28.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

Waathirika dawa za kulevya wafika 350,000

Na Amina Omari -Tanga

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema kwa sasa nchini kunakadiriwa kuwa na waathirika wa dawa za kulevya  kati ya 200,000 hadi 350,000.

Akizindua huduma ya Methadone mkoani Tanga jana, Ummy alisema kati ya waathirika wote wa dawa za kulevya, 30,000 wanatumia kwa njia ya kujidunga na asilimia 35 wanakadiriwa kuwa na maambukizi ya VVU.

Ummy alisema kiwango hicho ni kikubwa mara tano zaidi ya kiwango cha maambukizi kwenye jamii.

Aidha alisema hali ya maambukizi mapya katika kundi hilo kwa sasa yamepungua hadi kufikia mdungaji mmoja katika kila 10 wanaojidunga ikilinganishwa na wanne kati ya 10 kwa mwaka 2014.

“Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2016, unaonyesha Mkoa wa Tanga una zaidi ya waathirika 5,190 na hivyo kuufanya kuwa wa pili kwa kiwango cha maambukizi,” alisema Ummy.

Alisema Mkoa wa Tanga una idadi kubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya hali inayosababisha ongezeko la watumiaji kutokana na uwepo wa mazingira chochezi ya utumiaji tofauti na mikoa mingine nchini.

Ummy alisema kutokana na changamoto hiyo, Serikali ndipo ilipoamua kuja na tiba ya bure ya dawa ya methadone kuhakikisha tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya.

“Lengo la Serikali ni kufungua vituo vingine sita katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi mpaka ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, ili kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi,” alibainisha Ummy.

Katika hatua nyingine, Ummy alizindua mwongozo wa matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya ambao utatumika nchini nzima kwa kuwatibu waathirika hao.

Kwa upande wake, Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), James Kaji alisema kuwa uwepo wa kituo hicho ni mpango wa kuweza kufikisha huduma kwa walengwa kwa haraka.

Alisema kuwa ufunguzi wa kituo hicho ni mwendelezo wa uwepo wa vituo nane ambavyo tayari vinatoa huduma kila siku kwa waraibu wapatao 8,500 kila siku.

Hata hivyo aliishukuru Serikali kwa kuja na mtaala wa athari za dawa za kulevya utakaoanza kufundishwa mashuleni kuanzia darasa la tatu hadi sekondari, ambao utaweza kusaidia kutoa elimu ya janga hilo.

Nae Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Tiba na Afya barani Afrika (Amref), Dk. Florence Temu alisema kuwa wameamua kuunga mkono jitihada za Serikali za kupambana na tatizo hilo kwa kuanzia na uanzishwaji wa kituo cha muda ambacho kimegharimu Sh milioni 14.

Alisema kuwa uwepo wa huduma hiyo utaweza kusaidia jamii ya wana-Tanga ambao walikuwa wanahitaji huduma hiyo kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Donathan Budemu alisema kuwa hadi kukamilika kwa jengo hilo, Serikali inatarajia kutumia Sh milioni 786.

Aliwaomba wananchi pamoja na wadau wengine kuwashawishi  waathirika wa dawa za kulevya waweze kufika kwenye kituo hicho kupata huduma za tiba na ushauri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles