alikuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi cha Barcelona, lakini kwa kuwa alimkuta mfalme wa klabu hiyo Messi akiwa kwenye ubora wake ilikuwa ngumu kwa wafalme wawili kufanya kitu kimoja kinachofanana.

Hata kama Neymar akifanya makubwa lakini Messi anaonekana zaidi, hivyo Messi hakuwa na kazi kubwa sana ya kupigania nafasi yake kwa kuwa mji wa Catalunya wanaamini hakuna zaidi ya yeye.

Maamuzi ya Neymar kuondoka ni sahihi, kwanza ni kutokana na kiasi cha fedha alichowekewa na PSG, pili ni kutafuta ufalme sehemu nyingine kwa kuwa Barcelona ilikuwa ngumu kumuangusha Messi.

Si tu kwa Barcelona, hata kama Neymar angekuwa anacheza soka kwenye klabu ya Real Madrid, ingekuwa ngumu kuuvua ufalme wa Ronaldo, amefanya maamuzi sahihi ya kwenda kuutengeneza ufalme wake ndani ya PSG.

Kila kona kwa sasa Jiji la Paris hasa kwa mashabiki wa PSG, jina linalozungumzwa ndani ya midomo yao ni Neymar, tayari mchezaji huyo ameanza kuutengeneza ufalme wake, kama ameshindwa kutwaa Ballon d’Or tangu amejiunga na Barcelona, basi mwacheni atengeneze historia ya kusajiliwa kwa bei kubwa kuliko mchezaji yeyote duniani, kwa pauni milioni 198, zaidi ya bilioni 500 za Kitanzania.

Hii tayari ni aina yake ya historia mbali na Ballon d’Or, japokuwa kutwaa tuzo kama hiyo ni sehemu ya mafanikio makubwa katika soka duniani. Neymar anajua kwanini amejiunga na PSG, alikuwa anajua aina ya ligi hiyo, haina idadi kubwa ya mashabiki kama ilivyo Hispania na England, lakini kujiunga kwake kunaongeza idadi kubwa ya mashabiki hasa kutoka nchini Brazil.

Hakuna mchezaji dunia hii ambaye angeweza kukataa kujiunga na PSG kwa kiasi cha fedha ya usajili na mshahara aliowekewa Neymar wa pauni 500,000 kwa wiki, zaidi ya bilioni 1 na milioni 443 kwa mwezi, huku kwa mwaka akichukua pauni milioni 26 zaidi ya bilioni 75.

Kiasi hicho cha fedha ni kwamba, Neymar anachukua 206,201,000 kwa siku, huku kwa saa anachukua 8,591,220, wakati huo kila dakika anachukua 144,342.

Kwa sasa Neymar amekuwa mchezaji wa pili duniani ambaye analipwa kiasi kikubwa cha fedha, huku nyota wa zamani wa klabu ya Juventus na timu ya Taifa ya Argentina, Carlos Tevez, anayekipiga katika klabu ya Shanghai Shenhua ya nchini China, akichukua pauni 650,000 kwa wiki, zaidi ya bilioni 1 na milioni 876, wakati huo kwa mwaka akichukua pauni milioni 34, zaidi ya bilioni 98.

Nafasi ya tatu inashikwa na Ezequiel Lavezzi, anayekipiga katika klabu ya Hebei China Fortune nchini China, analipwa bilioni 1 na milioni 327 kwa wiki, huku kwa mwaka akichukua bilioni 69.

Kiungo wa zamani wa Chelsea, Oscar de Santos, anachukua bilioni 1 na milioni 248 kwa wiki katika klabu ya Shanghai SIPG, sawa na Lionel Messi, huku Cristiano Ronaldo akichukua bilioni 1 na zaidi ya milioni 53 kwa wiki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles