27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Meya wa zamani Arusha amwandikia barua JPM

Na JANETH MUSHI -ARUSHA

ALIYEKUWA Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro, amemwandikia barua maalumu ya shukrani Rais Dk. John Magufuli, kwa kile alichosema ni kumshukuru kwa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa jijini hapa na Serikali ya awamu ya tano.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini hapa, Lazaro alisema ameamua kuandika barua hiyo ambayo itaambatana na muhtasari unaoelezea utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuanzia mwaka 2015 hadi 2020.

Lazaro ambaye alikuwa Meya wa Jiji la Arusha kwa tiketi ya Chadema, alikihama chama hicho Novemba mwaka jana na kujiunga na CCM.

Alisema katika jiji hilo aliasisi bajeti ya mwaka 2015/16, 2016/17, 2017/18, 2018/19 na 2019/2020 ambayo inaisha Juni 30, hivyo utekelezaji wa shughuli za miradi ya maendeleo ulikuwa mikononi mwake.

“Nimemwandikia Rais barua ya shukrani kwa niaba ya wananchi wa Jiji la Arusha, nafanya hivi kwa sababu pengine hakuna mtu atapata fursa ya kueleza haya.

“Namshukuru kwa sababu ya kauli yake akihutubia Bunge, alisema maendeleo hayana chama wala itikadi, mnakumbuka Jiji la Arusha lilikuwa na mbunge wa Chadema, meya na naibu meya wa Chadema na madiwani wa Chadema 24, wa CCM alikuwa mmoja, ila Rais hajabagua maendeleo kwa sababu ya itikadi.

“Nimeandika barua rasmi kumshukuru kwa fedha na miradi ya maendeleo, naambatanisha na muhtasari wa miradi iliyotekelezwa, nitatuma kwa ndege ziende Ikulu.

“Naona hata halmashauri zilizoongozwa na upinzani hakuna hata moja ambayo haijapata miradi ya maendeleo, hivyo ni muhimu kushukuru,” alisema Lazaro.

Alisema mwaka huu wananchi wa Jiji la Arusha wana deni kwa kuhakikisha wanaongoza kura nyingi za Rais.

 “Mwaka 2015 hakupata kura za kutosha kwa sababu ya wimbi lililokuwepo, lakini mwaka huu na kwa vile mimi ni meya mstaafu na nimeingia CCM niko naye, uchaguzi huu Jiji la Arusha tutaweka rekodi kwenye kura za Rais,” alisema Lazaro.

Akieleza mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitano, alisema kati ya mwaka 2015 na 2020 vikundi vya wanawake vilipata mikopo zaidi ya Sh bilioni 4.23 ambapo wanawake 840 wamenufaika huku pia vijana 595 wakipata Sh bilioni 3.1 na walemavu Sh milioni 142.5.

“Katika sekta ya elimu, madarasa 137 ya shule za msingi yamejengwa, madawati 3,118, matundu ya vyoo 282 yamejengwa katika shule za msingi,” alisema Lazaro.

Alisema katika kipindi hicho halmashauri hiyo ilipokea na kutumia Sh bilioni 99.1 kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo mapato ya ndani Sh bilioni 33.3 na Sh bilioni 65.7 kutoka Serikali Kuu na wahisani.

Lazaro alisema pia kamera za ulinzi (CCTV) zimefungwa katika mizani za halmashauri, uhuishaji wa taarifa kwenye kanzi data ya wafanyabiashara na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa ulipaji wa tozo, ushuru na mapato mengine ya wafanyabiashara.

Akizungumzia madai ya kutajwa kuwania ubunge Jimbo la Arusha Mjini, alisema kwa sasa hajatangaza nia.

“Mimi kuhusishwa na nafasi yoyote bado sijatangaza nia, ikifika wakati sijui watu tutasikiliza sauti ya Mungu, ila sijasema nagombea chochote bado,” alisema Lazaro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles