Derick Milton, Simiyu
Ikiwa imepita mwaka mmoja tangu serikali kuanza kutoa vitambulisho vya ujasiriamali kwa wafanyabiashara wadogo wadogo (machinga) pamoja na wajasliamali, katika mkoa wa Simiyu wameeleza faida za mfumo huo.
Wakiongea na Mtanzania Digitali leo katika maeneo ya Lamadi, Dutwa na Bariadi wajasliamali hao, wamesema kuwa kuletwa kwa vitambulisho hivyo vimeondoa gharama kubwa walizokuwa wanatumia kulipa ushuru kila siku.
“ Mbali na kuondoa usumbufu wa kukimbiza na mgambo kila siku, lakini zile gharama za ushuru kila siku hakuna sasa hivi, tunafanya biashara kwa amani, kwa wiki mimi nilikuwa natumia 20,000 ushuru tu, leo nalipa ela hiyo kwa mwaka,” amesema Agness Laulian mjasliamali Lamadi.
Naye Janeth Masunga muuza nguo katika manada wa Dutwa, amesema kuwa katika kazi yake hiyo kwa wiki utembeza nguo kwenye minada mitano, na kila mnada alikuwa anatozwa sh.1000 hivyo minada yote alitakiwa kulipia sh. 5000.
“Kwa gharama hizo ndani ya mwezi unalipa 20,000, leo hii nalipa kiasi hicho kwa mwaka, tunashukuru Rais kwa kuja na mbinu hii, hatusumbuliwi, mtu unafanya biashara kwa amani, mitaji yetu imeongezeka,” amesema Janeth.
Nao Wafanyabishara wa samaki katika soko la Bariadi, walisema kuwa mfumo wa kitambulisho umekuwa bora zaidi kuliko ushuru ambao walikuwa wakilipa kila siku ambapo wameomba usisitishwe.
“ Vitambulisho hivi vimetupa unafuu zaidi sana, kila siku humu sokoni ilikuwa kukimbiza na mgambo, leo mtu unalipa kwa mwaka tu, tunaomba mfumo wa vitambulisho uendelee usisitishwe hata kidogo, tulikuwa na hali mbaya leo hii tunafurahia kazi yetu,” amesema Njigeilele Mhuli.
Hata hivyo baadhi ya wajasliamali katika mgodi wa Bulumbaka Gasuma Wilayani Bariadi, wakaomba serikali kuboreshewa vitambulisho hivyo kwa kuwekewa majina ua picha zao ili kuepuka usumbufu wa kuibiwa.
Afisa Biashara Wilaya ya BARIADI Dalali Stephano amesema mwaka huu wamepata jumla ya vitambulisho vya wajaslimali 9000 na mahitaji yamekuwa makubwa.