29.2 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Kigwangalla ateta na mabalozi

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amesema kuwa Tanzania imejipanga na iko tayari kupokea watalii kutoka katika mataifa mbalimbali, ikiwemo nchi za Sweden na Israel ambazo raia wake wamekuwa wakitembelea vivutio mbalimbali vya utalii vya Tanzania.

Dk. Kigwangalla ameyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Ulf Kallstig na Balozi wa Israel kwa Tanzania, Oded Joseph ikiwa ni mwendelezo wa mikutano yake na mabalozi wa nchi mbalimbali ambazo ni masoko makuu ya utalii kwa Tanzania.

Katika kikao hicho, aliwaeleza mabalozi hao kuwa mikutano anayoifanya na mabalozi wa nchi mbalimbali inalenga kulinda uhifadhi na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu hatua zilizochukuliwa na Tanzania kufungua sekta ya utalii wakati huu wa janga la corona na kuwaomba mabalozi hao wawahamasishe na kuwashawishi raia wa nchi zao na kampuni za utalii waendelee kufanya biashara ya utalii na Tanzania.

Aliwaambia mabalozi hao kuwa Tanzania imekwisha fungua anga na kuruhusu ndege za abiria za kimataifa kutua hali iliyochangia kufunguka kwa sekta ya utalii kutokana na utayari, mazingira salama na maandalizi mazuri ya kupokea na kuhudumia  watalii  watakaowasili nchini wakati huu wa janga la corona.

Dk. Kigwangalla alisema kuwa Tanzania imezindua mwongozo wa taifa wa uendeshaji wa shughuli za utalii  unaosimamia usalama na afya za wadau wote wanaojihusisha na sekta ya utalii wakati huu wa janga la corona.

Aliwahakikishia mabalozi hao kuwa watalii wote wanaowasili Tanzania katika kipindi hiki cha janga la corona wako salama kutokana na uwepo wa mwongozo huo unaolinda afya za wasafiri kuanzia kuwasili na kuondoka kwao.

“Mwongozo huu unatoa usimamizi kwenye viwanja vya ndege, hoteli za kitalii, watoa huduma za utalii, upimaji wa afya za wahudumu na wageni wote wanaoingia nchini pamoja na ukusanyaji wa taarifa za wasafiri wote wanaoingia nchini Tanzania,” alisema Dk. Kigwangalla.

Aidha, amewahakikishia mabalozi hao kuwa mifumo ya huduma za afya nchini imeimarika na iko tayari kuhudumia watalii watakaokuwa wakiwasili kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii, akibainisha kwamba Tanzania ina hospitali za kisasa, maabara za upimaji zenye vifaa vyote  na huduma za dharura kwa watalii watakaoshukiwa au kuonyesha dalili za ugonjwa wa corona.

Kwa upande wao, mabalozi hao wakizungumza kwa nyakati tofauti wamemshukuru Dk. Kigwangalla kwa hatua na juhudi anazozifanya kuendeleza uhifadhi nchini na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za uhifadhi.

Katika juhudi zake za kuhamasisha na kufungua sekta ya utalii, Dk. Kigwangalla ameshakutana na kuzungumza na mabalozi wa nchi mbalimbali ikiwemo Ujerumani, Israel, Sweden, Uholanzi na Finland.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles